ANA KWA ANA: ‘Ustaa ulifanya nihisi spesho na najuta sana’
Na THOMAS MATIKO
HIVI unamkumbuka mwigizaji mcheshi Dennis Mugo au ukipenda OJ?
Alipata umaarufu mkubwa sana kupitia kipindi cha Tahidi High ila toka alipoondoka kwenye kipindi hicho, stori yake nayo ikazima.
Tetesi za yeye kung’oka kwenye shoo hiyo zilidai kwamba alifukuzwa kutokana na kupenda kukata maji au ukipenda ulevi. Safu hii ikiwa kwenye mishe mishe za mjini kusaka stori , iligongana naye na gumzo likawa kama hivi
Hebu tuanzie mwanzo, ulikozaliwa na kulelewa?
OJ: Nilizaliwa Molo, nikasomea Nyahururu Elite masomo ya msingi kisha Nakuru High kwa ajili ya sekondari na baada ya hapo nikajiunga na Chuo cha uanahabari cha Kenya Mass Communication na kutoka hapo kila kitu kilichonihusu mimi kilihusiana na TV.
Umaarufu ulikukuta ukiwa bwana mdogo, hivi ulikuathiri vipi?
OJ: We acha tu, nilivimba kichwa. Ule ustaa ulinivurugia mawazo na kunifanya kujiona mtu ‘spesho’ sana. Niliringa sana, kitaani nilikuwa naiona dunia kama yangu vile. Si wajua tena ujana bwana. Mademu nao niliwafyeka sana sababu nilikuwa na pesa. Wengine niliwazengulia hasa wale walionikataaga kipindi nikiwa sina kitu. Nilishindwa kutofautisha kazi na umaarufu. Ilinichukua muda kuja kujielewa.
Unasema uliwahangaisha mademu?
OJ: Kwa saana tu mzee halafu nilikesha sana baa. Niliishi kwenye maisha ya anasa muda mwingi. Kila nilichowaza zaidi ya kazi, lazima ingekuwa starehe.
Ulipogutuka?
OJ: Nilikuja kugutuka baadaye na kubaki nikijuta tu. Starehe ina gharama mzee, nilipoteza fedha nyingi ambazo kama ningewekeza au kuweka akiba, leo ingenisaidia kupiga hatua zaidi. Wajua unapokuwa celeb unapoteza maisha yako ya uhalisia. Huwezi kuishi kama wewe ila unalazimika kuishi jinsi jamii inavyokuona, sasa usipokuwa makini unapotea kabisa sababu unakuwa unaisha maisha sio yako.
Kwenye harakati hizo pia skendo uliziamsha sana, ipi ilikutikisa?
OJ: Ukiachana na kuzushiwa kifo kama mara kama nne, niliripotiwa kuwa nimeaga dunia. Taarifa hizi ziliitesa sana familia yangu. Skendo nyingine iliyonitesa ni ishu kwamba nilikuwa mtumizi wa madawa ya kulevya. Ndio kulewa nililewa lakini utumizi wa maunga wala hata siku moja, sikuwahi kulamba poda.
Kulewa huko hakukuwa kwa kawaida pengine ndio sababu za tetesi hizo?
OJ: Sijawahi kuwa mtumwa wa pombe ila kuna vipindi nililewa kwa kupitiliza. Lakini pamoja na matukio hayo, sijawahi kupelekwa rehab kisa kuwa mtumwa wa pombe, haijawahi kufikia levo hiyo.
Pia tetesi zilidai kwamba ulevi ndio ulikupelekea kupoteza kazi Tahidi High?
OJ: Kuondoka kwangu Tahidi kulitokana na kudumisha uhalisia wa kipindi. Tulikuwa kwenye shoo hiyo kwa zaidi ya miaka sita hivyo ili kudumisha uhalisia wake ilikuwa bora zaidi kama tungefuzu na kumaliza kidato.
Baada ya Tahidi ukaingia mitini?
OJ: Nilikwenda kufanya kazi kwenye kampuni moja ya matangazo Triple H Media; sema uigizaji nikaacha kidogo.
Baadaye ulirejea kwenye kipindi kama mwalimu?
OJ: Baada ya kuondoka Tahidi nilijiendeleza zaidi na masuala ya uandaaji filamu na uzalishaji vipindi. Lengo langu halikuwa kurudi tena Tahid High ila ilitokea kama ajali vile. Ipo siku tulikuwa tunatia stori na mwelekezi kipindi ndipo akanipendekezea wazo la kurudi kama mwalimu ukizingatia kwamba nilikuwa naelewa maisha ya shule ile. Nikaona isiwe kesi na kurejea.
Kisha kulitokea stori kwamba ulioa?
OJ: Hehehe! Yule ni mama wa mwanangu, tulikutana zamani kidogo nikiwa naigiza pale Tahidi kama mwanafunzi. Uhusiano wetu ulidumu kwa takribani miaka sita saba hivi na ndipo tukaweza kujaliwa kumpata mtoto wetu wa kwanza ambaye sasa ana umri wa miaka mitano.
Toka umepata mpenzi na familia, uliacha kula bata?
OJ: Nilipunguza mzee, sio kama zamani ila mara nyingi lazima tutoke na washikaji kubadilishana mawazo na muda mwingi unakuta mazungumzo yetu yanazunguka kwenye masuala ya familia au biashara zetu.