Anavyogeuza taka kuwa mboleahai
IKIWA kuna msemo unaomfafanua vyema Richard Mwangi, basi ni huu: “Nipe tatizo, nitaligeuza kuwa fursa yenye thamani.”
Mwangi ndiye mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Organic Fields Ltd, kampuni inayojishughulisha na uundaji wa mboleahai kutokana na taka za chakula.
Kampuni hiyo iko katika eneo tulivu la Kwihota, Ruiru, Kaunti ya Kiambu, ambako taka za chakula hugeuzwa kuwa bidhaa muhimu kwa wakulima – mboleahai.
Safari yake imetokana na msingi wa tajiriba na malengo, ambapo baada ya kufanya kazi na wakulima, hasa wadogo, kwa zaidi ya miaka 10, Mwangi alishuhudia changamoto zao.

Ingawa serikali inaendelea kuweka mikakati kukabiliana na baa la njaa na kuhakikisha usalama wa chakula, mjasiriamali huyu anaamini kuwa suluhisho linaanzia kwa kuboresha mbinu za kilimo.
Isitoshe, anaona Kenya kuendelea kuagiza kutoka nje mbolea – hasa fatalaiza ambazo kwa kiwango fulani zimesheheni kemikali ndiyo changamoto kuu inayopaswa kuangaziwa.
“Kwa zaidi ya miaka kumi – muda ambao nilihudumia wakulima, niligundua afya ya udongo na mbinu bora za kilimo ndizo msingi wa kuongeza kiwango cha uzalishaji chakula,” Mwangi anasema.
Ni gapu hiyo na kuendelea kuharibiwa kwa udongo na vilevile mazingira kulimchochea kuasisi Organic Fields Ltd mwaka wa 2016.

Wazo lake lilikuwa rahisi lakini lenye mashiko kwenye mtandao wa kilimo – kuunda mboleahai kwa kutumia taka.
Shabaha ya Mwangi anasema ilipania kuangazia kiwango cha juu cha asidi kwenye udongo, kuongeza kiwango cha mazao na pia kuhakikisha yamezalishwa kwa njia salama.
Elimu yake ikiwa na msingi wa Sayansi ya Mazingira na Kilimo Endelevu, bila kusahau uzoefu wake, anatambua kuwa wakulima wengi hasa wa mashamba madogo (small scale farmers) wametekwa katika mbinu duni za kilimo zinazowalazimisha kutegemea pembejeo zenye kemikali kwa matarajio ya mazao mengi.
“Nilikuwa nafunza wakulima jinsi ya kutengeneza mbolea ya mboji (compost manure), kuhifadhi afya ya udongo, kutumia matandazo (mulching) na kuhifadhi maji. Udongo wetu umeharibika pakubwa,” Mwangi ambaye ana Shahada ya Sayansi ya Mazingira na ile ya Uzamili katika Kilimo Endelevu anasema.

Organic Fields Ltd ilianza rasmi uzalishaji wa mboleahai 2018, ikilenga kukabiliana na changamoto ya kudhoofika kwa kiwango cha udongo nchini na pia kusaidia kuzalisha mazao salama.
Mwanzoni, Mwangi anadokeza kwamba alikuwa akikusanya kati ya kilo 200 hadi 400 za taka za chakula kila siku kutoka masoko ya mitaa na kuzigeuza kuwa mboleahai.
Kwa sasa, kampuni hiyo huzalisha hadi tani 20 za mbolea kila siku. Mbali na taka za chakula, pia hukusanya taka za mimea na mazao shambani, na pia samadi ya mifugo.
“Tunakusanya taka kutoka masoko ya Kaunti ya Kiambu na Nairobi,” anadokeza.
Kando na kiwanda cha Ruiru, eneo la Tatu City ana kituo cha ukusanyaji taka, na kingine Mwea kinachotumika kutengeneza biochar, malighafi muhimu kwenye mbolea anayounda.
Biochar inasifika kwa kuboresha afya ya udongo, kuhifadhi maji na virutubisho.
“Mbolea yetu hutengenezwa kwa mfumo wa kisasa wa kuingiza vijidudu maalum, kuondoa harufu, na kutibu kwa muda kabla ya kusafishwa na kupakiwa,” anaeleza Juliet Njeru, Mkurugenzi wa Oparesheni na mwanzilishi mwenza wa kampuni hiyo.

Organic Fields Ltd inashirikiana na taasisi kama Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo na Teknolojia (JKUAT), Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), Egerton, pamoja na KALRO, KEBS, Cropnuts na Kilimohai Organic – ilyothibitisha bidhaa zao kuuzwa Afrika Mashariki baada ya kuafiki viwango vya kimataifa vya ISO.
Kampuni hiyo inatumia mashine zilizotengenezwa hapa nchini, zikiwemo mashine ya kusaga na kusafisha mbolea.
Uzalishaji wa mbolea huchukua kati ya miezi miwili hadi mitatu.
Chini ya chapa ya Hygrow, mfuko wa kilo 10 huuza Sh700, kilo 25 Sh1,500, na kilo 50 Sh2,500.

Mwangi anapongeza serikali kwa kuzindua Mkakati kuendeleza Kilimohai (Agroecology) wa 2024-2033, akisema utasaidia kujumuisha matumizi ya mbolea kama anayounda kwenye sekta ya kilimo ili kulinda mazingira.
Mkakati huo, aidha, unalenga kuboresha afya ya udongo, kuongeza uzalishaji na kuendeleza mfumo wa kilimo endelevu na wenye usawa.
Mwangi anakadiria kuwa biashara yake imebuni zaidi ya nafasi 300 za ajira kwa njia ya moja kwa moja, na isiyo ya moja kwa moja.
Licha ya mafanikio, analalamikia changamoto kama vile leseni nyingi zinazohitajika na ukosefu wa mikopo kutoka taasisi za kifedha.
