• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
ARI YA UFANISI: Anaelimisha wengi kukuza mipapai ya kimo kifupi inayozaa matunda tele

ARI YA UFANISI: Anaelimisha wengi kukuza mipapai ya kimo kifupi inayozaa matunda tele

Na PETER CHANGTOEK

ALEXANDER Kituku alisomea Shahada ya Sayansi ya Biokemia (Biochemistry) katika Chuo Kikuu cha Egerton kabla ya kufuzu na kuhitimu mnamo 2014.

Baada ya kuhitimu, alifunza katika shule moja ya upili iliyoko katika kaunti ya Kirinyaga, na pia kufanya kazi katika kampuni ya EPZ, eneo la Athi River.

Hata hivyo, anasema kuwa alikuwa na ari ya kujihusisha na masuala ya kilimo kwa sababu moyo wake ulikuwa ukipenda mambo ya zaraa.

“Moyo wangu ulikuwa katika mambo ya kilimo. Nilianza kulima kama njia ya ziada ya kujipatia fedha wakati nilipokuwa nikifunza, na mwaka huu nikajitosa katika kilimo-biashara,’’ anasema mkulima huyo mwenye umri wa miaka 29.

Mkulima huyu hukuza na kuuza na miche ya mahuluti (hybrid) ya mipapai na aina fulani ya michungwa, katika eneo la Cabanas, Nairobi, na katika eneo la Athi River.

Yeye hukitumia kipande cha ardhi chenye ukubwa wa mita mia moja mraba; yaani mita 20 kwa urefu kwa mita 5 kwa upana, ambapo amekijengea kivungulio.

“Nyanya na babu yangu walikuwa wakulima. Sisemi kuwa walinifunza kuhusu kilimo, lakini walizidisha ari yangu ya kujihusisha na kilimo,’’ anaeleza mkulima huyo.

Kituku anafichua kwamba alijitosa katika shughuli ya kuikuza miche ya mipapai mnamo 2015, akiutumia mtaji anaoutaja kuwa mdogo.

Alianza kwa kununua mbegu za mipapai kutoka kwa duka moja la kuuza pembejeo za kilimo. “Maduka ya kuuza bidhaa za kilimo yana aina tofauti za mbegu, na mtu anaweza kuzinunua chache na aongezee baadaye,’’ anadokeza.

Ingawaje yeye alianza kwa kuikuza miche ya mipapai pekee, kwa wakati huu, anaikuza pamoja na miche ya mimea mingineyo, mathalani michenza mahuluti.

Kwa mujibu wa mkulima huyo ni kwamba, kiasi cha matunda yanayochumwa kwa mipapai hutegemea aina ya mimea hiyo.

Anasema kuna aina iliyoboreshwa ijulikanayo kwa jina Solo Sunrise, ambayo huzaa matunda ambayo saizi yake ni ndogo, na tunda moja huwa na uzani wa gramu 300 na mkulima anaweza kuyachuma matunda 200 tu kutoka kwa mmea huo mmoja, kwa mwaka mmoja.

Lakini anaeleza kuwa kuna aina nyingine ya mipapai kama vile Dwarf Calina papaya, ambayo matunda yake huwa na uzito wa zaidi ya kilo moja, na mtu anaweza kuyachuma matunda 150 kutoka kwa mmea mmoja, kwa mwaka mmoja.

Anafichua kuwa Dwarf Calina papaya huanza kuwa na maua baada ya muda wa miezi miwili baada ya kuatikwa au kupandikizwa, na matunda huwa tayari kuchumwa baada ya miezi sita baada ya kuatikwa. Kwa jumla, aina hiyo huchukua muda wa miezi minane kuanzia wakati mbegu zinapopandwa.

Kufaulisha kilimo cha matunda hayo, yeye hutumia mbolea asilia kuikuza miche yake ambayo anakiri imeboresha juhudi zake.

Wateja wake wengi wa miche hujitokeza msimu wa mvua unapoanza kwa kuwa wanataka angalau waweze kupanda mvua ikiendelea kunyesha.

“Mauzo hutegemea misimu. Watu wengi huipanda miche ya matunda mwanzoni mwa misimu wa mvua- Oktoba na Aprili. Kwa wakati huo, ninaweza kuiuza miche 5,000 kwa msimu mmoja. Kuna wakulima wengine ambao hutumia unyunyiziaji maji kuikuza mimea, na hivyo huweza kuipanda kwa wakati wowote,’’ anasema, akiongeza kuwa yeye huuza hadi miche 500 kwa mwezi hasa kwa wale wanaotegemea kilimo cha unyunyizaji maji. Anaeleza kuwa huwa anaiuza miche hiyo kwa Sh100 kila mmoja.

“Mimi huuza kote nchini, na hutumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kuvumisha biashara yangu. Huko mitandaoni natambulika kama “Alex Kituku wa Papaya” ama “Papaya Empire”, ambapo amejikita sana na ukuzaji wa mipapai aina ya ‘Calina (IPB9) papaya na iliyoboreshwa ‘Solo sunrise’.

Ili kuikinga mimea yake dhidi ya uharibifu kutoka kwa wadudu na magonjwa, Kituku anasema huhakikisha kuwa usafi unadumishwa kwenye kitalu, na pia huhakikisha kuwa inapata virutubisho vinavyofaa.

Changamoto

Ukosefu wa maji safi ya kuikuza miche ni mojawapo ya changamoto ambazo hupitia katika shughuli hiyo. Aidha, kutoota kwa mbegu zote za mimea pia ni tatizo.

Mbali na miche ya mipapai, mkulima huyo pia huiuza miche ya michenza kwa Sh250 kila mmoja na anasisitiza kuwa biashara hiyo ni ya kuvutia.

Anawashauri watu, hususan vijana kujitosa katika shughuli za kilimo kwa kuwa kina manufaa.

“Anza kwa mmea unaopenda. Mimi hupenda kuhusishwa na mipapai, hiyo ni nembo yangu,’’ asema, akiongeza kuwa si lazima mja awe na shamba, bali anaweza kulikodi.

Kituku anasema kuwa ana hamu ya kuwaona watu walioko katika maeneo yanayokumbwa na ukame wakiikuza mipapai.

“Ninanuia kuwafunza vijana wenzangu kutengeneza vitalu vyao karibu na wakulima,’’ asema Kituku, akiongeza kuwa hilo litawapa vijana ajira na kuangamiza ukosefu wa usalama na umaskini.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge apendekeza naibu gavana awe na mamlaka zaidi

SHANGAZI AKUJIBU: Nimependa mwenye umri sawa na mama...

adminleo