Athari za vita vya Israel-Iran kwa Kenya
LUKE ANAMI na CHARLES WASONGA
HATUA ya Iran kuishambulia Israel mnamo Jumamosi, Aprili 13, 2024 inaweza kusababisha changamoto ya kidiplomasia na kibiashara kwa Kenya na majirani zake zinazojaribu kutoonekana kuunga upande wowote katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.
Huenda shughuli za kuagiza mafuta, nafaka na vifaa vya kiufundi zinazoagizwa kutoka nje kuletwa Kenya zikaathirika na mashambulio ya hivi punde katika eneo hilo.
Na tayari Waziri wa Biashara, Rebecca Miano ametambua athari za vita hivyo kwa biashara kati ya Kenya na mataifa hayo ya Mashariki ya Kati.
Jumamosi usiku, Iran ilitekeleza mashambulio kadha ya makombora na droni nchini Israel huku taharuki ikiendelea kupanda eneo hilo kutokana na vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza.
“Kenya inasikitishwa zaidi na hatua ya Irani kuishambulia taifa la Israel. Hali hii ya kukera itazidisha misukosuko inayoendelea kushuhudiwa eneo la Mashariki ya Kati,” Rais Ruto alisikitika kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X.
“Shambulio hilo ni tishio halisi kwa amani na usalama kimataifa na linakiuka Mikataba ya Umoja wa Mataifa na lapasa kulaaniwa vikali na nchi zote zinazopenda amani,” akaongeza.
Shirika la habari la kitaifa nchini Iran lilisema shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi baada ya Israel kufanya shambulio la angani dhidi ya kituo cha kidiplomasia cha Irani nchini Syria mnamo Aprili 1, 2024.
Israel imekuwa ikitekeleza mashambulio nchini Syria dhidi ya vituo vya Irani na washirika wake kwa miaka mingi na ndani ya miezi sita ya operesheni yake dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Lakini shambulio la Aprili 1 lilikuwa la aina yake ikizingatiwa kuwa lililenga kituo cha kidiplomasia ambacho kwa kawaida husazwa wakati wa vita.
Aidha, shambulio hilo lilikuwa la aina yake kwa sababu lilionekana kulenga maafisa wa Iran wa cheo cha juu.
Shirika la habari la kitaifa la Iran lilisema hatua ya Iran kushambulia jengo la ubalozi wa Iran jijini Damascus, Syria lilisababisha vifo vya wanachama wa Iran Islamic Revolutionary Guard Corps, akiwemo kamanda wa cheo cha juu Mohammad Reza Zahedi na Brigedia Jenerali Mohammad Hadi Haj Rahimi.
“Kujibu vitendo hivi vya uchokozi, Kenya inatoa wito kwa Israel ijizuie kwa kuzingatia haja ya pande zote kujiepusha na vita vitakavyosababisha uharibifu mkubwa,” akaeleza Rais Ruto.
Ikitoa kauli yake kufuatia hatua ya Iran kutekeleza mashambulio nchini Israel, Afrika Kusini ilielezea kusikitishwa na matukio hayo.
“Alivyosema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kuna hatari kubwa ya machafuko makubwa kutokea katika eneo hilo,” taarifa kutoka serikali ya Afrika Kusini ilisema.
“Katika hali hii, Afrika Kusini imesisitiza kuwa pande zote sharti zijizuie na kukomesha kitendo chochote ambacho kinaweza kuongeza taharuki katika eneo la Mashariki ya Kati ambalo tayari linakumbwa na vita.
Afrika Mashariki, Upembe mwa Afrika na Kusini mwa Afrika zinakabiliwa na changamoto katika uuzaji na uagizaji bidhaa katika Mashariki ya Kati, kutokana na uwezekano wa kutokea vita vikubwa eneo hilo.
Waziri wa Biashara nchini Kenya, Rebecca Miano alionya kuwa vita katika mashariki ya kati vinaweza kuathiri usafirishaji wa bidhaa na huduma kutoka Afrika kuelekea eneo la Ghuba na Bara Uropa.
“Athari kubwa ni kuvurugwa kwa mfumo wa usafirishaji bidhaa hadi masoko ya Mashariki ya Kati na Uropa. Afrika yote itaathirika,” akasema Bi Miano.
Kwa mfano, usarifishaji wa bidhaa ambazo Kenya huagiza kutoka mataifa kama China, Milki ya Umoja wa Kiarabu (UAE), India, Malaysia na Saudi Arabia huenda ukaathirika kutokana na vita hivyo.
Waziri Miano alionya kuwa endapo hali itakuwa mbaya zaidi, huenda Kenya na majirani zake zikalazimika kusaka suluhu za kinyumbani.
“Matukio katika Mashariki ya Kati ni funzo kwa nchi mbalimbali kujizatiti kujitegemea hususan katika nyanja ya utengenezaji wa bidhaa za viwanda. Tunapaswa kuanza kutengeneza bidhaa ambazo ni muhimu kwetu jinsi tulivyofanya wakati wa janga la Covid-19 tulipoanza kutengeza vitu ambavyo t ulikuwa tukiagiza nje kama vile chanjo,” akasema Miano.
Kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, gharama ya usafirishaji bidhaa baharini ilipanda kwa Dola 500 (Sh75,000) kwa konteina huku mapato kutokana na biashara ulimwenguni yakishuka kwa kima cha asilimia 42.
Hii ni kulingana na ripoti ya hali ya kibiashara iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Maendeleo ya Kibiashara (UNCTAD) Machi 2024.
Kwa mfano, katika mkondo wa usafirishaji wa Kaskazini (Northern Corridor) unaohudumia Uganda, Sudan Kusini, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kahawa na majani chai kutoka Uganda na Kenya ilikwama katika mabohari kwani wauzaji walivunjwa moyo na gharama ya juu za usafirishaji baharini.
Hii ni kutokana na ongezeko la hitaji la vyombo vya usafirishaji kama vile meli.
Kando na vita katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati, katika eneo hili, vita vinavyoendelea mashariki mwa DRC vimeathiri usafirishaji wa bidhaa na huduma katika eneo la Afrika Mashariki.
“Vita havitakoma. Kwa hivyo ipo haja ya suluhu za kidiplomasia na kisiasa. Mikataba mbalimbali ya Umoja wa Mataifa imeweka wazi njia za kupambana na mapigano chini ya sheria za kimataifa,” akasema Profesa Ben Shihanya, mwanasheria mwenye uzoefu katika masuala ya Kikatiba demokrasia ya kimataifa.
Rais wa Amerika Joe Biden alilaani mashambulio dhidi ya Israel.
Aliongea na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu kukariri Amerika imejitolea kuihakikishia Israel usalama wao.