AWINO: Mikakati inayopendekezwa kukabili nzige isigeuke janga
Na AG AWINO GILBERT
WIKI jana, Wakenya walishuhudia sarakasi kwenye darubini ya Kamati ya Afya bungeni kuhusu madai ya wizi na ufujaji uliodaiwa kutekelezwa katika shirika la kiserikali linalohusika na usambazaji wa bidhaa za afya (Kemsa).
Kwenye darubini hiyo, ambayo ilifanyika ndani ya Bunge, mmoja wa wafanyabiashara aliyepewa kandarasi ya mamilioni ya pesa alichekesha wananchi alipodai eti chanzo cha kupewa kandarasi na Kemsa kilitokana na bahati nzuri ya ziara yake.
Ingawa kuna maswali mengi ambayo tunaweza tukajiuliza kutokana na madai ya mfanyabiashara huyu, madai yake yanapiga darubini kiwango cha uozo na ufisadi unaoshuhudiwa kila wakati ambapo Kenya inajikuta katika mkasa fulani. Kwa mfano, mwaka jana, mabilioni ya pesa yalipotea katika kaunti mbalimbali. Pesa hizi zilikuwa zimenuiwa kutumiwa katika sekta ya afya.
Kabla ya janga la corona, mkasa ambao ulikuwa tishio sana ulikuwa uvamizi wa nzige ambao walishuhudiwa Nairobi, Meru, Magharibi na hata katika sehemu za Turkana. Ilihofiwa kwamba kuwepo kwao kungetumbukiza nchi katika baa la njaa na ukosefu wa chakula. Ingawa nzige hawa hawakumalizwa kabisa licha ya serikali kujaribu mbinu mbalimbali za kuwakabili kama vile unyunyiziaji dawa kwa kutumia ndege maalumu mapema mwaka huu, ripoti zimeanza kusambaa kuhusu kuwepo kwao katika kiwango hatari. Cha ajabu ni kwamba kemikali ambazo zilitumiwa kunyunyizwa sasa zimekuwa donda ndugu kwani zina madhara mengi kiafya. Imedaiwa kwamba zinaleta magonjwa kama vile saratani.
Licha ya kwamba Katibu wa Elimu ya Juu na Utafiti, Bw Samson Nabukwesi amelalamika kwamba kila kuchao, imekuwa vigumu kukabiliana na wadudu hawa kwani dawa zilizodhaniwa kuwa na uwezo wa kuwaua hazifanyi kazi tena, kilio hiki hakitoshi licha ya kuungwa mkono na wadau wengine kwani Mkurugenzi Mkuu wa Akiba ya Kitaifa Kuhusu Utafiti (NRF) Dkt Jemima Onsare amesema hawana pesa za kutosha za kukabili nzige.
Wanasayansi
Swali la kujiuliza ni kwamba, mbona wanasayani wetu huachwa nyuma kila mara na kuishia kulalamikia tu ukosefu wa fedha kama sababu moja kuu ya kukosa kutekeleza wajibu wao?
Ni aibu kwamba baada ya mabilioni kutumiwa – kwa ushirikiano na ushauri wa asasi za sayansi na utafiti, badala ya kuomba msamaha kwamba walikuwa wamekosea katika kukubali matumizi ya kemikali, wanalilia fedha. Mbona hawakupendekeza njia mbadala tangu zamani?
Sikatai kwamba utafiti wa kisayani huhitaji fedha nyingi tena kwa muda mrefu. Hata hivyo, wanasayansi wamekuwa kama limbukeni ambao pia wanajaribu tu. Miezi michache iliyopita, madaktari walikuwa wakitifua vumbi pindi wanapoona mgonjwa waliyedhani alikuwa na corona.
Kwa kuwa pesa nyingi hupotea na kuibwa wakati wa mikasa, lazima njia mwafaka zibuniwe kwa wakati unaofaa ili mkasa huu wa nzige usiwe nafasi nyingine kwa walafi kujitajirisha badala ya kuokoa wananchi. Licha ya kwamba katika kila mkasa kuna wale wanaofaidi, mikasa isitumiwe na wataalamu kufilisi rasilimali za wananchi.