Charlene Ruto atangaza shindano la mshindi kuchomoka na Sh100,000
BINTI wa Rais William Ruto, Charlene Ruto, amezindua shindano la ubunifu kwa kushirikisha vijana walio na ujuzi wa kuunda nembo za kidijitali.
Kwenye ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Charlene ametaka vijana wa umri wa miaka 18 hadi 30 kutuma nembo kwa kuzingatia sheria na masharti akiahidi kwamba mshindi atatuzwa Sh100,000 na kupata fursa ya kushiriki naye katika dhifa ya chakula cha mchana.
Alitoa tangazo hilo mnamo Jumanne.
“Mtandao wa Vijana wa Kimataifa (TYPNI) unatafuta nembo. Shindano hili linatoa fursa kwa wabunifu chipukizi kuonyesha vipaji vyao na kuchangia utambulisho mahiri wa TYPNI,” akaandika Charlene.
Nafasi hiyo itatumiwa na vijana kuonyesha ujuzi kwenye taaluma ya ubunifu.
Baadhi ya wachangiaji maoni mtandaoni wamesifia shindano hilo, wakimtaja Charlene kuwa ni kielelezo cha vijana walio katika mstari wa mbele kuwasaidia vijana wenzao.
El Passo alimpongeza kwa hatua hiyo.
“Hatua nzuri sana. Wewe ni kielelezo kwa kizazi chetu,” akasema El Passo.
Mary Thuku naye alitaka binti huyo wa kiongozi wa nchi kuongeza umri wa vijana kwenye shindano hilo.
“Asante kwa nafasi hii. Lakini kwetu tuliozidi umri? Naomba uweke umri wa kutoka miaka 18 hadi 35,” akaomba Bi Thuku.