Baba hatarini kutupwa jela baada ya mwanawe ‘gaidi’ aliyemsimamia dhamana kuyoyomea Msumbiji
MWANAMUME amepata pigo baada ya Mahakama Kuu kumuamuru alipe faini ya Sh1.5 milioni la sivyo afungwe jela, kufuatia kutoweka kwa mwanawe aliyekimbilia Msumbiji na kujiunga na magaidi.
Rashid Mohamed sasa ana hadi Desemba 11 kulipa fedha hiyo baada ya mwanawe, Salim Mohamed Rashid almaarufu Chotara, kukosa kuhudhuria kesi kortini licha hati za kukamatwa kwake kutolewa.
Katika uamuzi uliotolewa Novemba 27, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa Rashid, kama mdhamini, alishindwa kutimiza wajibu wa kuhakikisha Salim anahudhuria vikao vya mahakama.
Mahakama ilisema kuwa, Salim hakuwa na haki ya dhamana na kwamba wadhamini wanatakiwa kulipa kikamilifu kiasi cha dhamana ya Sh1.5 milioni kila mmoja.
Aidha, mahakama iliagiza kuwa endapo watashindwa kulipa, magari mawili yaliyotolewa kama dhamana yauzwe ili kurejesha fedha hizo, ikibainisha kuwa kifungo cha jela kitazingatiwa tu iwapo fedha hazitapatikana kutokana na mauzo ya mali hiyo.
“Ninaamuru walalamishi walipe Sh1.5 milioni kila mmoja kufikia Desemba 11, 2025. Iwapo kiasi hicho hakitalipwa, na hakiwezi kupatikana kutokana na mauzo mali iliyotolewa kama dhamana, walalamishi watatumikia kifungo cha miezi sita gerezani,” mahakama ikaamua.
Kwa Bw Rashid, hatua aliyochukua kwa upendo imegeuka kuwa mzigo mzito unaomweka karibu na vifungo vya jela, akiadhibiwa si kwa makosa yake, bali kwa kile mwanawe alichokigeuka.
Mnamo Juni 6, 2019, Salim alishtakiwa kwa kuwa mwanachama wa Al-Shabaab na kwa kumiliki vifaa vya kutengeneza vilipuzi.
Alikana mashtaka hayo, na baada ya miezi miwili rumande, mahakama ilimpa dhamana ya Sh3 milioni, baadaye ikapunguzwa hadi Sh1.5 milioni, kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili.
Bw Rashid aliwasilisha magari mawili kama dhamana ili kumpatia mwanawe uhuru wa muda huku kesi ikiendelea kusikizwa.
Mwanzoni, Salim alihudhuria mahakamani bila kukosa.
Hata hivyo, kufikia Oktoba 7, 2020, alitoweka. Uchunguzi wa baadaye ulibaini kuwa alikimbilia Msumbiji, akaungana na wanamgambo wa Islamic State, na akapanda ngazi za uongozi ndani ya kundi hilo.
Kutoweka kwake kulisababisha mahakama kuwaita wadhamini wajieleze kwa nini dhamana yao isichukuliwe na serikali.
Mnamo Mei na Oktoba 2021, Bw Rashid aliieleza mahakama kuwa Salim hajarudi nyumbani tangu Desemba 4, 2020.
Aliripoti kutoweka kwake kwa polisi chini ya OB 15/5/12/2020 na kutoa taarifa kwa Kitengo cha Kupambana na Ugaidi (ATPU).
Mahakama iliwaelekeza wadhamini kushirikiana na wachunguzi wa kesi na kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu juhudi za kumtafuta.
Mnamo Julai 10, 2023, Bw Rashid aliijulisha mahakama kuwa familia imepata taarifa kwamba Salim alikamatwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuhukumiwa kunyongwa kwa kumuua mwanajeshi wa nchi hiyo.
Hata hivyo, Mei 27 mwaka huu, mahakama ya mahakimu ilibaini kuwa hakuna ushahidi thabiti unaoonyesha kwamba Salim amefariki, na ikahitimisha kuwa wadhamini walishindwa kutekeleza wajibu wao.
Bw Rashid, ambaye hakuridhika na uamuzi huo, aliomba Mahakama Kuu iupitie upya uamuzi huo, lakini mahakama hiyo iliunga mkono uamuzi wa mahakama ya mahakimu.
Kwa sasa, Bw Rashid anakabiliwa na shinikizo la kulipa Sh1.5 milioni au kufungwa miezi sita.
Salim alikamatwa nchini DRC akiwa na washirika wake wawili mjini Beni, karibu na Hifadhi ya Taifa ya Virunga na Milima ya Rwenzori.
Walikuwa wakijaribu kusafiri kuelekea Afrika Kusini waliponaswa na wanajeshi waliowashuku kuwa wapiganaji wa Allied Democratic Forces (ADF).
Katika DRC, Salim alishtakiwa kwa kumuua mwanajeshi na akahukumiwa kunyongwa.
Hata hivyo, familia yake ilitumai serikali ya Kenya ingeomba arejeshwe ili kutumikia kifungo chake nchini, lakini hilo halikufanikiwa.
Kufikia umri wa miaka 28, Salim alikuwa miongoni mwa watuhumiwa watano wa ugaidi waliotangazwa na DCI, ambapo mnamo Novemba 9, 2021, serikali ilitoa ofa ya Sh10 milioni kwa yeyote atakayetoa taarifa kuhusu aliko.
Baadaye, wachunguzi walifuatilia safari yake kupitia Msumbiji na DRC hadi kwenye mtandao wa misimamo mikali ulioko Kwale, ambao ni sehemu ya mtandao mpana wa usajili wa wapiganaji wa Al Shabaab na Islamic State katika ukanda huu.