Babu, 80, arudi chuoni kusaka digrii
NA ELIZABETH OJINA
MZEE mwenye umri wa miaka 80 amesajiliwa katika Chuo cha Kilimo cha Bukura kuendeleza masomo yake.
Katika umri wake, Mzee Henry Mulongo Mukhanu anapaswa kuwa nyumbani akichunga mifugo au akisimamia shughuli katika shamba lake lililoko Cheranganyi Hills, Kaunti ya Trans Nzoia.
Je, nini kilifanya babu huyu, aliyehudumu kama afisa wa mifugo katika Wizara ya Kilimo kwa miaka 35, kurudi darasani baada ya kustaafu miaka 19 iliyopita?
“Wanangu waliniambia; baba, ulikosa nafasi ya kuendeleza masomo yako ili utusomeshe. Huu ndio wakati wa kukulipa,” Bw Mulongo anaeleza.
Vile vile, sababu nyingine iliyomfanya arudi darasani ni kuwapa motisha vijana.
“Iwapo babu wa miaka 80 anaweza kurudi chuoni, basi hakuna umri unaoweza kuzuia mtu kusoma,” alisema mkongwe huyu ambaye pia anapenda kuandika vitabu.
“Ninapenda kuandika vitabu. Lakini wasomaji hawatachukulia kazi yangu kwa umakini iwapo elimu yangu ni ya kiwango cha chini,” anahoji.
Alipomaliza masomo yake katika Kidato cha Sita Shule ya Eldoret Hill mnamo 1969, Bw Mulongo aliajiriwa katika Wizara ya Kilimo kama afisa wa mifugo 1970.
Akiwa hapo alipata nafasi nyingi za kunoa bongo ikiwa ni pamoja na masomo ya miezi mitatu nchini Uholanzi kupata mafunzo ya ufugaji ng’ombe wa maziwa.
Baba huyu wa watoto wanane bado alikuwa na hamu ya kujiendeleza kimasomo hata alipoweka kando azma yake ili asomeshe wanawe.
Akaahidi kuwa siku moja angerudi darasani kutimiza ndoto yake.
“Hamu ya kutaka kuendelea na masomo imekuwepo kwa muda mrefu. Hivyo, watoto wangu walipopendekeza mwaka jana nijiunge na chuo nilikuwa tayari kabisa,” aeleza Bw Mulongo ambaye anasomea Ustawi wa Uzalishaji na Afya ya Wanyama katika Chuo cha Ukulima cha Bukura.
Wanawe wawili wana Shahada za Uzamili huku watoto wake wengine wakiwa na Digrii za Kwanza katika taaluma mbalimbali.
Bw Mulongo anasimulia jinsi msajili katika taasisi hiyo alifikiri kwamba alienda kufuatilia watoto wake au wajukuu.
“Walidhani nilikuwa natania nilipofanya uamuzi wa kurudi darasani ili kuendeleza masomo yangu,” anakumbuka.
Bw Mulongo huanza siku yake saa kumi asubuhi na kusoma hadi saa kumi na mbili asubuhi anapopumzika ili kuburudika. Anaondoka nyumbani kwenda chuoni dakika 30 baadaye.
Yeye hukaa karibu na taasisi hiyo akiwa na mke wake Helen Masambo. Jambo la kushangaza ni kwamba, licha ya kuwa mwanafunzi mzee zaidi katika taasisi hiyo Bw Mulongo anatangamana kwa uhuru na takriban wanafunzi wote ambao ni wadogo wa umri wake.
Kwa hakika, kizazi cha vijana, ambao wengi wao wana umri wake wanaweza kujifunza mawili matatu.