Bambika

Filamu ya Bobi Wine yapata uteuzi Oscars

January 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

FILAMU iliyotayarishwa na mwanasiasa Robert Kyagulanyi almaarufu ‘Bobi Wine’ ambaye pia ni staa mkubwa wa muziki nchini Uganda, imeteuliwa kwa tuzo za Oscar, nchini Amerika.

Filamu hiyo inaitwa ‘The People’s President’ yaani Rais wa Watu.

Bobi Wine alipokea habari hizo kwa furaha.

Mkewe, Barbie Kyagulanyi aliwahi kusimulia jinsi ambavyo hata hawakuwa na mtazamo sawa kimaisha maana aliishi kumshangaa Bobi Wine na maisha yake ya mabandani.

Kadri siku zilivyosonga ndivyo kani zilizowaleta pamoja zilivyozidi kupata nguvu.

“Mwanzoni nilikuwa mtu ‘simple’ ambaye ndoto yake ilikuwa ni kumiliki tu gari na nyumba ndogo maana tayari nilishazoea maisha katika mitaa ya mabanda,” aliwahi kusimulia.

Tuzo hizo huwa kubwa na maarufu zaidi katika tasnia ya utengenezaji senema duniani.

Mnamo Jumanne, mwanasiasa huyo alieleza furaha yake kutokana na uteuzi huo, kwenye ujumbe alioandika katika mtandao wa X (zamani Twitter).

“Habari za kufurahisha: Sinema yetu #BobiWineRaisWaWatu… imepata uteuzi kama Filamu Bora kwenye Tuzo za Oscar,” akasema mwanasiasa huyo.

Filamu hiyo inapigania demokrasia na utawala bora na vilevile kuhimiza raia kuongeza nguvu kwa juhudi zao za kuukabili utawala wowote wa kidhalimu.

Akaongeza: “Ni fahari kubwa kuona filamu inayoelezea hali ilivyo Uganda ikipata uteuzi kwenye Tuzo za Oscar. Harakati za kupigania demokrasia nchini Uganda na duniani kote bado zinaendelea. Ahsante sana kwa uteuzi huo.”

Filamu nyingine zilizopata shavu pamoja na hiyo ya Bobi Wine ni ‘The Eternal Memory’, ‘Four Daughters’, ‘To Kill a Tiger’ kisha ’20 Days in Mariupol’ kwenye kategoria ya Makala Bora ya Simulizi, kategoria ya Filamu.

Uteuzi huo unajiri siku chache baada ya mwanasiasa na mwanamuziki huyo kuwashinikiza wakazi wa jiji la Kampala kuandamana kulalamikia barabara mbovu.

“Polisi na jeshi limezunguka makazi yangu na kutuweka chini ya kizuizi cha nyumbani. Hata hivyo, maandamano yataendelea. Tutengenezee barabara zetu! Waachilie wafungwa wa kisiasa! Wape raia wa Uganda uhuru wao!” akasema Bobi Wine kwenye mtandao wa X.

Kiongozi mwingine wa upinzani nchini humo, Kizza Besigye, pia alitoa picha za polisi wakiwa wamezunguka makazi yake, akisema: “Makazi yangu yamezungukwa na waoga! Hatutarejea nyuma, tunahitaji huduma bora.”

Wawili hao wamekuwa wakiongoza kampeni kali dhidi ya utawala wa Rais Yoweri Museveni.