Makala

Bado ugali kwetu ni ndoto

February 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

LICHA ya serikali kutangaza kwamba bei ya unga wa ugali ilishuka, ukiuzwa kati ya Sh145 hadi Sh170, bado familia nyingi nchini zingali zinabahatisha tu kupata chakula hata angalau mara moja kwa siku.

Leo hii, ugali ambao umekuwa chakula kikuu kwa Wakenya, umekuwa adimu sana kwa familia za kipato cha chini.

Katika mtaa wa Mutego, Dagoretti Kusini, Taifa Leo ilimpata Bi Jackline Mutakalo aliyesema ni vigumu kwa familia yake kula kushiba.

“Nilitarajia bei hiyo iwe Sh100 au chini ya hapo kwa pakiti ya kilo mbili. Nikinunua pakiti moja ya unga nalazimika kugawanya ili kuhakikisha ninatumia mara tatu kwa wiki. Siku ya kwanza kila mmoja huka akashiba lakini siku nyingine zinazofuata inabidi nipike kidogo kila mmoja aonje,” alisimulia Bi Mutakalo.

Lakini pia alisema wiki nyingine, kwa sababu ya mapato yasiyotabirika, hushindwa kununua unga huo.

Kulingana na Bi Mutakalo, ambaye ni mjakazi na hulipwa Sh6,000 kila mwezi, anasema hazitoshelezi mahitaji yake ya kila siku kama vile kula, kulipa kodi na kununua mavazi.

“Kazi yangu ni ya kuenda na kurudi, nachukua Sh2,000 kulipa kodi ya nyumba, Sh,300 za maji kila mwezi, Sh1,500 karo ya watoto wangu wawili, na Sh5,00 kupunguza deni,” akasema.

Bi Jackline Mutakalo akiwa nje ya nyumba yake. PICHA | FRIDAH OKACHI

Pesa zinazosalia, yeye hutumia kununua chakula na wakati mwingi huwa ni unga na mboga.

“Katika bajeti yangu ya chakula, nitanunua pakiti tatu za unga. Unga huo tunatumia siku 12 kila mwezi,” akasema.

Katika mtaa wa Kangemi James Keronzi ambaye ni mhudumu wa bodaboda alisema kuwa japo msimu wa mvua na bei ya pembejeo iliyopunguzwa ilichangia kuwepo kwa mazao mengi, bado bei iliyopo kwenye maduka ya jumla na maduka ya rejareja inamuumiza mwananchi wa kawaida.

“Hayo yote yamefanywa lakini nchi yetu ina wanasiasa ambao ni watu walio na tabia zisizopendeza. Wengi wao wanaangalia masuala ambayo hayatufaidi. Napata riziki yangu kila siku lakini kwenye mfuko wangu sina chochote,” alisema Bw Keronzi.

Serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na Rais William Ruto imekuwa ikijitetea kwamba imeokoa hali kwa sababu akitoka mamlakani, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta aliacha pakiti ya unga wa mahindi ikiuzwa kati ya Sh190 na Sh215.