AWINO: Kilimo cha parachichi kimevutia pato bora kwa wakulima
Na AG AWINO
TAARIFA kwamba Kenya iliuza katika nchi za nje parachichi nyingi na kuongezea mapato yake ni njema na ya kuigwa na wakulima wa mazao mengine.
Kulingana na Umoja wa Wauzaji wa Parachichi, parachichi kutoka nchini Kenya huuzwa kwa kiwango kikubwa katika Milki za Kiarabu, Qatar na Saudi Arabia. Katika nchi hizi, parachichi hununuliwa sana hata kushinda mahitaji katika bara Uropa ambalo pia limekuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa hii.
Ripoti zinaonyesha kwamba Kenya iko katika nafasi ya mbele hata kuliko nchi nyingine kama vile Afrika Kusini katika kuuza takribani tani elfu hamsini ya jumla ya takribani tani 200 elfu ambayo huvunwa katika mwaka mmoja.
Mwaka huu ambapo janga la corona limeathiri sekta nyingi za kiuchumi, kiwango cha parachichi kilichouzwa katika nchi kama vile Uholanzi kiliongezeka na kuzidisha mapato kwa wakulima na wauzaji.
Swali ni je, ni nini ambayo wakulima hawa hufanya ambayo wenzao wa miwa hawawezi kufanya?
Kuna sababu nyingi. Kwanza parachichi huchukua muda mrefu kuliko miwa shambani na huhitaji baina ya miaka mitano hadi 13 kukua ilhali miwa huchukua chini ya miaka miwili. Kwa hivyo huhitaji uwekezaji wa muda mrefu. Pia, matumizi ya sukari ni mengi zaidi ikilinganishwa na parachichi ambayo mara nyingi hutumika kuongezea protini mwilini, kutengeneza mafuta ya nywele na pia hutumika kama siagi. Sukari kwa upande mwingine, hutumika kutengeneza biskuti, maandazi, pombe, sharubati, chai na vingine vingi. Yaani kwa kweli sukari ina matumizi zaidi kuliko parachichi na kwa hivyo pia ina wanunuzi wengi kuliko parachichi.
Wakulima na wanunuzi wa parachichi wana umoja wenye nguvu na ambao hutafuta soko katika nchi za nje na pia hupigania nafasi yao humu nchini.
Tofauti ni kwamba umoja huu unatawaliwa kwa kiwango kikubwa na wafanyabiashara na wataalamu ambao tayari wamejua kiwango cha ubora kinachohitajika katika nchi za nje. Wanaongozwa na faida tu. Aidha, wanajua wakati mahitaji yameongezeka katika nchi za nje na ubora ambao mazao haya sharti udumishe. Hutawapata wakililia serikali ili kuwainua kifedha au kuajiri wakurugenzi wa makabila yao kuendesha kampuni za sukari.
Wanaofanya kilimo cha parachichi ni watu ambao washaelewa ni masoko yapi ambayo wanalenga. Ni watu wanaowekeza katika kilimo bila kutegemea mvua isiyojilikana itakuja lini. Hawatagemei wanasiasa kuwaahidi mageuzi fulani wanapotafuta kura ya kuingia bungeni au mabaraza ya kaunti.
Wakulima wa parachichi tayari wameonyesha kwamba kilimo hiki kinaweza kuleta faida iwapo kitaendeshwa kwa kitaalamu bila kutegemea ndoto za wanasiasa ambao kila mara hawana haja na wakulima.