Apu zasaidia masonko kuagiza ‘chapo madondo’ kwa ‘vibandaski’
NA LABAAN SHABAAN
WAKENYA wengi wenye kipato cha chini na cha wastani hupendelea kula katika hoteli za kitaa almaarufu ‘vibandaski’.
Hii ni kwa sababu vyakula huwa vya bei nafuu katika hoteli za aina hiyo.
Kadri ukuaji wa kiteknolojia unavyozidi kushuhudiwa, ndivyo wamiliki wa hoteli wanavyokuwa wabunifu ili kuteka wateja walio mbali na upeo wa macho yao.
Bi Leah Kimani ambaye anamiliki hoteli ya kiwango cha aina hiyo kwa jina Damaka Dishez iliyoko Kihunguro, eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, anasema akianza, alilenga kuuzia wapitanjia chakula. Vile vile alilenga wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyo mkabala na barabara kuu ya Thika Superhighway.
Lakini sasa amesema mambo yamebadilika kwani anahudumia wateja wengi tangu aanze kuuza vyakula kupitia mitandao ya kijamii.
Bi Kimani anaambia Taifa Leo kwamba mbali na kuuza chakula kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii, pia amesajili biashara yake katika apu ya glovo ambapo ameweka menu au ankara ya vyakula vya kuanzia Sh200.
Anasema wateja wake wameongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 tangu akumbatia matumizi ya teknolojia.
Anafichua kwamba wateja wenye hela zao, mabwanyenye ambao zamani waliogopa kuingia kwa kibanda chake kuagiza chakula, wanafanya hivyo kupitia hayo majukwaa ya mitandao ya kijamii na apu.
“Wateja wanaoagiza vyakula mitandaoni ni wenye hadhi ambao nisingewapata sababu waliona aibu kuja katika kibanda changu kununua na kula chakula wakiwa wameketi,” akaeleza Bi Kimani.
Anasema wengi hupendelea kuagiza chapati na maharagwe, ama kwa lugha ya mtaani ‘chapo madondo’.
“Wengi wao hufanya kazi katika ofisi zilizoko mjini Ruiru na viunga vyake na wakienda katika hoteli za hadhi ya juu, vyakula vitawagharimu hela zaidi kwa sababu ya usafiri na bei,” akaongeza.
Naye Bi Lenson Munene ambaye pia amekumbatia teknolojia, anasema huchangamkia mitandao kuuza vyakula vyake kutoka hoteli yake iliyoko katika wadi ya Kahawa West eneobunge la Roysambu, Kaunti ya Nairobi.
“Hata nimetoa bonasi ya asilimia 10 kwa wateja wanaoagiza vyakula kutumia mitandao ya kijamii na apu za kidijitali,” Bi Munene ambaye anamiliki Lakers Dishes, akaambia Taifa Leo.
“Tunahakikishia wateja wetu vyakula vilivyopikwa vizuri ili waendelee kuagiza kupitia majukwaa hayo,” akaongeza.
Sawa na Bi Kimani na Bi Munene, Bi Rhoda Nyakio ambaye ni mmiliki wa hoteli ya Testimony eneo la Ruiru, hukumbatia mitandao kuvumisha biashara yake.
“Wengi wa wateja wetu ni wanafunzi wa vyuo vikuu lakini pia tunawahudumia wanaofanya kazi za ofisini wanapoagiza vyakula vyetu,” Rhoda asema.
“Kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa dijitali ndiyo njia ya uhakika ya kuwa na wateja wakati wote,” akaongeza akisema bei ya vyakula hupanda kidogo kulipia huduma za apu na nauli na malipo kwa wasambazaji wa vyakula ambao mara nyingi hutumia pikipiki.
Matumizi ya apu dijitali na mitandao ya kijamii yamekuwa maarufu sana kwa wafanyabiashara wanaotaka kuendelea kukua na kunawiri.