Baada ya kunyolewa na ‘wembe ule ule’, Ben Githae asema hana haraka kutunga wimbo wa siasa
MWANAMUZIKI maarufu wa injili Ben Githae, anayejulikana kwa kuzua midahalo ya kisiasa kupitia muziki wake, ameendelea kuvutia hisia mseto katika juhudi zake za kurejesha ushawishi wake wa kisiasa na kijamii katika eneo la Mlima Kenya.
Githae aliibua taharuki mwaka 2017 baada ya kuacha nyimbo za kiroho na kuimba “Uhuru-Ruto Tano Tena”, wimbo uliotumiwa kupigia debe serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.
Tangu wakati huo, safari yake ya kisiasa imekuwa ya kupanda na kushuka, mara nyingi ikimsukuma kubadili misimamo kulingana na mwelekeo wa siasa za eneo analolitegemea kimuziki.
Katika miezi sita iliyopita pekee, Githae ameonekana akifanya mazungumzo au kushiriki shughuli katika mirengo mitatu tofauti ya kisiasa, kuanzia ziara ya wasanii kwa Naibu Rais Kithure Kindiki Mei 23, 2025, hadi kuhudhuria Mkutano wa Kitaifa wa Jubilee ulioongozwa na Rais mstaafu Kenyatta mnamo Novemba 7, 2025.
Jumanne hii, alionekana tena Murang’a akisalimiana hadharani na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, hatua iliyojiri baada ya miaka ya mivutano ya kimyakimya kati yao.
Wakiwa katika mazishi ya Herbert Kareithi, Githae alimwambia Gachagua kwamba ameacha “kubeba mizigo ya zamani” na yuko tayari kuunga mkono maslahi ya jamii.
Gachagua alimshukuru kwa “kuona mwanga,” akisema msanii yeyote hawezi kustawi Mlima Kenya akihubiri siasa ambazo hazipendwi na wakazi. Aidha, aliondoa msimamo wake mkali wa awali wa kuwatenga wasanii waliopinga msimamo wa eneo, akisema “wakati wa kuwasamehe umefika.”
Safari ya Githae imekuwa na misukosuko: kutoka “Wembe ni ule ule” baada ya mahakama kufuta matokeo ya 2017, hadi kujiunga na Azimio 2022 na kuimba kwamba “mlima umetekwa,” hatua ambayo sasa anaiita “ujinga.”
Anakumbuka vyema uchaguzi wa mwaka huo ilipodhihirika kuwa alikosea katika utabiri wake kuhusu kura ambazo Azimio ingepata Mlima Kenya.
Mnamo Mei 2025, alijaribu kurejea na wimbo wa “Kindiki ni wetu,” lakini alishambuliwa vikali mtandaoni na kulazimika kuomba msamaha. Tangu hapo amesisitiza kuwa maamuzi yake—si watu—ndio yalikuwa shida, na sasa anadai kuwa “ameamua kutembea na mashabiki wake.”
Mwanamuziki huyo anasema msukumo wa kuingia kwenye muziki wa kisiasa ulitokana na urafiki wake binafsi na Rais mstaafu Kenyatta, ambaye anamtaja kama “kaka.” Anasema nyimbo zake zilimletea mafanikio ya kifedha kutokana na ukarimu wa rais huyo wa zamani.
Lakini mvutano wa 2022 kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto ulimweka njia panda. Anadai Gachagua, alipoingia mamlakani kama Naibu Rais, alimfanya kupitia “kipindi kigumu” kwa kumtaja msaliti wa jamii.
Leo, anasema ameamua kuacha chuki nyuma na kuanza ukurasa mpya.
Kuhusu uchaguzi wa 2027, Githae anakiri kuwa hatungi tena wimbo wa kisiasa hadi awe na uhakika wa “hali ya hewa ya kisiasa,” akisema msanii anaweza “kujiangamiza kabisa” kwa kusoma vibaya mwelekeo wa kura.
Kwa sasa, anasubiri upepo wa siasa utakapoelekea kati ya mrengo wa Dkt Fred Matiang’i, anayeungwa mkono na Rais mstaafu Kenyatta, na ule wa Gachagua—mirengo miwili ndani ya Muungano wa Upinzani.
Kwa Githae, hatima yake ya kisiasa iko wazi: “Mashabiki wangu ni wafalme. Nitakuwa upande wao.”