Gwiji wa utangazaji Joyce Gituro asimulia changamoto za ndoa
NA WANDERI KAMAU
GWIJI wa utangazaji Joyce wa Gituro ameeleza jinsi ndoa yake ilivyokumbwa na changamoto nyingi na sababu zilizomfanya kutengana na mume wake.
Mtangazaji huyo alieleza kuwa alijaribu kuvumilia masaibu waliyokuwa wakipitia, ingawa mwishowe alishindwa na akaamua kumwondokea mumewe.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Alhamisi, wa Gituro pia alidai alijaribu kuingizwa kwenye dini ya giza lakini “nikanusurika kwa neema ya Mungu”.
Baadhi ya vituo vya redio ambavyo mtangazaji huyo ashawahi kufanyia kazi ni Radio Citizen, Milele FM, na Radio Jambo.
“Kwenye kanisa hilo, pasta alikuwa akitoa ‘tabiri’ za ajabu kunihusu. Alikuwa akieleza jinsi alivyoonyeshwa masaibu ambayo yangenikumba baadaye. Kwa wakati mmoja, alitabiri kwamba ningepata ajali na mtoto wangu. Tabiri hizo zilianza kunitia wasiwasi. Nilimuuliza mume wangu kuhusu kanisa hilo,” akasema Bi Gituro.
“Nilijitoa pamoja na watoto wangu baada ya kushiriki kwa muda wa miezi miwili,” akaongeza.
Akaongeza: “Baada ya kuendelea kumuuliza maswali ya ndani zaidi kuhusu kanisa hilo, alianza kutoroka nyumbani. Angetoroka nyakati za jioni kwenda ‘maombi’ katika kanisa hilo na kurejea asubuhi. Nilijaribu niwezavyo. Niliita hadi wazazi wake ili kujaribu kumwokoa na kuondoka katika kanisa hilo, ila juhudi hizo zote hazikuzaa matunda.”
Bi Gituro alisema anaamini Mungu ndiye alikuwa amemtuma katika kanisa hilo ili kuona hali halisi ilivyokuwa.
Anasema kuwa hajui hatima yake ingekuwa vipi ikiwa hangekubali wito wa kuenda na kuona hali ilivyokuwa.
Alisema Wakenya wanafaa kuwa waangalifu kuhusu aina ya makanisa wanayoshiriki, kwani baadhi yao ni dini za giza ambazo lengo lake ni kuwapotosha na kuwahangaisha.
“Kumekuwa na visa vingi vya watu wanaopofushwa na dini zao. Wito wangu kwao ni wafunguke macho ili kutoingizwa kwenye giza ambalo hawawezi kujitoa,” akasema.