AWCON: Safari ya #HarambeeStarlets kutinga fainali Accra
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya almaarufu Harambee Starlets itakuwa kwenye droo ya Kombe la Afrika (AWCON) itakapofanywa Oktoba 21 jijini Accra nchini Ghana baada ya kurejeshwa mashindanoni hapo Oktoba 17, 2018.
Starlets ilinufaika na Equatorial Guinea kupigwa marufuku kushiriki mashindano haya ya mataifa manane kutokana na udanganyifu wa kutumia mchezaji Anette Jacky Messomo, ambaye inasemekana si wa taifa hilo.
Kenya inaungana na Ghana, Zambia, Afrika Kusini, Mali, Cameroon, Algeria na mabingwa watetezi Nigeria katika Kombe la AWCON litakalofanyika Novemba 17 hadi Desemba 1 mwaka 2018.
Mwaka 2016, Equatorial Guinea ilipigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kushiriki mashindano yake yote yakiwemo mechi za kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016 pamoja na Kombe la Dunia mwaka 2019 kutokana na udanganyifu huu.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lilikuwa bado limeruhusu Equatorial Guinea kushiriki mashindano yake yakiwemo mechi za kufuzu kushiriki AWCON mwaka 2018 kabla ya kuipiga marufuku hapo Oktoba 17 na pia kuiamrisha ilipe faini ya Sh1, 008,985 za Kenya.
Kenya ilishtaki Equatorial Guinea kwa kuchezesha wachezaji ‘mamluki’ katika mechi za raundi ya pili ya kufuzu kushiriki AWCON mwezi Juni mwaka 2018. Starlets ilishinda Equatorial Guinea 2-1 Juni 6 uwanjani Machakos kabla ya kupigwa 2-0 Juni 9 katika mechi ya marudiano jijini Malabo na kubanduliwa nje.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) liliandikia CAF barua rasmi ya malalamishi mnamo Juni 9 likishuku Equatorial Guinea ilitumia wachezaji sita dhidi yake ambao hawakuwa wa nchi hiyo.
Kamati ya Nidhamu ya CAF iliandaa kikao chake katika makao makuu ya CAF jijini Cairo nchini Misri juma hili kabla ya kutangaza uamuzi wa kutupa nje Equatorial Guinea hapo Oktoba 17.
Licha ya kufurahi kupata tiketi ya kushiriki AWCON kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuwa katika makala ya mwaka 2016, swali kubwa linalosalia ni je, Starlets itahudhuria?
Tangu Agosti, FKF imekuwa ikilia sana kuhusu hali yake ya kifedha. Ina zaidi ya kesi 10 mahakamani zikiwemo kutoka kwa makocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanaume – Adel Amrouche na Bobby Williamson wanaotaka fidia ya zaidi ya Sh100 za Kenya baada ya kandarasi zao kukatizwa. Akaunti za benki za FKF pia zilifungwa na Halmashauri ya Kutoza Ushuru (KRA) kutokana na deni la Sh44 milioni ambalo ni malimbikizi ya ushuru.
Wizara ya Michezo imekuwa ikisema haipati fedha za kutosha kutoka kwa Serikali. Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) ni moja ya mashirikisho yatakayofuatilia kwa makini hatua ambayo wizara itachukua kusaidia Starlets hasa baada ya kuomba isaidiwe kuandaa timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Simbas.
KRU imefutilia mbali mechi tatu za kirafiki za Simbas kutokana na ukosefu wa fedha. Simbas inajiandaa kwa mechi muhimu za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2019.
Vijana wa kocha Ian Snook watapimana nguvu dhidi ya Romania pekee yake mapema mwezi Novemba kabla ya kuenda Ufaransa kumenyana na Canada, Hong Kong na Ujerumani kati ya Novemba 11 na Novemba 23 katika mchujo ambao mshindi atajikatia tiketi ya kuelekea Japan mwaka 2019.
Kenya itajipata katika upande mbaya wa sheria ikikosa kupeleka Starlets nchini Ghana mwezi ujao kwa Kombe la Afrika. Kwa sasa hata hivyo, FKF inatarajiwa kuanza kuandaa ratiba ya mazoezi ya Starlets na mipango ya kuleta wachezaji wanaosakata soka nje ya Kenya kama Esse Akida aliyetua Israel wiki moja iliopita.
Ethiopia pia ilikuwa imewakilisha kesi kama ya Kenya dhidi ya Algeria, ingawa bado CAF haijatangaza uamuzi wake. Ethiopia ilidai kwamba Algeria ilitumia wachezaji wawili dhidi yake ambao hawakustahili.
Ilisema kwamba beki Isma Ouadah na kipa Nedjat Fadoul waliwakilisha nchi ya Milii za Kiarabu kati ya mwaka 2010 na 2015 kabla ya kuchezea Algeria katika mechi za kufuzu dhidi ya Ethiopia mwezi Juni mwaka 2018.
Wakati wa droo, CAF itaunda makundi mawili ya timu nne nne. Aidha, Carolyne Wanjala na Mary Njoroge kutoka Kenya watakuwa nchini Ghana kama refa na refa msaidizi, mtawalia, wakati wa kombe la AWCON.