Makala

Baa za ngome ya Gachagua zapata idhini ya mahakama kuhudumu

March 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

MUUNGANO wa wamiliki wa baa katika eneobunge la Mathira atokako Naibu Rais Rigathi Gachagua, umepata afueni mahakama ikiamuru biashara zao zilizokuwa zimefungwa zifunguliwe mara moja.

Mahakama ya Nyeri iliagiza mnamo Ijumaa kwamba baa zote eneo hilo ambazo ni zaidi ya 300 zilizokuwa zimefungwa katika kampeni inayoongozwa na Bw Gachagua, zirejelee kuhudumu.

Hii ni baada ya wamiliki hao, wakiongozwa na Kamati Shirikishi ambayo mwenyekiti wake ni Jimmy Ruhando, kuwasilisha kesi mahakamani.

Walalamishi walidai kwamba amri ya kufunga baa zao ilikuwa na dosari kwa kuwa haikuzingatia haki za kimsingi za kibiashara na za binadamu.

Wahudumu wa baa katika eneobunge la Mathira wakiwa katika mkutano mjini Karatina ambapo walifahamishwa kwamba mahakama imewarejeshea uhuru wa kufungua biashara zao baada ya kufungwa katika vita vilivyoanzishwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua. PICHA | MWANGI MUIRURI

Wamiliki wa baa mjini Karatina ambao ndio mji mkuu wa eneobunge la Mathira nao waliteta kwamba “tunamalizwa na viongozi wetu pasipo kuzingatia haki”.

Mwenyekiti wao Bw Charles Wachira alisema wanaunga Bw Gachagua katika vita dhidi ya pombe ya mauti.

“Kile ambacho tunapinga ni vita hivi kuelekezwa kwa biashara halali na ndio sababu tumeenda mahakamani,” akasema Bw Wachira.

Bi Jane Njihia ambaye amekuwa katika biashara ya baa kwa miaka 38 sasa alisema alijuta kufanyia kampeni kuchaguliwa kwa serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto.

“Licha ya kutumia rasilimali zangu kuvumisha kampeni zao huku Mathira, wamenilipa wema wangu kwa ukatili wa kunifungia baa,” akalalama Bi Njijhia.

Kamishna wa Nyeri Pius Murugu alisema licha ya agizo hilo la mahakama, vitengo vya udumishaji wa usalama vitaendelea mbele na operesheni dhidi ya pombe ya mauti, mihadarati na wanaokiuka masharti ya kisheria katika biashara ya vileo.

Maafisa wamwaga pombe katika eneo la Mathira kwenye operesheni kali. PICHA | MWANGI MUIRURI

Baa zilizokuwa zimefungwa ni zile ziko katika maeneo ya makazi vijijini na pia zilizo umbali wa chini ya mita 300 kutoka taasisi za elimu.

Katika ilani ambayo imekabidhiwa makamanda wa stesheni zote za polisi, hakuna baa yoyote ambayo inafaa kufungwa hadi kesi iliyowasilishwa isikilizwe na iamuliwe.

Hii ni mbinu ambayo imekuwa ikitumika na wengi wa wamiliki wa mabaa kupinga msako huo wa Bw Gachagua, wenzao wa Murang’a tayari nao wakiwa wametoa ilani ya kwenda mahakamani wakati wowote nao kupinga ilani ya baadhi ya baa kufungwa.

Hili ni pigo kuu kwa vita hivyo ambavyo mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi pamoja na Seneta wa Nyeri Bw Wahome Wamatinga tayari wametoa onyo hadharani kwamba wataunga kikamilifu amri ya Bw Gachagua kwamba baa zipunguzwe na pia pombe za mauti ziandamwe na ziharibiwe.

Bw Gachagua tayari ameonya kwamba mahakama imekuwa kimbilio la walio na nia ya kukwepa uwajibikaji katika vita dhidi ya ulevi kiholela, pombe za mauti na mihadarati.

[email protected]