Anaeleza ilivyo muhimu kuzingatia kilimo-hai na asilia
Na SAMMY WAWERU
CHAKULA kinachoenziwa na kuliwa kwa wingi ni kilichosindikwa (processed).
Baadhi ya vyakula vya kusindikiwa aghalabu hutiwa kemikali ili kuvihifadhi kwa muda.
Wataalamu wa masuala ya afya huonya dhidi ya kuvila sana kwa sababu ya athari zinazoibuka siku za usoni, uuguaji wa magonjwa kama Jongo, Kisukari, Shiniko la Damu na Saratani miongoni mwa mengine.
Takwimu za idara ya afya kwa ushirikiano na wadau husika zinazotolewa kila mwaka, zinaonesha magonjwa hayo ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo nchini.
Aidha, wataalamu wa masuala ya afya wanasema yanaweza yakadhibitiwa kwa kiwango kikubwa iwapo kila mmoja atazingatia mlo kamili.
Isemwavyo; kinga ni bora kuliko tiba, ulaji wa matunda ainati, uzingatiaji wa chakula asilia na kile hai, ni baadhi tu ya unachohimizwa kutumia mara kwa mara.
Mbali na kuwa mtaalamu wa kilimo, Bw James Macharia ni balozi wa siha bora kupitia jitihada zake za zaraa ya kipekee.
Ukizuru Green Oasis Plants Centre huko Kabati, kaunti ya Murang’a, pembezoni mwa lango utakaribishwa na mimea mbalimbali ya kusawazisha hewa chumbani maarufu Indoor Air Cleaners, yenye maumbo sawa na maua.
Spider plant, Areca Palm, Peace plant, Mothers-in-law palm, Boston Fern na Rubber plant, ni baadhi tu ya mimea hii anayokuza Bw Macharia.
Mazingira ya makazi tunayoishi, aghalabu kiambaza hupakwa rangi zilizochanganywa na bidhaa za petroli, jokofu, vifaa vya plastiki vya kulia na kunywa, chupa za vinywaji, na mazulia, vyote kwa jumla vikiundwa kwa malighafi yasiyokosa kemikali.
“Nyingi ya bidhaa hizo inapozidiwa na kiwango cha joto huachilia gesi ya Carbon, Benzene na Formaldehyde. Kemikali hizo husababisha magonjwa kama ya Kansa, na mimea ya Indoor Air Cleanersimeumbwa na uwezo wa kuzivuta, na kuachilia hewa safi ya Oxijeni,” aeleza mtaalamu huyu.
Kusawazisha hewa ya nyumba
Shirika la usafiri wa Anga (NASA) mwaka wa 1989 lilifanya jaribio la mimea 50 katika safari yake kwa sayari mbalimbali, na kugundua inaweza kutumika kuzalisha Oksijeni badala ya ile ya kujiundia.
Utafiti wake pia uliashiria kwamba mimea hiyo ni bora katika kusawazisha hewa ya nyumba. Kiunga cha Bw Macharia na chenye ukubwa wa ekari moja na nusu kimesheheni miche ya matunda aina mbalimbali na miti.
Ukila tunda kwa siku husemekana “humuweka daktari mbali nawe”, amekipamba kwa matofaha, mapapai, mapera, tree tomato (ya kuongeza damu mwilini), zabibu, Brazilian cherry, bukini, maembe, ndizi, macadamia, hayo yakiwa machache tu kuyataja. “Matunda hudhibiti magonjwa ibuka. Jizoeshe angaa kula tofauti kwa siku,” ashauri Bw Martin Nderitu, muuguzi na mtaalamu wa masuala ya afya.
Isitoshe, Macharia amepanda mimea asilia inayokabiliana na matatizo ya tumbo, kudhibiti usambaaji wa Saratani, ugonjwa wa shinikizo la damu na Kisukari, nayo ni; Lemon grass, Herbal Hibiscuss, Mulberry na Herbal Rosemary.
“Nina mashine maalumu ya kuisaga inapokomaa, unga wake hutengeneza sharubati kwa kuuchanganya na maji moto na asali,” aelezea. Wataalamu wa afya hupendekeza viungo asilia vya mapishi vitumike, na mkulima huyu wa aina yake huvikuza na kuviunda.
Wakati wa mahojiano alifichua aina saba ya mimea anayolima, na kuunda bidhaa za aina mbalimbali akiitambua kama ‘mints’. “Kuna mints aina saba kila moja na matumizi yake. Tropical ni ya kuunda peremende, chokoleti (kando na kuunda chokoleti yenyewe, ni ya dawa za kupiga meno mswaki), pepper (mapishi), spear (kubadilisha rangi ya chakula), corsican(minukato), apple na orange pia zinatengeneza dawa za kupiga meno mswaki,” alifafanua.
Kilimo chake kimeegemea mimea yenye ukwasi wa madini ya Calcium, Potassium, Vitamini na Magnesium.
Macharia ambaye ni mzawa wa Nyeri, anasema mapenzi katika kilimo ameyapalilia tangu akiwa mdogo kiumri.
Akivuta mawazo yake nyuma, akiwa katika shule ya msingi alikuwa na kiunga kidogo alichopanda matunda na miti. Wavyele wake walifurahishwa na juhudi zake na hata kumpiga jeki.
Alikuwa na bahati kama mtende kwani shule ya upili aliyojiunga nayo ilitilia maanani masomo ya zaraa, ambapo alishiriki miradi kadhaa ya kilimo.
La kutia moyo, baada ya kuhitimu kidato cha nne ombi lake kujiunga na Chuo Kikuu cha Egerton, Nakuru liliitikiwa na akasomea Stashahada ya Kilimo-mseto, masuala ya mimea.
Safari ya mbali huanza kwa hatua moja, mdau huyu aling’oa nanga mwaka wa 2008 kwa kiunga kilichomgharimu mtaji wa Sh23,000 mtaani Kahawa Sukari, kaunti ya Nairobi. Aidha, kilikuwa pembezoni mwa Thika Super Highway, na mradi wa ujenzi wa barabara hii ulipoanza alilazimika kuondoka akahamia Ruiru, Kiambu mwaka wa 2009.
Changamoto kuu eneo hilo ilikuwa ukosefu wa maji, ikizingatiwa kuwa ufanisi katika kilimo unategemea kiungo hiki.
Mwaka wa 2010 alipata kiunga Murang’a, alichoko kwa sasa. Hata ingawa hakufichua mapato yake wakati wa mahojiano, alisema bei ya bidhaa zake ni kati ya Sh50-500.
Ameajiri wafanyakazi sita, na mitandao ya kijamii kama vile; Facebook, WhatsApp, OLX na Instagram imemsaidia pakubwa kupata soko la mazao yake.
Ili kufanikisha kilimo cha aina hii, anasema mkulima chipukizi sharti awe na chanzo cha maji ya kutosha na ambayo ni safi.
“Ni muhimu kujua kiwango cha asidi au kukosekana kwake (pH) katika mchanga.
Wakulima wanapaswa kutibu mchanga kwa kutumia lime na mboleahai-ya mifugo.
“Wajaribu kadri wawezavyo kupunguza matumizi ya pembejeo, ili uhifadhi virutubisho,” ashauri.
Kauli yake inawiana na ya Daniel Mwenda, mtaalamu wa kilimo, anayehimiza haja ya wanazaraa kufanya kilimo-hai.
“Chakula kitakuwa salama tukiepuka kutumia mbolea zenye kemikali,” asisitiza Bw Mwenda.