ANA KWA ANA: Upekee wa ufundi wa magari unategemea ari ya mtu sio jinsia
Na WANGU KANURI
ZAMANI kazi ziliainishwa kwa msingi wa jinsia.
Ilikuwa mwiko kwa mwanamke kufanya kazi ambazo zilikuwa zimezoeleka kuwa za kiume na sawia mwanamume kufanya kazi zilizotambulika kuwa za kike.
Hali kadhalika, ujeo huu upya wa karne ya 21 umeivunja miiko hii na hata ingawa mtazamo huo bado umekolea kwa wengine, asilimia kubwa ya watu wamekubali mabadiliko hayo. Ninakutana naye Thogori Ng’ang’a ambaye amebobea katika ufundi wa magari na ambaye ameamua kutambulika sio kwa jinsia yake bali katika kazi yake kuntu.
Tueleze kwa kifupi, wewe ni nani?
THOGORI: Thogori Ng’ang’a ni kifungua mimba katika familia ya watoto watatu wa bwana na bi. Ng’ang’a. Nina umri wa miaka 30 na nina gereji ya magari iliyoko Industrial Area, jijini Nairobi. Katika ukurasa wa Facebook, tunaweza kuwasiliana kupitia TK_Auto Garage.
Aliyekuchochea kupenda kuzikarabati magari ni nani?
THOGORI: Baba yangu aliisisimua ari yangu ya kupenda kutengeneza magari. Alinifunza kutengeneza redio, televisheni na vifaa vingine vya kielektroniki. Baadaye alileta pikipiki ambazo tuliweza kutengeneza pamoja. Hatima yangu kuweza kupata ufundi huu wa kipekee ulijidhihirisha wakati ambapo nilijiunga na shule ya Dobie ambayo baada ya mahojiano kadha wa kadha na wakurugenzi wa shule hiyo, nilipata nafasi ya kusomea taaluma ya ufundi wa magari.
Jamii imeweza kutofautisha kazi kwa jinsia. Je, wewe unahisi vipi kama fundi wa kike wa magari?
THOGORI: Kitambo watu waliweza kushutuka walipompata mwanamke akifanya kazi ambazo zilikuwa zimetengewa wanaume, lakini sasa nyakati zimebadilika. Mtazamo huu umewafanya wengi kutoangazia sana suala la jinsia bali utaalamu alionao mtu. Mimi kama fundi wa kike nimejiimarisha katika kazi yangu na hiyo imenifanya kuwa gwiji katika sekta ya ufundi wa magari kiasi cha kuwavutia wateja wengi.
Changamoto unazopitia katika kukarabati magari ni zipi?
THOGORI: Nimekuwa katika kiwanda hiki cha ufundi wa magari kwa takriban miaka 12. Nilipoanza watu hawakuwa wanaamini ujuzi wangu kiasi cha kwamba nikaanza kujishuku. Kutokuwa na uhakika katika kazi hii kuliimarishwa sana na mtazamo potovu kutoka jamii kwani ufundi wa magari hufanywa sana na wanaume. Hii kwangu imenifanya nihisi kuwa lazima nifanye kazi maradufu kuliko wanaume wenzangu hata ingawa nimefanikiwa.
Unajivunia nini kama fundi wa magari?
THOGORI: Cha kujivunia ni kwamba nimeweza kuwapa moyo na motisha wanawake kwani nimeufanya ufundi wa magari kuwa pahala pangu pa riziki na kujiimarisha hapo. Isitoshe, kutokufa moyo japo lazima nifanye kazi maradufu zaidi ya wanaume kumenipa ari ya kuendelea.
Kwa kuelewa vyema kuwa kazi yako inafanywa na wanaume wengi kuliko wanawake, je ni nini cha kipekee ambacho wewe hufanya ili uwapate wateja?
THOGORI: Mimi hukakikisha kuwa kila mteja wangu amejua hitilafu katika gari lake na kumweleza kile ambacho nitakuwa nikifanyia gari lake ili kulikarabati.
Ufundi wa magari hasa kwa jinsia ya kike ni kazi ambayo haijavuma. Je, unaweza washauri vipi wanawake?
THOGORI: Takribani kila nyanja ina wanaume wengi kuliko wanawake kwa hivyo cha muhimu ni kuelewa kuwa haupo katika shindano na wanaume bali katika kuifanya kazi yako kwa upeo wa uwezo wako.
Ni magari yepi ambayo umebobea kutengeneza?
THOGORI: Nilipokuwa katika chuo cha uhandisi nilifunzwa kutengeneza magari aina ya Mercedes, Jeep na Nissan lakini baada ya kujiajiri, nimejua kutengeneza magari ya Volkswagen, Audi, BMW na Toyota.
Taaluma ya ufundi wa magari imedunishwa. Hisia zako ni zipi kuhusu suala hilo?
THOGORI: Binadamu amefunzwa kuwa kazi ambayo mtu anapata uchafu kutoka kwake si nzuri lakini dhahabu inapatikana kwenye uchafu. Hali kadhalika, usafiri ni kigezo kikuu cha ustawi wa rasilimali za nchi yoyote ile na kama fundi wa magari ninajihusisha kufaulisha hili japo si moja kwa moja.
Unalenga nini katika siku zako za usoni?
THOGORI: Ninaangazia kuanzisha shule ya ufundi wa magari kama shukrani kwa jamii. Vile vile ninanuia kupanua gereji yangu.