Bambika

Burudani: Waliovuma zama zao kuteseka hadi lini?

January 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

WASANII wengi waliovuma katika enzi zao nchini, sasa wanaishi katika hali ya upweke na mahangaiko, hali ambayo imeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wao.

Wengi wao kwa sasa wako kwenye miaka ya uzeeni, huku michango yao kwenye sanaa ikibaki kuwa kumbukumbu zinazowachangamsha Wakenya wengi hadi sasa.

Baadhi yao ni wanamuziki, waigizaji, wacheshi kati ya fani nyingine.

Kile kimeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wao, ni mtindo ambao umeibuka katika siku za hivi karibuni, ambapo baadhi yao wamekuwa wakifanyiwa michango kuwasaidia kugharimia matibabu yao au hata kujiendeleza kimaisha.

Ni mtindo ambao umeibua maswali kuhusu ikiwa waliwekeza vizuri fedha walizopata kutokana na sanaa, au sanaa ziliwalipa vizuri kuwawezesha kuwekeza kwenye miradi ambayo baadaye ingewasaidia nyakati za uzeeni. Cha kufadhaisha ni kuwa, baadhi yao wamefariki wakiwa katika hali hizo za kusikitisha.

Baadhi ya wasanii ambao wamejipata katika hali hiyo ni mwanamuziki Dick Munyonyi (Firirinda-aliyefariki Jumamosi), Karanja David (wote kutoka ukanda wa Mlima Kenya), mwigizaji Bwire Ndubi, mwanamuziki Sukuma bin Ongaro (Magharibi), Fadhili William, wacheshi David Wanjau (marehemu Mzee Ojwang), Othuol Othuol kati ya wengine.

Kabla ya kifo chake mnamo Jumamosi, mwanamuziki Dick Munyonyi alikuwa amesaidiwa kurejea kwenye fani ya muziki kwa muda wa miaka miwili, tangu 2021, na wanamuziki maarufu katika eneo la Kati.

Kabla ya kusaidiwa kurejea katika fani hiyo, mwanamuziki huyo mkongwe alikuwa ametoweka kwa karibu miaka 20, baada ya kuzongwa na changamoto za kimaisha.

Hata hivyo, wimbo wake ‘Firirinda’ (Kusherehekea), uliotungwa katika miaka ya themanini, ulifufuka kimiujiza kwenye mitandao ya kijamii, na kusambaa kote kote.

Kuufufuka kighafla kwa wimbo huo ndiko kulimwezesha kupata usaidizi wa wanamuziki na wanasiasa maarufu kutoka Mlima Kenya kurejea katika fani hiyo.

Mwanamuziki mkongwe Karanja David, aliyevuma katika miaka ya 1990 Mlima Kenya, pia amejipata katika hali iyo hiyo.

Mnamo 2021, alirejea katika fani ya muziki kimiujiza, baada ya masaibu yake kuangaziwa na kituo kimoja cha habari.

Kulikuwa na mchango mkubwa wa fedha uliofanywa kumsaidia, jaoo madai yameibuka kuwa pesa hizo zilifujwa na baadhi ya watu waliokuwa wakisimamia ukusanyaji wake.

Kwa sasa, bado yuko kwenye jangwa la kimaisha, ijapokuwa aliiambia Taifa Jumapili ameanza kupata matumaini, baada ya mtu mmoja kujitokeza na kumpa kipande cha ardhi katika eneo la Subukia, Nakuru, kujenga nyumba yake.

Kwa mashabiki wa uigizaji, masaibu ya mwigizaji Bwire Ndubi ni ya kusikitisha.

Mumewe mwigizaji huyo, Bw Dan Sonko, alikiri majuzi kwamba walilazimika kutalikiana baada ya Bi Bwire kupatikana na saratani ya matiti.

“Mimi ndiye niliyemwacha mke wangu kwanza. Baadaye, tulikubaliana tuachane. Lengo kuu ni kumpa kila mmoja nafasi kujiendeleza kimaisha kwa njia huru na ya amani,” akasema Bw Sonko, kwenye mahojiano.

Kwa wacheshi Mzee Ojwang’ na Othuol Othuol, iliwalazimu wacheshi wengine nchini kuungana ili kufanya michango ya kuwaandalia mazishi yao kwani walikuwa wakipitia hali ngumu kimaisha kabla ya kukumbana na mauti.

Kutokana na mwelekeo huo, mtaalamu na msomi wa masuala ya burudani, Dkt Maina wa Mutonya, anasema kwamba ijapokuwa ni jukumu la msanii kuwekeza fedha anazopata ili kumsaidia katika siku za usoni, kuna haja serikali kubuni mfumo thabiti wa kuwasaidia wasanii wakati wanapolemewa kimaisha.

Anawataja wasanii kama watu wa kipekee sana, ambao hudumisha historia na tamaduni za nchi, kupitia tungo zao—iwe ni nyimbo, ucheshi au hata uigizaji.

“Ni kweli kuwa usanii ni sawa na kazi nyingine yoyote, hivyo msanii anafaa kujiwekea akiba kama wafanyakazi wale wengine. Hata hivyo, lazima serikali na wadau husika kuweka mifumo thabiti kuhakikisha kuwa wasanii wanasaidiwa wanapolemewa maishani,” akasema Dkt Mutonya kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.

Anasema kuwa kuna umuhimu Kenya iyaige mataifa ya Magharibi kama vile Amerika na Uingereza, ambako kando na uwepo wa sera thabiti wa kuwasaidia wasanii kifedha uzeeni wao, kuna makavazi maalum yanayojengwa kuhifadhi tungo zao.