Bambika

Baada ya msoto, Colonel Moustapha atamani kurudi soko, anamisi kuwa na demu

April 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na SINDA MATIKO

COLONEL Moustapha amechoka. Rapa huyo aliyetrendi mwaka jana baada ya kuonekana akifanya kazi za mjengo, anasema amechoshwa na upweke na sasa anatamani kumpata mpenzi wa kuanzisha familia na yeye.

“Nimekuwa mpweke kwa muda mrefu sana, sikuwa sawa kisaikolojia, singeweza hata kuwa na mpenzi maana sikuwa hata na hisia hizo. Lakini kwa sasa baada ya mama kupata nafuu, nahisi ni muda wa kujijali vile vile. Nataka kuwatengenezea tena watu muziki mzuri, lakini pia nataka kuanzisha familia maana sina familia bado. Awali nimekuwa kwenye mahusiano na mademu wakanizengua ila naamini nitampata wangu,” anasema Colonel.

Moustapha aliyewahi kuwa staa mkubwa wa burudani miaka ya 2000, anasema hajaweza kuwa na mwanamke kwa zaidi ya miaka minne sasa baada ya kufilisika  kiasi cha kumfanya kuuza mali zake zote ikiwemo gari lake na mwishowe kuishia kujipata akifanya vibarua vya mjengo kujipatia riziki.

Moustapha analaumu kufilisika kwake kwa matumizi mabaya ya pesa zake lakini pia ugonjwa wa kansa uliomkuta mamake.

“Nilipokuwa staa mkubwa, enzi zile za hiti yangu ya ‘Kinyaunyau’ nilikuwa natumia hadi Sh2,000 kwa siku kula vyakula aina aina kama ma-burger na machipsi vile. Nilipofilisika nilikuwa natumia Sh150 kwa siku,” anakiri Moustapha.

Hali hiyo ya uchochole ndio ilimfanya kukaa mbali na mademu kwani hangeweza kumudu gharama zao.

Lakini hata zaidi, mamake alipopatikana kuwa na kansa aina ya lymphoma mambo yakawa mabaya hata zaidi. Kugharamia matibabu ya mamake haikuwa jambo rahisi  kitu ambacho kilimsukuma kuuza kila kitu alichonacho.

Na alipokosa alijipata akiwa mwanavibarua.

Moustapha alijikuta akitrendi mwaka jana  baada ya mmoja wa wapita njia kumwona akibeba zege na kokoto kwenye eneo la mjengo na kisha kumpiga picha iliyoishia mitandaoni.

Kilichofuata ni Wakenya kujitokeza kwa wingi na kumchangia zaidi ya shilingi milioni moja.

“Sitachoka kuwashukuru sana Wakenya kwa sapoti walionionyesha. Wengi ni wale nilianza kuwaburudisha wakiwa wachanga, sasa hivi wamekuwa watu wazima,” anasema Moustapha.

Kwenye matumizi ya fedha hizo anasema asilimia kubwa ilienda kwenye kugharamia matibabu ya mamake.

“Mama alikuwa anaumwa kansa la lymphoma ambao ni uvimbe uliokuwa umemea kwenye figo yake ya kushoto. Ulikuwa uvimbe mkubwa wa kama sentimita 10, basi ulianza kukatwa na sasa umesalia kama asilimia 2.5% tu. Kwa sasa mama yupo afadhali.”

Kupata unafuu kwa mamake ndio sasa kumempa fursa Moustapha kutamani kurudi kwenye mapenzi tena.