• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Asimulia jinsi alivyozindua mochari za Montezuma Monalisa

Asimulia jinsi alivyozindua mochari za Montezuma Monalisa

Na MWANGI MUIRURI

BW Benjamin Kibiku akiwa na mtaji wa Sh150,000 mwaka wa 1988 alinunua gari aina ya pickup kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu.

Kwa kuwa mashirika ya kifedha yalikuwa yakimhepa wakati alifichua kwamba alikuwa akihitaji mkopo ili anunue gari la kubeba maiti katika wazo lake la kibiashara la kuwekeza katika chumba cha kuhifadhi maiti, aliamua kubadilisha mbinu.

“Safari hii, niliwaendea wakopeshaji nikawaambia nilikuwa nikihitaji gari hilo kwa shughuli za kilimo,” asema Bw Kibiku.

Hofu ya wakopeshaji ilikuwa kwamba ikiwa angelemewa kulilipia gari la kubeba maiti, litwaliwe na liwekwe katika mnada, pengine hakuna wengi ambao wangejitokeza kutaka kulinunua na mkopo uishie kuorodheshwa kama mkopo hatari.

Bw Benjamin Kibiku. Picha/ Mwangi Muiruri

Aidha, akiwa katika taaluma ya uhasibu katika sekta ya bima nchini, na ambapo awali alikuwa akifanya kazi katika sekta ya kawi, kupata barua ya usajili ili azindue chumba chake cha kwanza cha kuhifadhia maiti bado ilikuwa ni changamoto.

Baadaye alifanikiwa kuzindua biashara hiyo yake mwaka huo wa 1988 na ndiyo kwa sasa inajulikana kama Montezuma Monalisa.

Anasema kuwa alitatizika sana kusaka jina mwafaka la hifadhi zake za maiti kwa kuwa alipendelea majina kama New World Funeral Services na Heavenly Kingdom.

Anasema alikumbuka kwamba akiwa katika shule ya upili hiyo miaka ya 1970, aliwahi kuwajibikia mchezo wa kuigiza ufahamikao kama Montezuma’s Daughter akifahamika kama Monalisa. Ndipo jina likaingia ghafla, na nikapata nembo ya biashara yangu,” asema.

Anasema kuwa shida nyingine alikumbana nayo ni ya kusaka wateja na alipofungua afisi yake ya kwanza katika eneo la Burma jijini Nairobi karibu na mtaa wa Shauri Moyo, wengi walikuwa wakimkemea kwa dhati kwa kuegesha gari la kubeba maiti katika mtaa wao.

“Nilikuwa na mfanyakazi mmoja katika afisi hiyo yangu akiwa ni mwanamke na ambaye alikuwa wa kupokea wateja na ambao hata hawakuwa wakijitokeza.

Nilianza kupekua matangazo ya vifo katika magazeti na nikaanza kujitokeza katika kamati za mazishi na kusaka biashara za kuafirisha maiti hadi katika maeneo ya mazishi…” asema.

Anasema kuwa hata huduma za madereva zilikuwa shida kupata kwa kuwa wengi walikuwa wakijitokeza lakini mwili ukishapakiwa ndani ya gari hilo, wakawa wanahepa kwa kuogopa kuendesha gari lililopakiwa maiti.

‘Ilikuwa inanibidi niwe katika visa vingi nijiendeshee gari hilo ikimaanisha nihepe kazi. Lakini haba nah aba ikajaza kibaba. Bidii na uadilifu zikanifaa na nikawa nimejulikana katika safu hii ya heshima za mwisho,” asema.

Anasema kuwa hakuwa amesahau jinsi alipoteza rafiki wake wa karibu katika jaribio la mapinduzi ya kiserikali nchini Kenya mwaka wa 1982 na jinsi alihangaika kupata huduma bora za uhifadhi wa mwili na pia uchukuzi wa hadi eneo la mazishi.

Ajishindia imani ya wengi

Alibadilisha eneo la biashara yake hadi mtaa wa Mbagathi ambapo alijenga hifadhi yake ya maiti na hadi sasa, anaripoti tu kupanuka kwa biashara yake kwa viwango vikuu na ambapo anasema amejishindia imani ya wengi.

“Kitu cha kwanza ni usafi ndani ya hifadhi hizi za Monalisa. Huduma bora iliyo na uadilifu ukijua kuwa unahudumia watu ambao wanasononeka kwa kupoteza wapendwa wao. Gharama pia iwe ni ya kujali masilahi ya wote,” asema.

Anateta kuwa hospitali hapa nchini ziko katika harakati za kuzindua hifadhi za maiti.

“Hospitali ni za kutibu wagonjwa au ni za kufanya biashara ya kuhifadhi maiti? Ni bora wasimamizi wa hospitali hizi waongeze juhudi za kutibu au wawekeze rasilimali katika uhifadhi wa maiti? Mimi ningepigia kura wapanue huduma za kimatibabu na waachie wengine nje ya uuguzi suala la kuhifadhi maiti,” asema.

Anasema kuwa anaunga mkono maamuzi ya kuchoma maiti badala ya kuizika.

“Ni maamuzi ya kupunguza gharama za mazishi. Tutahifadhi mazingira kwa kuwa hatutahitaji kukata miti ili tujenge majeneza. Na hakutakuwa na mizozo ya kifamilia kuhusu mahala pa kuzika mwili,” asema.

Anasema kuwa anatarajia kuwekeza katika kila Kaunti hapa nchini na ambapo ametua katika Kaunti ya Murang’a ambapo katika kando mwa barabara ya Thika Superhighway karibu na Mji wa Kabati, amejenga tawi la biashara hii yake.

Anasema kuwa biashara hii yake ni sawa na duka moja la heshima za mwisho ambapo “utajinunulia jeneza, maua, ujipe huduma za usafirishaji maiti kando na kuhifadhiwa mwili.”

  • Tags

You can share this post!

She-Flames ya Malawi yawasili kumenyana na Harambee...

‘Jinamizi la ajali nchini linahitaji kutathminiwa kwa...

adminleo