• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 6:50 AM
Anavyojituma kuangazia kero ya mimba za mapema kwa matineja

Anavyojituma kuangazia kero ya mimba za mapema kwa matineja

NA PETER CHANGTOEK

BAADA ya kufutwa kazi jijini Nairobi, Nancy Bulinda alirudi nyumbani – Kaunti ya Vihiga, ambapo aligundua changamoto nyingi ambazo vijana wengi walikuwa wakipitia, na akaasisi mradi uliolenga kuziangazia.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na mimba za mapema, ambapo wasichana walikuwa wakipachikwa wakiwa wadogo, utumiaji wa mihadarati na ukosefu wa ajira.

“Vijana niliozungumza nao hawakuwa na wasaidizi na washauri wa kuwaelekeza. Kwa kuwa nilikuwa na shauku kwa huduma kwa jamii na ruwaza ya kubadilisha maisha, niliamua kutengeneza afisi kijijini, katika Kaunti-ndogo ya Hamisi,” asimulia.

Bulinda, mwenye umri wa miaka 40, ni mwasisi wa wakfu unaojulikana kama Mentor Dada Foundation.

Alikuwa amesajili shirika hilo kama la kijamii (CBO) 2016, na lilikuwa na afisi jijini Nairobi, kabla kulihamishia.

“Mimi ni mke na mama, na nina Digrii ya Usimamizi wa Biashara na Diploma ya Juu katika Masuala ya Usimamizi wa Mifumo ya Mawasiliano, na cheti cha Saikolojia,” afichua.

Bulinda anadokeza kuwa, alipoanzisha wakfu huo, alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya Sameer Africa Limited.

Mentor Dada Foundation hushughulikia masuala mengi yanayohusu vijana Vihiga, na kwa sasa, hushughulikia ajenda ya serikali ya kubuni nafasi za ajira kwa vijana.

“Katika kituo chetu, huchukua vijana wanaojihusisha na shughuli zinazoambatana na ujuzi wao wapate riziki. Kwa mfano, kwa sasa, tuna vijana wanaofanya shughuli ya kupika na kuchuuza vitafunio na vyakula katika kituo chetu, na kuuza katika afisi zetu na katika jamii, na hivyo kujiajiri,” asema Bulinda.

“Tungependa serikali ya Kaunti ya Vihiga ishirikiane nasi au wafadhili wengine, ili kuweka vifaa katika kituo chetu, ili kukiwezesha kuhudumia vijana wengi, kama vile wanaoshughulika na utengenezaji wa fasheni, ili watengeneze sare za kuuza, na wale wanaofanya useremala watengeneze fanicha za kuuza,” asema.

Anaongeza kuwa, wameweza kutembelea shule zaidi ya 20, wakitoa ushauri na mwelekeo kuhusu ajira.

Aidha, wamezuru vyuo vya anuwai zaidi ya vitano, vikiwemo Kaimosi na Gimomoi.

“Kupitia kwa uhamasishaji katika shule, tumeweza kupunguza kuongezeka kwa mimba kwa wasichana na matumizi ya mihadarati miongoni mwa vijana,” adokeza Bulinda.

Anaongeza kuwa, shirika lake huziba pengo baina ya wazazi na wanao; kwa kuzungumzia masuala ambayo wazazi wanaogopa kuyazungumzia na wanao.

Hata hivyo, anasema kuwa, changamoto iliyopo ni kukosa usaidizi kutoka kwa wazazi, hususan kwa suala la kuongezeka kwa mimba miongoni mwa wasichana wadogo.

“Jamii bado haijakumbatia umuhimu wa elimu na hivyo, vijana huoa au kuolewa wakiwa na umri mdogo, miaka 16, na tunapoongea na wazazi hao, wao huonekana wakiwa sawa na suala hilo. Ikiwa vijana watashauriwa kuacha kujamiiana bila kinga, basi tatizo hilo linaweza kukabiliwa,” asema.

Bulinda anasema kuwa, mipango yao ya miaka mitano ijayo ni kufanya kituo hicho kuwa na uwezo kutoa ajira kwa vijana, ambao wanafuzu kutoka vyuo vya kiufundi vya serikali.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya wamkumbuka ‘Mr Ibu’ kwa ucheshi wake

Ujangili: Wahubiri walilia Ruto

T L