• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Dorcas Rigathi ampamba DP Gachagua kwa maneno matamu

Dorcas Rigathi ampamba DP Gachagua kwa maneno matamu

NA FRIDAH OKACHI

MKE wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Bi Dorcas Rigathi, amempamba mume wake kwa maneno matamu akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Bw Gachagua kwa sasa amefikisha umri wa miaka 59.

Bi Rigathi alimtaja kiongozi huyo kuwa ni mtu wa kawaida na msema ukweli ambaye walikutana mwaka wa 1987 akiwa katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU).

Mchungaji huyo alisema mumewe amekuwa nguzo katika familia yake.

“Kuwa na siku ya kuzaliwa yenye furaha mwanamume wangu wa upekee wa aina yake, mume, mwandamani na rafiki. Wewe ni nguzo kwa familia yetu. Unachukua kila kitu kwa hatua inayotakiwa na ni mkweli kupindukia,” akaandika Bi Rigathi.

Aliongeza kuwa yeye na wana wao wawili, wanajionea fahari kubwa kuwa naye maishani mwao.

“Kevin, Keith na mimi tunasherehekea zawadi nzuri ya maisha yako. Wewe ni baba na mume bora. Bwana akupe kibali, maisha marefu na baraka tele. Na atimize kila hitaji la moyo wako. Kwa upendo wangu wote, Dorcas,” akampamba.

Aliongeza kuwa Naibu Rais kila mara huwajali watu na hufanya kazi bila kuchoka ili kutimiza ahadi za serikali kwa Wakenya.

Naibu Rais Rigathi Gachagua akiwa na mkewe, Bi Dorcas Rigathi (kushoto) katika hafla ya awali. PICHA | MAKTABA

Shabiki mmoja katika ukurasa wa Facebook anayefahamika kama A-Diplomat Omarai Jeff, alimsifia Bi Rigaathi kwa ‘kubadilisha’ mumewe kupitia maombi.

“…Dorcas, nafikiri umefanya kazi muhimu kwa kubadilisha moyo wake kupitia maombi. Wewe ni kielelezo chema kwa wanawake ambao huombea waume wao badala ya kuwaweka vitani,” akachangia A-Diplomat Omaria Jeff.

Naye Bernard Birundi alishangaa mbona baadhi ya wanawake huwaficha waume wao katika siku muhimu kama hii.

“Wewe ni mfano wa mke mwema. Wengine wanaficha mabwana zao kwa gunia hata kwa siku muhimu maishani mwao,” akasema Birundi.

  • Tags

You can share this post!

Pasta Ezekiel alivyomtetemesha mwenzake Benny Hinn kwa...

KAULI YA WALLAH: Harakati za kila mwanadamu ni kutafuta...

T L