Makala

Asomea taaluma ya uuguzi badala ya kujitia unyongeni ndoa kuenda ndivyo sivyo

November 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

BAADA ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE 2008, matamanio ya Regina Wangechi yalikuwa kusomea taaluma inayohusiana na masuala na huduma za afya, kama chaguo la kwanza.

Endapo asingemudu kuwa katika sekta ya afya, ambapo alitaka sana kuwa muuguzi, chaguo mbadala lilikuwa ualimu.

Hatimaye matokeo ya KCSE yalipotangazwa, alipata C+ na kwa sababu ya ukosefu wa fedha, baadhi ya ndugu zake wakiwa wangali shuleni, alilazimika kusomea ualimu.

Wangechi alituma maombi ya nafasi katika taasisi moja inayotoa mafunzo ya ualimu nchini, ambapo aliitiwa kozi ya chekechea, ndiyo Early Childhood Development Education, ECDE.

Licha ya changamoto za ukosefu wa karo nyakati zingine, anasema wazazi wake na ambao anakiri historia ya ufanisi wa maisha yake ikiandikwa hii leo majina yao hayatakosa kujumuishwa, walimpiga jeki pakubwa.

Alijiunga na taasisi hiyo 2009, na kwa kipindi cha muda wa miaka miwili baadaye akafuzu kwa cheti cha ECDE.

“Kibarua kilichofuata kikawa cha kutafuta kazi, tayari vyeti na stakabadhi za masomo zilionyesha nilikuwa mwalimu, ila nilihitaji kuonyesha umahiri huo kwa matendo darasani,” anaelezea.

Ari ya kuwa darasani kupevusha watoto na bidii za mchwa alizokuwa nazo, hatimaye zilizaa matunda baada ya kupata nafasi ya kazi katika mojawapo ya shule za mmiliki binafsi Nairobi.

“Nilifunza kiwango cha chekechea,” Wangechi anadokeza.

Ni kazi aliyojitolea mhanga kuifanya, na kwa neema za Mwenyezi Mungu shule iliyompa nafasi ya ajira ilikuwa ikitambua jitihada za walimu waliotia bidii, na alikuwa miongoni mwao.

Sawa na kijana yeyote yule anapobaleghe, Wangechi anafichua kwamba alikutana na barobaro ambaye baada ya kuchumbiana kwa muda aliuteka bakunja moyo wake.

Kilele cha uhusiano wao 2012 kikawa kuwa mume na mke. Licha ya kuwa jamaa huyo alitegemea vibarua vya hapa na pale kujiendeleza kimaisha, Wangechi anasema hakuangalia hali yale wakati huo “kwani nilifahamu ufukara hauna mizizi ikiwa mtu anatia bidii”.

Kulingana na simulizi yake, alitumia mapato yake kumpiga jeki, naye mumuwe hakumuangusha. Baraka za Mola huja kwa njia nyingi, na hatimaye walijaaliwa mtoto wa kiume ambaye kwa sasa yuko daraja la chekechea.

“Tulijitahidi na tukafanikiwa kununua kipande cha ploti kiungani mwa jiji la Nairobi,” anafichua mwanadada huyo.

Akidhania kuwa ndio sasa mambo yamekuwa mazuri, mambo yalianza kugeuka. Yalianza kwa uchachu, uchachu ukazidi uchachu kali, na hatimaye kuwa shubiri.

Wangechi anaelezea kwamba kilichoanza kama mzaha mumewe kuwa na wapenzi wengine, kiliishia kuwa dondandugu. Alipotaka kujua sababu ya mumewe kubadilika ghafla, majibu yalikuwa vita.

Hatimaye alihisi kuwa ndoa yake na aliyotamani kuipalilia iwe kivutio, isingeendelea tena.

Akaamua kuondoka, ila na makovu ya kidonda cha moyo, uamuzi unaopigiwa upatu na wataalamu na washauri wa masuala ya ndoa ikiwa ndoa imegeuka kuwa ukumbi au ngome ya vita.

“Ndoa ikigeuka kuwa uga wa vita, na endapo mazungumzo ya patanisho hayazai matunda mwathiriwa achague kuondoka,” anashauri Askofu Wilson Karanja, mtaalamu wa masuala ya ndoa, akionya kuwa baadhi ya mizozano kwenye ndoa inaweza kuchangia maafa.

Kauli ya mdau huyo inawiana na ya Dianah Kamande, ambaye alinusurika kifo kwa tundu la sindano katika ndoa yake.

Anasema mumewe aliyemjua kama mwanaume mpole na mwenye heshima, usiku mmoja alimgeukia kwa panga na baada ya kumtendea unyama usiomithilika, jaribio sawa na hilo kwa wanawe lilizuiwa na waliotika mzozano kati yao.

Mama huyo ambaye kwa sasa ni mjane na mwasisi wa Shirika lisilo la Kiserikali, Cometogether Widows and Orphans Organization, linalojibidiisha kuangazia changamoto za wajane, mayatima na dhuluma za kijinsia, anasema muhimu zaidi kwa mwathiriwa ni kutafuta amani.

“Vita na dhuluma za kijinsia kwenye ndoa vimesababisha maafa ya wanaolegea kuiondokea. Amani na utulivu ni muhimu,” Dianah anaelezea.

Kuondokea ndoa tata kabla maji kuzidi unga, ni uamuzi wa busara ambao Regina Wangechi anausifia kwani ulimfungulia awamu nyingine ya maisha.

Mwaka uliopita, 2019, mwanadada huyo ambaye ni mama wa mtoto mmoja aliacha kazi ya ualimu, akiwa na lengo, lengo la kufufua azimio lake kuwa katika sekta ya afya.

Mapema mwaka huu, 2020, Wangechi, 30, baada ya kutuma maombi ya kusomea taaluma ya uuguzi katika chuo cha mafunzo ya utabibu, KMTC, alipata mwaliko.

Licha ya mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19 nchini, uliochangia shule zote na taasisi za elimu ya juu kufungwa Machi 2020, Wangechi angali na matumaini ataafikia ndoto zake, ndoto za kuwa muuguzi.

Kufuatia kufunguliwa kwa gredi ya nne, darasa la nane na kidato cha nne, pamoja na wanafunzi wa taasisi na vyuo vikuu, mwezi uliopita, hasa wanaofanya mtihani wa mwisho, mwanadada huyo anasema kwa sasa wanaendelea kupata mafunzo mitandaoni.