Makala

ANA KWA ANA: Washikaji walioleta nguvu mpya kwenye gemu

November 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na THOMAS MATIKO

TASNIA ya muziki wa Kenya inazidi kukua japo kwa utaratibu katika nyanda tofauti tofauti.

Upande mmoja wa tasnia unaozidi kuimarika ni kunoga kwa ushindani kutokana na vipaji vinavyoibuka kile leo.

Mojawepo ya vipaji vya hivi karibuni kuchipuka na kuja kufanya vyema ni Ndanah Miqasaa na Spizzoh, wasanii wawili washikaji kutokea Pwani wanaofanya kazi za pamoja na pia zao mbali mbali.

Kwa muda sasa toka wajitambulishe kwenye gemu, baadhi ya kazi zao zimeweza kutrendi ikiwemo Kidege, Wenge, Lolo, Nipe namba kati ya nyinginezo. Kwa kutaka kuwafahamu zaidi na kuelewa nguvu hii waliyokuja nayo kwenye gemu, safu hii iliwaibukia:

Spizzo na Ndanah ndiyo majina yenu kamili au?

Hapana mimi naitwa Yusuf Kazungu aka Spizzo. Nami ni Mohammed Karisa ukipenda Ndanah.

Hivi mlikutanaje au mna undugu?

Spizzoh: Wala, mimi na huyu bwana safari yetu ilianza 2011 tulipokutana kwenye freestyle battle ya Nokia Don’t Break the Beats kule Mombasa, nikaibuka bingwa huyu akawa wa pili. Baada ya hapo tukaja kukutana tena kisadfa Dar es Salaam ambapo akina mama zetu wanaishi na hata cha ajabu ni majirani kwenye mtaa huo. Nilikuwa nimekwenda kumcheki mama kumbe naye Ndanah akawa huko toka hapo tukaanza kuwa na ile koneksheni ukizingatia kwamba wote pia ni wanamuziki. Ni kipindi hicho tukiwa Dar kulitokea freestyle battle nyingine huko safari hii ikiwa ni ya fiesta, na kati ya watu 500 sisi wawili ndio tuliibuka washindi. Baada ya hapo kuna mmoja wa maprodusa waliyemsaidia Diamond kutoka anaitwa Lamar akatusaini.

Kwa hiyo muziki mlianza 2011 ila mumekuja kutambulika hivi majuzi?

Ndanah: Baada ya hapo tulirejea Kenya, mimi nikahamia zangu Nairobi mwenzangu akarudi Mombasa kumalizia masomo yake. Alipohitimu akanifuata Nairobi na kupata tayari nilikuwa nishaachia ngoma mbili.

Kwa nini mkakurupukia Nairobi, hata Mombasa muziki mngefanya bado tu?

Ndanah: Wajua ukiwa Mombasa, au wapi kule gemu ya muziki wa Kenya inaendeshwa na Nairobi kwa sababu redio nyingi ziko hapa, na kila kitu kinachohitajika kutengeneza na kusukuma muziki.

Nafikiri huo ni mtazamo wenu tu kwa sababu mtu kama Susumila muda wote yupo Mombasa ila ni mkubwa hata Nairobi?

Spizzoh: Wajua Susumila ni msanii mkali sana lakini pia ukiachana na jitihada zake na anavyojituma kuna ile kasumba ya kuwa msanii wa Nairobi ni wa Nairobi na wa Mombasa ni wa Pwani na vitu kama hivyo. Ila sisi hatutaki kujiwekea vikwazo kama hivyo, kwa mfano ukimwangalia mtu kama Diamond, haipo siku utamsikia akitaja anakotokea japo ni jamaa wa Tandale, anasema ni msanii wa Tanzania. Hajajiwekea vikwazo na ndivyo tunavyotaka sisi kuwa, twataka muziki wetu ukwende mbali.

Hivi nitakuwa sahihi kusema Ndanah na Spizzo ni kundi?

Ndanah: Usiweke kihivyo sisi ni wasanii wawili tofauti ila tukiwa pamoja kwa sababu tuna ile koneksheni inakuwa rahisi kujisukuma kimuziki ukizingatia pia kwamba sisi ni wasanii chipukizi. Hivyo huwezi kusema sisi ni kundi kwa sababu hatuna hata jina la kundi lenyewe unaona tunatumia majina yetu ya stejini kila mmoja. Tupo kama ile kombinisheni ya zamani ya Khristoph na Khaligraph kipindi wanaanza.

Mliwahi kudai kuwa wimbo wenu wa ‘Wenge’ uliibiwa na Otile Brown na Timmy wakatoa ‘Wembe’?

Spizzoh: Hatutaki ionekane kama vile ni kiki ila ukisikiza kazi zote hizo utajijazia mwenyewe, kutoka kwa mdundo na baadhi ya mashairi Otile aliusampo wimbo wetu kabisa ila hamna neno kwa msanii mkubwa kuchukua kazi yetu na kukopi inaonyesha kuwa tunafanya vitu vya maana. Kinachouma zaidi ni kwamba tulipomfuata tufanye remix kolabo ya wimbo huo alituitisha Sh200,000 na hatukuweza kuendelea ila sio ishu tena tuliachia ipite.

Kazi yenu ‘Kidege’ imekuwa kubwa sana; imewafungulia milango gani?

Spizzoh: Kwa kweli imetufungulia milango kadhaa kwa mfano hapa tunapofanya mahojiano na wewe, ni fursa nzuri kwa sababu mwanzoni hukuwa ukitufahamu japo tulikuwa tayari tumeachia kazi kadhaa. Pia imetupa umaarufu, koneksheni kibao na katika hapo imesababisha milango mingine zaidi kufunguka.

Huo umaarufu mmenufaikaje?

Ndanah: Imetuwezesha kupata shoo kibao kote nchini, watu wengi wametufahamu, mapromota wanatusaka na pia wasanii wengine wakubwa wametufikia na tukaweza kufanya kolabo kama vile Nairobi, Bruce Melody miongini mwa wengine. Pia koneksheni za nje za nchi tumeweza kupata.

Labda kwa kumalizia, ni kwa nini wasanii wengi wa Mombasa wanapopata umaarufu kidogo, inawaingia kichwani wanaishia kuvimba vichwa na mwishowe wanapotea?

Spizzoh: Kuna kasumba kuwa wasanii kutoka Mombasa wana uzembe fulani, wakitoa hiti moja, jina linakuwa kubwa, anapata posho zuri, interview kibao wanalegea kwa kuona wamefika na katika hilo anatokea msanii mwingine anaichukua nafasi hiyo na wao wanapotea.