• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Askari jela aliyemwaga unga akitibiwa aomba arudishwe kazini

Askari jela aliyemwaga unga akitibiwa aomba arudishwe kazini

NA GEORGE ODIWUOR

WAZAZI na nduguze Joseph Ochoro walikuwa na furaha sana waliposikia angejiunga na Idara ya Magereza.

Ulikuwa mwaka wa 2019 wakati alishiriki zoezi la usajili wa makurutu mjini Homa Bay na akafuzu.

Alipokea mafunzo Ruiru, Kaunti ya Kiambu na akafaulu kuwa askari jela katika gereza la Nyahururu kuanzia mwaka 2020.

Taifa Leo ilipomtembelea nyumbani Imbo, Kayanda Mashariki, alifichua kwamba kazi yake ilikuwa kuhakikisha wafungwa wanafuata sheria za jela.

Alipopata kazi yake hiyo, mama yake, Bi Janet Achieng, alifurahi kuwa mtoto wake angebadilisha maisha yake.

Ni mkulima mdogo ambaye aling’ang’ana sana kulea watoto wake.

“Tulikuwa na matumaini makubwa sana naye na niliweka matumaini yangu yote kwake,” Bi Achieng akasimulia jinsi alivyomtegemea mwana wake.

Lakini matumaini hayo yaliyeyuka ghafla kwa sababu miaka miwili baadaye, Bw Ochoro alifutwa kazi.

Hii ni baada ya kutoripoti kazini kwa miezi miwili na jaribio la kuomba kurejeshwa likagonga mwamba.

“Sikupewa barua ya kuachishwa kazi. Nilifutwa kazi kwa mdomo,” anadai Bw Ochoro.

Bw Ochoro anakumbuka alipoomba likizo ya wiki mbili akiwa kazini.

“Mama yangu alikuwa mgonjwa na nililazimika kuenda kumwona nyumbani baada ya kuomba likizo,” anasema.

Akiwa safarini kuenda nyumbani Homa Bay, Bw Ochoro anasema alizirai mjini Kisii na ikabidi akimbizwe hospitalini.

“Nilimwambia bosi wangu kilichojiri wakati huo nikiwa hospitalini. Aliahidi kunisaidia hadi nirudi kazini lakini hilo halikutimia,” Bw Ochoro akasema.

Anaeleza kuwa afisa msimamizi wa maslahi ya wafungwa katika gereza la Kisii ndiye alistahili kutuma taarifa kwa jela ya Nyahururu kuthibitisha madai hayo.

“Nilipewa Sh100 na ahadi kuwa taarifa ingetumwa. Nilikuwa ninaamini ningerudi kazini baada ya kupata afueni,” anasema.

Baada ya kuondoka hospitalini, Bw Ochoro alienda nyumbani ambapo anaeleza kuwa hali yake ilidorora na akalazwa tena katika hospitali nyingine.

“Niliambiwa nisiwe na hofu kwa sababu walikuwa wamepiga picha zangu nikiwa kwa kitanda cha wagonjwa pale hospitalini,” anaeleza askari jela huyo wa zamani.

“Nililazwa mwezi mmoja hospitalini na nikaenda nyumbani kwa mwezi mmoja zaidi,” akaongeza.

Lakini aliporudi kazini Nyahururu, alishangaa kupokea onyo kuwa hakustahili kuwepo pale kazini tena.

“Niliomba nipewe barua ya kuachishwa kazi lakini niliambiwa faili yangu ilipelekwa katika makao makuu jijini. Nilijaribu kufuata hadi huko lakini sikufaulu,” Bw Ochoro anaeleza.

Afisa aliyemtembelea hospitalini alikiri kuwa alisahau kutuma ujumbe kuhusu hali yake hadi Nyahururu.

Bw Joseph Ochoro akionyesha cheti cha Huduma kwa Idara ya Magereza. PICHA | GEORGE ODIWOUR

Sasa ni miaka miwili tangu kitumbua kiingie mchanga ambapo amekuwa akisubiri apigiwe simu arejee kazini.

Maisha yake kijijini yamekuwa magumu na ameamua kufanya kazi za vibarua, zikiwemo zile za kujenga nyumba.

“Mke wangu aliniacha kwa sababu ya changamoto za kifedha nyumbani. Ninaendelea kumtunza mama yangu mgonjwa lakini nimeshindwa kupata pesa za kutosha kugharimia matibabu,” anaeleza.

Anatoa wito kwa viongozi wa ngazi za juu katika idara ya magereza kusikia kilio chake.

“Nina stakabadhi za hospitalini kuonyesha nilikuwa mgonjwa. Ninavyoelewa ni kwamba mambo yaliniendea segemnege pale afisa wa Kisii alikosa kutuma taarifa Nyahururu,” Bw Ochoro anamalizia.

  • Tags

You can share this post!

MC: Mfahamu chifu ‘simpo’ anayezipa sherehe ‘tempo’...

KVDA yawaondolea hofu wakazi ikisema ni vigumu bwawa la...

T L