Anafuga nguruwe jijini Nairobi, mapato ni ya kuridhisha
NA SAMMY WAWERU
Sekta ya kilimo na ufugaji ni kati ya ambazo zinaendelea kutia tabasamu wanaoithamini na kuifanya afisi yao.
Mtaa wa Mumbi, takriban kilomita kumi kutoka Thika Super Highway na kiungani mwa jiji la Nairobi Esther Wanjiru amejibidiisha kuimarisha mradi wake wa ufugaji wa nguruwe.
Kwenye ploti anayomiliki, yenye ukubwa wa futi 100 kwa 100, ana zaidi ya nguruwe 30. Aliingilia shughuli hiyo 2016, ambapo alianza na nguruwe watano pekee.
“Ilinigharimu mtaji wa Sh18, 000. Nilinunua nguruwe watano, wanne wakiwa wa kike na mmoja wa jinsia ya kiume,” Wanjiru aelezea.
Ana mazizi mawili, moja ni la nguruwe waliozaa na lililogawanywa kwa makundi kadhaa kwa mujibu wa umri wa vivimbi – wana wa nguruwe, na pia lina sehemu ya anayewajibikia kujamiisha yaani nguruwe wa kiume.
Zizi la pili, nalo ni la walio na ujauzito kulingana na umri. Pia, lina eneo la mapishi ya mlo wa mifugo hao, analolitambua kama ‘jikoni’.
Ikizingatiwa kuwa ufugaji wa nguruwe ni kazi yenye shughuli chungu nzima na inayoaminika kufanikishwa na wanaume, Wanjiru ambaye ni mama wa watoto wanne anasema yeye ndiye hujifanyia majukumu yote.
“Mradi huu ndio afisi yangu ya kila siku, umeniajiri,” adokeza, akiendelea kueleza kwamba ufugaji wa nguruwe umemsomeshea wanawe, mmoja kwa sasa akiwa chuo kikuu. Binti zake wawili wamemfaa pakubwa, haswa wakati wa likizo ambapo humsaidia kwa gange za hapa na pale.
Asubuhi na mapema, anaporauka, hatua ya kwanza huwa usafi wa mazizi, vifaa vya kuwatilia chakula na maji. Hali kadhalika, hukagua walivyolala nguruwe wake, kubaini ikiwa kuna aliye na shida yoyote ile.
“Muhimu zaidi ni usafi wa mazingira wanamoishi na usafi wa wao wenyewe, pamoja na vifaa vyao vya kuwatilia mlo na maji,” asisitiza mfugaji huyo. Hadhi ya usafi ikiwa ya kupigiwa upatu, kero la usambaaji wa vimelea kama vile viroboto, kupe na minyoo na pia magonjwa limepungua.
Simon Wagura, mtaalamu wa masuala ya ufugaji anasema chanjo pia ni muhimu kwa nguruwe. “Wanapoonyesha udhaifu, shirikisha daktari au mtaalamu wa mifugo,” ashauri mdau huyo.
Magonjwa sugu kwa nguruwe ni Swine dysentery, Coccidiosis na Mastitis – hasa kwa wanaonyonyesha.
Esther Wanjiru anasema hulisha nguruwe wake mara moja kwa siku. Ili kupunguza gharama, huwalisha masalia ya chakula cha binadamu, matunda yaliyotupwa, karoti, pamoja na mboga na viazi.
Aghalabu, ni mlo unaopatikana katika mengi ya masoko nchini. “Ukitembelea masoko, hutakosa kutazama matunda, mboga, viazi na karoti zilizotupwa. Mazao hayo huyageuza chakula cha nguruwe,” asema.
Anapoyakusanya pamoja na masalia ya chakula cha binadamu, jambo la kwanza ni kuyaosha. Ana madramu kadhaa yanayochukua mahala pa sufuria, halafu anawapikia. “Kazi huwa kuwatafutia chakula na kuwapikia,” aeleza.
Mbali na mlo huo, pia huwalisha chakula maalum, aina ya unga wa nguruwe, ambao mfuko wa kilo 50 huuzwa Sh2,000. Anaeleza kwamba kwa siku nguruwe mmoja hula wastani wa kilo 1.5.
Anasisitizia haja ya kuwanywesha maji safi na kwa wingi. Isitoshe, mama huyo pia huosha nguruwe wake, katika mchakato mzima wa kudumisha kiwango cha usafi.
Wanjiru anasema ufugaji wake ni wa biashara, na vivinimbi wa kiume wanapozaliwa huwatoa uume. “Hilo linasaidia kuepusha kujamiisha waliozaliwa pamoja nao, ‘dada zao’ na pia kuimarisha ubora wa mifugo,” afafanua.
Ana nguruwe mmoja wa kiume, aliyemnunua nje. Aidha, idadi kubwa ni ya kike.
Nguruwe wa kike anapotungwa ujauzito, huzaa baada ya miezi mitatu wiki tatu na siku tatu. Mmoja huzaa kati ya vivimbi 6 – 12.
Wakati wa mahojiano, mfugaji huyo alisema mwana mmoja humuuza zaidi ya Sh3,000 huku nguruwe aliyekomaa akinunuliwa hata zaidi ya Sh10,000.
“Uhaba wa chakula ndio kizingiti kikuu kupanua ufugaji huu. Ningepata chakula kwa bei nafuu, ningetia saini mkataba na Farmers Choice (kampuni inayotengeneza soseji) ili kuimarisha soko na namna ya kuendeleza ufugaji kitaalamu,” akasema. Wateja wake ni wenye buchari kaunti ya Nairobi na Kiambu.
Iwapo angekuwa akihifadhi nguruwe tangu alipoanza, Wanjiru anasema angekuwa na maelfu ya mifugo hao, ila suala la chakula na uhaba wa ardhi haumruhusu.
Ili kuruhusiwa kuendesha ufugaji mijini, mkulima anapaswa kupata kibali kutoka kwa idara husika, kama vile wizara ya kilimo na ufugaji ngazi ya kaunti na halmashauri ya kitaifa ya mazingira, ndiyo Nema.
Hata hivyo, katika kaunti zinazofahamika kwa shughuli za kilimo, wengi wanaruhusiwa kuingilia ufugaji hasa ikiwa mifugo hawaachiliwi kujitafutia lishe.