Anavyojipa mapato kupitia mafuta ya macadamia
JANGA la Covid-19, mwaka 2020, lilipokuwa linatesa taifa na ulimwengu, Petronillah Mugeni alipata wazo la kibiashara ambalo limebadilisha maisha yake.
Akiwa mzaliwa wa Meru – mojawapo ya kaunti Kenya zinazozalisha macadamia, anasema alitamani sana kusaidia kushusha gharama ya mafuta ya kupikia.
Nchini, viwanda vya mafuta huagiza kutoka nje asilimia 95 ya malighafi – mbegu, hii ikiashiria kuwa ni asilimia 5 pekee inayotoka ndani kwa ndani, Petronillah akiapa kujitolea kusaidia kuziba gapu hiyo kubwa.
“Virusi vya corona vikienea, niliamua kujitosa kwenye uuzaji wa mafuta ya macadamia,” anasema.
Wakati huo, alikuwa ameajiriwa na hatua hiyo anasema ilikuwa faafu mno kumpa pato la ziada.

Kibindoni, kijana huyu anafichua alikuwa amejiwekea kiasi fulani cha pesa kama akiba.
Pamoja na akiba hiyo kaka yangu alinimpa mkopo, nikapata mtaji jumla wa Sh50,000 kujitosa kwenye biashara ya mafuta ya macadamia, anadokeza.
Jukumu lake hasa kwenye mtandao huo ni kupakia mafuta. Alianza biashara hiyo katika Kaunti ya Embu ambako yeye ni mwenyeji na mkazi.
Utangulizi, hata hivyo, Petronillah anakiri haukuwa mteremko. “Nilianza kwa kuchuuza kwenye maduka na hata maofisi. Baadhi ya wanunuzi walitilia shaka bidhaa zangu,” anakumbuka.
Miaka mitano baadaye, mjasiriamali huyu anajivunia kuandikisha maendeleo.
Kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali, alidokeza kuwa kuanzia kuchuuza lita 2 za mafuta ya macadamia kwa siku, sasa anauza lita 50 kwa wiki.

Petronillah Mugeni, ambaye pia huuza asali, wakati wa Maonyesho ya MSMEs ya Afrika Mashariki (EAC) 2025 Uhuru Gardens, Nairobi, Novemba 14. Picha|Sammy Waweru
Isitoshe, amejumuisha asali. “Asali, kwa juma ninauza zaidi ya lita 100,” akasema, akifichua kuwa alilazimika kuacha kazi kuzamia kikamilifu biashara ya mafuta.
Mwanadada huyu amemudu duka la kusambaza bidhaa zake lililoko Embu, ambalo pia lina ofisi.
“Hununua mafuta kutoka kwa wanaokama na kurina, kisha ninapakia na kuweka lebo,” anaelezea mwasisi huyo wa Pure PetroOrganic Packers Ltd.
Lita moja ya mafuta anauza Sh700, sawa na asali, akifichua kuwa kando na Embu, pia amefanikiwa kupata jukwaa la soko kaunti jirani ya Meru, Kirinyaga, na pia Nakuru, Nairobi, Mombasa, Nakuru, na Uasin Gishu.
Hali kadhalika, ameanza kupata oda nje ya mipaka ya Kenya. “Wapo wateja kutoka Qatar, Dubai na hata Afrika Kusini, na kwa mwezi ninakadiria kuuza lita 30 za mafuta ya macadamia,” anadokeza.

Kuanzia mhudumu – yeye mwenyewe, sasa abuni nafasi za ajira kwa wafanyakazi saba wanaojumuisha; wanabodaboda na wapakiaji.
Aidha, Petronillah alikuwa miongoni mwa waliohudhuria makala ya 25 ya Maonyesho ya Kibiashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC MSMEs Trade Fair 2025, yaliyofanyika Uhuru Gardens, Nairobi.
Huku shabaha yake ikiwa kupenyeza mizizi kila kona ya taifa, anaamini kuwa ataweza kupeperusha bidhaa zake kwa mataifa makubwa ulimwenguni kama vile Amerika, nchi za Bara Uropa, Australia, kati ya mengine.
Biashara yake, hata hivyo, anasema haikosi changamoto haswa kutokana na wahuni wanaofeki nembo yake.
Hali kadhalika, mfanyabiashara huyu mchanga analalamikia gharama ya juu ya vifaa vya kupakia na ushuru unaotozwa wanaochakata bidhaa za kula.
