Makala

Arati na Osoro watumiwa kamishna mpya kupambana na vurugu zao

January 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

KAUNTI za Kisii na Murang’a ambazo katika siku za hivi majuzi zimekumbwa na misukosuko ya kisiasa zimefanyiwa marekebisho ya kiutawala na Waziri wa Usalama wa Ndani Bw Kithure Kindiki.

Kaunti ya Kisii imekuwa ngome ya vurugu kati ya wafuasi wa Gavana Simba Arati na kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa, Bw Silvanus Osoro ambao hukabiliana hata kwa risasi mikutanoni na kuwaacha baadhi yao wakiwa na majeraha ya risasi mwilini.

Murang’a nayo imekuwa  ngome ya ukaidi dhidi ya Naibu wa Rais Bw Rigathi Gachagua ambapo wafuasi wa mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro wakiongozwa na Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu wamezindua masharti kwa rais William Ruto amfute kazi naibu huyo wake 2027 na kisha azimwe kurithi mikoba ya Ikulu 2032.

Sasa, katika hali ambayo inaonekana kama ya kujaribu kuleta usimamizi mpya wa mikakati ya kiserikali, ikizingatiwa kwamba utawala wa kimaeneo ndio macho ya serikali mashinani, makamishna katika kaunti hizo wamehamishwa.

Katika Kaunti ya Kisii, Bw Tom Anjere alihamishwa hadi makao makuu Jijini Nairobi huku naye aliyekuwa Kamishna wa Murang’a Bw Patrick Mukuria akitumwa kupambana na fujo za Arati na Osoro.

Murang’a sasa kutakuwa na kamishna mpya ambaye ni Joshua Nkanatha kabla yake akiwa Kamishna wa Kaunti ya Kiambu.

Katika mabadiliko hayo, Bw Abdirisak Jaldesa ametumwa Nyandarua kutoka Kaunti ya Mombasa.

Mombasa sasa imo mikononi mwa kamishna Mohamed Nur, aliyekuwa akihudumu Kaunti ya Tana River.

Bw Erastus Mbui ametumwa kuwajibikia Kaunti ya Laikipia kutoka ile ya Kitui na ambapo sasa Kitui kutashughulikiwa na Bw Kipchumba Rutto ambaye awali alikuwa kamishna Busia.

Bw Henry Wafula kwa sasa ndiye Kamishna wa Kaunti ya Makueni kutoka yake ya awali ya Samburu na ambapo Bw Onesmus Kyatha kutoka Kaunti ya Nyamira ataingia afisini Kaunti ya Samburu.

Bw Hiram Kahiro amerushwa kutoka makao makuu hadi kuwa kamishna wa Kaunti ya Kwale naye Apollo Okello akitolewa Wesk Pokot hadi kuwa msaidizi wa kamishna mshirikishi (RC) wa eneo la Rift Valley.

Bi Susan Waweru ametolewa Nairobi na kutumwa katika Kaunti ya Siaya, naye Jacob Ouma akitumwa Meru kutoka Kaunti ya Turkana.

Kwa sasa, Bw Ouma atakuwa na jukumu la kufuatilia siasa hasi za Kaunti ya Meru ambapo wafuasi wa Gavana Kawira Mwangaza hulumbana kwa kila aina ya hila na njama.

Kaunti ya Turkana kumetumwa Bw Julius Kavita kama kamishna mpya huku aliyekuwa Kamishna wa Nyandarua Bw Mohammed Barre na ambaye amefikisha miaka ya kustaafu akiteuliwa kuwa katibu wa masuala ya amani.

Uteuzi huo wa Bw Barre umezua maswali ya busara ya serikali kunyima waliohitimu kazi na kuipa aliyehudumu hadi kufikisha miaka ya kwenda nyumbani.

[email protected]