• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
BAMBIKA: KFCB bado mpo mtaani?

BAMBIKA: KFCB bado mpo mtaani?

Na MWANDISHI WETU

YALE mashairi ya wimbo maarufu Riziki uliotungwa na bendi ya Jamnazi Afrika miaka ya nyuma ghafla yamenishika mguu.

Ubeti wa kwanza huanza kwa mshangao. “Mimi ninalo jambo lanisumbua akili, ulimwengu umepasuka mahali. Mungu alipanga usiku saa ya kulala, mbona walimwengu mumebadili mipango… Usiku sasa imegeuka mchana na mchana sasa ni kama usiku jamani eeh eeeh mi nashangaa…”

Hii ndiyo butwaa niliyonayo kutokana na mwelekeo wa muziki wa kizazi kipya hasa kutoka kwa vipaji chipukizi vilivyoibukia mwanzoni mwa karne hii ya 21.

Tunachokiona kwa sasa kwa tungo zinazoachiwa na idadi kubwa ya wasanii hawa wa hivi majuzi ni mmomonyoko wa kimaadili.

Miziki wanayotunga imevunja nguzo zote za heshima, video za nyimbo hizo ni za kudhalilisha wanawake, ni video chafu usizoweza kutizama na familia, mashairi yenyewe yamesheheni misamiati ya ngono, laana, matumizi ya dawa za kulevya na anasa tupu.

Kinachotia hofu hata zaidi ni kuwa nyimbo hizi zimeishia kuwa maarufu na kuvutia utazamaji mkubwa kweli kweli.

Na licha ya kuwepo na taasisi za kudhibiti maadili ya sanaa nchini, vyombo hivyo husika vimefeli mtihani vibaya sababu hakuna hatua za kimsingi zinazoonekana kuchukuliwa.

Ingalikuwa ni Tanzania, kazi hizi hazingalipata kuona mchana wa jua kutokana na utendakazi wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) ambalo limejitwika jukumu la kudumisha nidhamu na maadili kwenye sanaa ya Bongo.

TAKATAKA (Alvindo)

Baada ya kurekodi audio ya wimbo huo iliyoishia kuwa ‘hit’ kubwa, ilimchukua msanii chipukizi Alvindo miezi kibao kabla ya kutoa video.

Video ya wimbo huo iliachiwa miezi miwili iliyopita na licha ya wimbo kuchujuka kutokana na maudhui yake, umeishia kuvutia zaidi ya ‘views’ laki sita.

Takataka ni wimbo wa machungu alioutunga Alvindo akimwombea mabaya aliyekuwa demu wake baada ya kumwacha kutokana na kuwa maskini.

Ni wimbo uliojaa mashairi ya laana. Bodi ya filamu nchini KFCB ilichukua hatua na kuupiga marufuku kuchezwa kwenye vyombo vya habari nchini huku ikimshurutisha Alvindo kuufanyia ukaratabati.

PIGWA SHOKA (Sheddy Empire)

Wimbo huu ulitoka mara tu baada ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kuuawa na mpenziwe kwa kukatwa na shoka.

Mashairi ya wimbo yanaendekeza mauaji kwa mademu wanaogomea mahusiano.

Maudhui ya mashairi hayo ya kusikitisha yamebebwa kwenye video.

Baada ya wimbo huo kutoka na kuzua utata mkubwa kiasi cha wazalendo kupendekeza wasanii hao wakamatwe, hakuna kikubwa kilichotokea.

KFCB ilisalia kimya. Wasanii hao waliomba msamaha kisha wakafuta wimbo huo kwenye Youtube japo bado unaweza kupatikana kiurahisi.

MATAKO (G-ROCK)

Ni wimbo uliotungwa na wasanii chipukizi The Boy Bleezy pamoja na mwenzake Madra ambao kwa pamoja wanaunda kundi la G-Rock.

Ashakum si matusi, huu ni wimbo usio na la tija wala heshima, maudhui yake yakiwa ni kusifia tu makalio ya mwanamke.

Video ni chafu kutizama; watoto kwa wazazi. Cha kusikitisha hata zaidi ni kuwa una zaidi ya ‘views’ 880,000, ishara tosha ya namna ulivyovutia utizamaji mkubwa.

GET A TAKO (Dmore, Addi Chokoch, Shangwah, Bofa, Shangwah)

Ni wimbo mwingine uliobeba maudhui sawia na ule wa Matako. Mashairi ni ya kusifia ngono za kiholela na udhalilishaji wa wanawake. Video ina ‘views’ zaidi ya laki tatu.

NA IWAKE, THUTHA (Ochungulo Family)

Ni kibao kingine kilichokiuka maadili ila kimevutia ushabiki kweli kweli. Thutha kinachosifia makalio ya mwanamke kina zaidi ya ‘views’ 490,000 huku kile cha Na Iwake kinachosifia uvutaji bangi na matumizi mengine ya dawa za kulevya, kikiwa na ‘views’ zaidi ya 998,000.

Video za nyimbo zote hizo ni za kichokozi, mashairi ya matusi, kuendekeza ngono na kusifia anasa.

WAMLAMBEZ (Sailors)

Ni lugha ya kitaani yenye maana fiche yakiwa ni maelezo ya kushiriki ngono. Video ya wimbo huu ina zaidi ya ‘views’ milioni 1.2. Mashairi yake ni machafu na ya kuwadhalilisha wanawake ikiwachora kama chombo cha ngono. Cha kuvunja moyo ni kuwa waliohusishwa kwenye video kama ‘video vixens’ ni mabinti wadogo na wanaoonekana wakitikisa makalio na kuchochea mihemko ya mahaba.

KAMENISHIKA (Zero Sufuri)

Hapa nchini uvutaji bangi iwe hadharani au mafichoni ni hatia kutokana na sheria kuharamisha starehe hiyo.

Ila kwenye video hii, wahusika na msanii mwenyewe wanaonekana wakivuta bangi, wakiitaja, wakiisifia bila ya woga. Hamna hatua zilizochukuliwa na taasisi yoyote ikiwemo KFCB.

Video japo ya kawaida sana licha ya mdundo mzuri, imevutia zaidi ya ‘views’ milioni moja.

POMBE BANGI (Washukiwa)

Ni kati ya nyimbo za kwanza chafu chafu kutoka. Kwenye video hii iliyozua utata mkubwa ‘video vixens’ wanaonekana wakiwa nusu uchi, kila aina ya dawa za kulevya zikitumika hasa bangi na pombe na pia kuwepo sehemu za ngono.

LAMBA LOLO, PANDANA, FIGA (Ethic)

Lamba Lolo ndicho kibao kiliwapa wasanii hawa umaarufu na kuwatambulisha kwenye gemu walipoachia wimbo huo mwaka 2018. Kiundani, lamba lolo ni shughuli chafu za ngono chumbani. Ndio maudhui katika nyimbo zote hizo; ngono tu.

Video za kazi hizo ni za kichokozi na hata zaidi zina zaidi ya ‘views’ milioni.

KFCB wametulia wala hawashughuliki.

You can share this post!

AFYA: Faida za mananasi katika mwili wa binadamu

JANDONI: Uganda katika mizani raundi ya 16-bora ikianza

adminleo