• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Askofu Yohana: Ukipata mke mcha Mungu, umepata mgodi wa dhahabu

Askofu Yohana: Ukipata mke mcha Mungu, umepata mgodi wa dhahabu

NA MWANGI MUIRURI

ASKOFU Danson Gichuhi almaarufu Yohana ambaye amegonga vichwa vya vyombo vya habari kwa kutoa mapepo kutoka kwa waumini wake wa kike kwa njia tata, amesema wanawake ni viumbe spesheli.

Huku ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake mnamo Ijumaa, Askofu Yohana alisema “wote ambao hutesa wanawake watapata adhabu ya Mungu”.

Akihojiwa na Taifa Leo mjini Murang’a, Askofu Yohana, alisema kwamba “wanawake ndio shamba la ulimwengu”.

Alifafanua msingi wa kutumia dhana ya shamba ni kutokana na ukweli kwamba mama hubeba ujauzito kwa miezi tisa na kuzaa mtoto akishakuwa tayari, hivyo basi kuihakikishia jamii kizazi cha kesho.

Yohana ambaye amekuwa kwa huduma ya maswala ya kiroho kwa miaka 30 alisema amekuwa na waumini ambao asilimia 70 ni wa jinsia ya kike.

“Wanawake ndio watiifu zaidi na wanaopenda sana kazi ya Mungu,” akafichua.

Alisema huwapa wanawake nafasi kubwa sana katika kazi yake ya kuendeleza Neno.

“Ninaweza nikaacha yote ambayo yako mbele yangu ikiwa mshirika wangu wa kike atanipigia simu katika hali ya dharura ili nikamwokolee hali,” akasema.

Alisema kwamba daima wanawake wanafaa kukumbatiwa kama joto la ulimwengu ambalo hufanya maisha ya mwanamume kuwa matamu.

“Hebu wazia dunia ambayo haina wanawake uniambie ingekuwa aje! Kanisani, wanawake huamini sana kuhusu maandiko na matakwa ya kuvumisha Injili. Ni watiifu kanisani na hujitolea kwa hali na mali kuhusu masilahi ya injili na wachungaji,” akasema.

Alitaja kwamba katika Biblia, wanawake ndio walionekana wakijali sana mwili wa Yesu Kristo na waliuosha na kuupaka manukato na kisha kufuatilia sana safari ya kufufuka kwake.

Askofu Danson Gichuhi almaarufu Yohana. PICHA | MWANGI MUIRURI

Aidha, alisema kwamba Kanisa haliwezi likasimama ikiwa halina ushirika wa wanawake jinsi tu ambavyo boma ambalo halina wanawake halistawi ipasavyo.

Aliwapa ushauri wanaume kwamba “mwanamke anafaa tu kusikilizwa, kuenziwa, kutulizwa na kupendwa”.

“Wanaume wanaolalama kwamba mabibi wao ni wakatili, wajue kwamba siri ni kuwaonyesha tu mapenzi na kuwatunza na bila shaka watabadilika mkose kuamini,” akashauri.

Akikiri kwamba wanawake huwa na presha kwa wanaume hasa kuhusu pesa, Askofu Yohana alisema kwamba “nao wakipata hizo pesa huwa wanajenga boma lako bora kukuliko wewe mwanamume”.

“Ukikutana na mwanamke ambaye humuogopa Mungu, si mlevi na ana bidi, utakuwa umepata mgodi wa dhahabu nyumbani kwako,” akaeleza.

Alidai mwanamke ukimpa Sh1,000 anaweza akazalisha zikafika Sh1 milioni huku kiasi sawa mikononi mwa mwanaume mara nyingi kikichunwa na ulevi wa saa au dakika chache.

Askofu huyo alisema kwamba atazidi kuvumisha injili ya Mungu katika upana akapowezeshwa na Muumba na katika safari hiyo, atazidi kuwathamini wanawake na atafanya juu chini kuwahudumia kwa amri za maandiko matakatifu.

“Licha ya kuwa ninakemewa na wengi walioniona katika mkanda wa video nikipunga pepo kutoka kwa muumini wa kike, sina majuto na kazi ya Mungu itaendelea. Ukinihukumu hapo kwa mujibu wa busara yako, kwa Mungu ninajua nitavuna faida kwa kuwa kusaidia wengi kuhepa mapepo,” akasema.

Kanisa lake ni Christian Committed Gospel Church na lina matawi Nakuru, Murang’a, na Kirinyaga.

Kando na masuala ya kiroho, Yohana ni shabiki wa klabu ya Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Walinzi wawili waumizwa na wezi wa mananasi ya Del Monte

Embarambamba akubali kurudi kwa laini

T L