ANA KWA ANA: Zaidi ya mwongo sasa na bado anatesa aisee!
Na THOMAS MATIKO
JUDITH Nyambura Mwangi al-maarufu Avril ni mwanamuziki wa siku nyingi tu. Toka aingie kwenye gemu, ni zaidi ya mwongo sasa.
Umaarufu wake umechangiwa pakubwa na urembo wake, sikwambii utanashati pamoja na baadhi ya skendo zilizomkuta hapa na pale. Unaweza ukampenda au ukamchukia hiyo ni shauri yako. Ila hilo haliwezi kuathiri umaarufu alionao na mkwanja anaopiga.
Safu hii ilimwibukia akiwa kwenye pilikapilika zake jijini Nairobi na kuchonga naye.
Umezamia sana kwenye dili za biashara-matangazo, muziki kidogo hatukuoni kama zamani ni kama vile huko ndiko unapiga mkwanja sana siku hizi?
Avril: Hapana, sio kweli. Dili nilizonazo za kutangaza bidhaa mbalimbali ni sehemu moja tu ya kuingiza kipato. Bado muziki wangu unalipa sababu napata shoo. Wajua miaka mitano nyuma, suala la biashara matangazo halikuwepo hadi mitandao ya kijamii iliposhika kasi na baadhi yetu wasanii tukaishia kupata ufuasi mkubwa unaotumiwa sasa na kampuni hizi kujitangaza na katika hilo, nasi tunafaidi.
Kwa sasa upo kwenye mkataba wa kimatangazo na nani?
Avril: Ninawatangaza Oppo, mojawapo ya kampuni kubwa za simu duniani. Wameshusha mzigo mpya sokoni Oppo F11Pro ambao ni simu ya kijanja sana unastahili kuijaribu uone matokeo.
Lakini pia umejitosa kwenye uigizaji, ndiko kusaka hela eti eeh?
Avril: Acha nikuambie kitu; wala sikupania naweza kuwa mwigizaji, ilitokea tu. Kama wakumbuka ile Series ya Shuga ‘Season One’ ndio mara ya kwanza nimepata fursa ya kuigiza. Ilikuwa ni kwenye majaribio ya rafiki yangu Anto Neosoul aliyeniomba niandamane naye, kufika kule wale maprodusa na waelekezi wakanishawishi nijaribu na bahati ikaniangukia, wakanikubali licha yangu kuwaambia sijawahi kuigiza. Ndivyo safari yangu ya uigizaji ilianza na nimeishia kutokea kwenye filamu ya World Tofauti na kipindi cha Sumu la Penzi.
Wapo watakaohoji kuwa ulipewa fursa kutokana na urembo wako na sio kwa sababu unastahili?
Avril: Lazima wakosoaji wawepo na kama huna wa kukutoa rangi, basi ina maana kuwa kuna vitu unavyofanya ambavyo havijakaa sawa. Lakini pia usisahau kwamba kunao pia mahasidi wenye roho mbaya. Wanahitaji kujielewa hawa.
Bifu yako na Naiboi mmeimaliza?
Avril: Yule ni mshikaji wangu wa siku nyingi na nimeshakutana naye mara kadhaa nikamuuliza tatizo nini akaniambia nikanyagie stori. Wajua alipokuwa akiandaa video yake ya 2 in 1 na akaniomba usaidizi ndio pia nami nilikuwa nimejifungua mwanangu na nilikuwa naendelea kupona baada ya kufanyiwa upasuaji. Kikweli sikuwa kabisa kwenye hali ya kujihusisha na muziki. Baadaye wakati natokea kwenye video ya Otile, siku zilikuwa zimepita na nikawa nimeyakubali yale mazingira mapya. Sijui kama umenielewa!
Pia uling’oka Kaka Empire, ilikuwa kwa uzuri au kwa hila?
Avril: Nilikuwa na mkataba nao wanisimamie. Ulikuwa ni wa mwaka mmoja kisha tukauongeza kwa mwaka mwingine. Baada ya hapo nikawa nimeunda timu iliyoonelea ni bora sasa tujitoe ili tuweze kufanya mambo kivingine, zaidi ya hivyo niliondoka kwa uzuri mkataba huo ulipofikia kikomo.
Umemtaja mwana wako, kuna tetesi kuwa ulikausha dili iliyomtaka naye ahusike?
Avril: Ni kweli, ilikuwa dili ya dola 1,000 (Sh1 milioni) na pamoja na babake tulikubaliana kwa kauli moja kuipiga chini. Lengo letu ni kumlinda M kwa hali zote ili aweze kuwa na maisha yake.
Ndio sababu ya kumficha mpaka jina?
Avril: Ndio sababu. Hata mimi mwenyewe sikuzaliwa kwenye umaarufu. Umenikuta; nimejifunza mengi. Katu siwezi kutamani mwanangu atembee njia hiyo. Najua itatokea siku mtamjua ila kwa sasa acha nibaki kumficha.
Babake M, J Blessing mzima?
Avril: Hahahaha! Naona unavyojaribu kuyapinda mambo. Alikwaambia yeye ndio babake mwanangu? Ishu ya baba wa mtoto wangu kamwe sitawahi kuizungumzia sababu haina umuhimu. Najua watu wanapenda kuyafuatilia maisha yangu ila mengine nafikiri bora niyabanie kabisa.
Kwa hiyo utakuwa upo singo?
Avril: Nani kasema, nina mtu mwenzio.
Umewazia kupata mtoto wa pili?
Avril: Kwa kweli natamani sana pamoja hata na ndoa ila kwa sasa nimeachia Mungu, binadamu hupanga yeye akaamua.