• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Askofu Yohanna akiri ni mfuasi wa Arsenal na atazidi kutoa waumini wake mapepo   

Askofu Yohanna akiri ni mfuasi wa Arsenal na atazidi kutoa waumini wake mapepo  

NA MWANGI MUIRURI

NI wiki moja sasa tangu mkanda wa video kuhusu askofu matata Danson Gichuhi, akijulikana vyema kama Yohanna ujitokeze mitandaoni akimpapasa, kumbana na kumnyegeza muumini wa kike kwa msingi wa kumtoa mapepo.

Askofu Yohanna sasa analia kwamba anapitia magumu akikashifiwa mitandaoni na katika gumzo mitaani ilihali yeye, akisema, alikuwa akitekeleza yake ya kiroho kusaidia ulimwengu kufukuza mapepo.

Katika mkanda huo wa takriban dakika saba, Askofu Yohanna anaonekana akiwa amelala kando ya mwanamke ambaye amepandwa na jadhiba huku akimpaka mafuta spesheli kwa matiti na pia kwa sehemu zake za siri.

Wakati Askofu amemalizana na harakati za kumtoa mapepo kwa njia hiyo ya kipekee ambayo wengi sasa wanaamini ni mfano wa uhaini wa kidini, mwanamke huyo anarejelewa na fahamu zake polepole na akionekana kuchangamka kwelikweli anatamka: “Askofu nusura uniue”.

Wachanganuzi mitandaoni wameshikilia kwamba mwanamke huyo amechangamka kihisia kuliko alivyokengeuka kiroho hivyo basi kugeuza hafla hiyo ya Askofu Yohanna kuwa kama ya kutumbuizana.

“Hapana, sio hivyo unadhania. Wakati unapomwona mwanamke huyo akijigaragaza akionekana kupandwa na hisia za kuchangamka kiajabu, ni mashetani yakimtoka na kuweka mwili wake huru na ndio sababu kuu ya kuonekana kama amenyegezwa,” Askofu akaambia Taifa Leo Dijitali.

Askofu Yohanna hupatikana sana katika baa moja ya Mjini Murang’a ambapo hujumuika hasa wakati timu ya Arsenali inacheza mpira kwa kuwa yeye ni mfuasi sugu wa masogora hao wanabunduki wa kocha Mikel Arteta.

Alisema kwamba yeye ni Askofu mzima ambaye ana kanisa linalojulikana kama Christian Committed Gospel Church lililo na matawi katika Kaunti za Murang’a, Nakuru na Kirinyaga”.

Mtandao wake wa Facebook unamtambulisha kama mchungaji ambaye hukomboa na kutoa ushauri nasaha kwa jina la Yesu Kristo wale wote waliotekwa nyara na mapepo.

Askofu Yohanna anasema kwamba alipata umaarufu katika kazi hii yake mwaka wa 2014 ambapo alifika katika boma moja Nakuru, kijijini Kuresoi ambapo mashetani yalikuwa yamevamia na hata kushambulia wachungaji 30 nusura yawaue isipokuwa ni vile walitoroka mbio kutoka eneo hilo.

“Lakini nilipofahamishwa, nilifika katika kijiji hicho na tukamulikana na mapepo hayo ana kwa ana na nikayaambia mimi sio wa kutishwa kama wenzangu. Tulipambana kwa siku nzima hadi yakatii na yakahama eneo hilo na kukawa salama,” asema.

Askofu Yohanna anasema kwamba ako katika kazi hiyo ya kupambana na mapepo kwa miaka 30 sasa na licha ya kuwa na ulemavu ambao haumwezeshi kutekeleza majukumu yake akiwa wima, anashikilia kwamba mapepo huwindwa kwa uteule maalum kutoka juu kwa Maulana.

Anafichua kwamba ulemavu wake ulitokana na maradhi ya Osteoarthritis na ambayo kuponywa, yanahitaji Sh600, 000 katika hospitali za kurekebisha ulemavu wa mifupa.

Kuhusu ni kwa nini yeye mwenyewe hawezi akajikomboa kutoka kwa pepo la ulemavu ili arejelewe na uzima wake wa miguu, Askofu Yohanna anasema kwamba “kuna mapepo ya magonjwa ambayo yanaweza tu kukabiliwa na madaktari hospitalini na kuna mapepo ya kiroho ambayo hutimuliwa na manabii wateule”.

Anasema kwamba yeye anaamini matibabu ya kisasa na ndiyo sababu ameelewa ulemavu wake ni wa kushughulikiwa na madaktari.

Anafichua kwamba mkanda huo wa video ukimwangazia katika hafla hiyo ya kumnusuru mwanamke kutoka kwa mapepo ulichukuliwa katika Kaunti ya Murang’a mnamo Februari 16, 2024.

Akiwa mzawa wa Kaunti ya Nakuru, Askofu Yohanna anasema kwamba mwanamke huyo alikuwa amesaka huduma za ukombozi kutokana na hali ya bwanake kutekwa nyara kiuchawi na mwanamke mwingine.

“Mwanamke huyo wa kichawi alikuwa amempumbaza bwanake na kumfanya ahepe familia yake. Katika harakati za kusaka afueni, mwanamke huyo alifika kwa mchawi ili naye apewe nguvu za kumvuta bwanake arejee kwa boma,” asema Askofu Yohanna.

Lakini hali iliishia kuwa mbaya wakati nguvu hizo za kichawi zilianza kumsumbua mwanamke huyo na ndipo akamwendea Askofu Yohanna ili atakaswe.

“Kwa kuwa alikuwa amepakwa mafuta ya kichawi kwa matiti na kwa nyeti zake, ni lazima nami ningempaka mafuta ya utakaso papo hapo kwa sehemu hizo,” akasema.

Askofu huyo alishikilia kwamba hakuna lolote nje ya maandiko matakatifu alikiuka kwa kuwa “huwezi ukakabiliwa na anayehitaji ukombozi wa kichwa nawe uende kumtibu mgongo…Unashughulikia eneo hasa lililo na shida”.

Alisema kwamba haja yake sio ya kupapasa wanawake kwa kuwa “mimi nina bibi, watoto na marafiki wengi nje ya huduma yangu ya kupambana na mapepo”.

Alisema kwamba yeye amejiorodhesha kwa jumuia ya walio na umuhimu sana hapa nchini kwa kuwa anasaidia nchi kupambana na majeshi ya giza yanayoandama wengi.

Alisema kwamba haogopi kusakamwa na serikali kwa kuwa “mimi sijatekeleza lolote kinyume na sheria za nchi na waumini wangu hawajalalamika”.

Aliteta kwamba “hawa watu wa mitandaoni kila kuchao wanapachika picha za aibu na hakuna anayewasakama, kwa baa naona watu wakiwa uchi na hakuna anayeteta lakini langu la imani la kuonekana nikitoa mwanamke mapepo linageuzwa na kupindwa hadi naonekana kama haini wa kidini… Si kitu, Mungu yuko katika kiti chake cha enzi na ataniulizia”.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Kundi la kina mama linavyotumia biashara ya miche kukomesha...

Waislamu 5,000 kufurahia msaada wa chakula Ramadhan

T L