Makala

Askofu adai ametabiri 2024 mafisadi watarushwa jela kula maharagwe

January 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

ASKOFU Harrison Ng’ang’a wa kanisa la Christian Foundation Fellowship (CFF) ametabiri kwamba mwaka wa 2024 wezi wengi wa pesa za umma watakiona cha mtema kuni.

Pasta Harrison anasema hatua hiyo inatokana na maombi ya Wakenya mafisadi wakabiliwe, na kwamba Mungu ameyaskia.

Kulingana na Mtumishi huyo wa Mungu, jambo hilo litaweka Kenya kwenye ramani ya ulimwengu.

“Bwana amesikia maombi ya wale ambao wamekuwa wakiombea nchi hii dhidi ya mafisadi na kwa hivyo taifa la Kenya limeangaliwa na jicho la kibali na Mungu akiwa mbinguni na watakamatwa huku tukipata kukubalika na dunia,” akasema.

Aliongeza kwamba “taifa la Kenya litapakwa mafuta na kukubalika huku dunia nzima ikianza kutufuata ihusishwe nasi, watalii wakifurika nchini”.

Lakini walio bado kujitakasa, wanahimizwa watekeleze hilo kwa dharura.

“Watu wa Mungu mjitakase sasa kwa kuwa Muumba amesema amekuwa katika vita na Wakenya kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita lakini kwa watakaojitakasa 2024 mapigo hayo yataisha,” akasema.

Askofu huyo anaongeza kwamba mwaka wa 2024 kutakuwa na wimbi mpya kabisa la kisiasa “ambapo serikali iliyo mamlakani ya Rais William Ruto itafanikiwa kustawisha taifa hili kupitia hata kuvutia wawekezaji wengi kutoka mataifa mengine”.

Alioongeza kwamba Mungu atakuwa na Wakenya wanaomwamini na atawapanulia baraka na kuwalegezea mizigo ya mahangaiko.

“Mungu amenifunulia kwamba atawaunga mkono kikamilifu wamwaminio na ni watakatifu,” akasema.

Aliongeza kwamba dunia itatikisika na itatetemeshwa zaidi 2024 lakini watu wa Mungu watakingwa na mkono ulio na nguvu wa uwezo wote wa Bwana.

Alisema kwamba kwa sasa kuna vita kubwa inayoendelea kati ya Mungu na wachungaji feki na kwamba 2024 ndio malumbano hayo yataingia awamu muhimu na ya kina, akidokeza “manabii, wachungaji na mitume wa uongo mtakipata huu mwaka, Mungu asema”.

Askofu huyo alisema kwamba maombi na imani zitatuzwa, lakini mchezo kanisani utahukumiwa kwa uhasi mkuu.
Alizidi kunabii kwamba watu wakome kupigana vita makanisani ili wainuliwe “kwa kuwa wengi mumekuwa mkiniomba kanisani huku nikikataa kuwajibu kwa sababu ya kujawa na vita miongoni mwenu”.

Alisema Mungu amejieleza waziwazi kwake kwamba “mkimaliza vita katika nyoyo zenu atawainua…Lakini cha maana ni lazima muwe watakatifu kwa kuwa muda wa kuwangojea ni mfupi”.

Askofu Ng’ang’a alisema 2024 dunia itajaa hamaki ya kivita dhidi ya mataifa “lakini Mungu atashikilia ulimwengu kwa njia ya kugeuza uvumi huo kubakia tu kuwa hekaya”.

 

[email protected]