‘Hatuna tamaa sana, wanaume wa Kenya ndio mkono gamu’
FRIDAH OKACHI Na WANDERI KAMAU
BAADHI ya wanafunzi wa kike katika vyuo vikuu na wanawake wanaotafuta wachumba jijini Nairobi, wanaomba wanaumme Wakenya kuwa wepesi wa kutoa pesa ili kuepuka kudhulumiwa na wanaumme kutoka mataifa ya nje.
*Lizzie ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kikuu, anafedheheshwa na jinsi wanaume nchini huwa na mkono gamu. Hali hiyo ikisababisha wanafunzi wengi wa kike kutafuta wachumba kutoka mataifa ya nje.
“Si kwamba wanaume Wakenya si wazuri? La hasha, hawa wengine tunaoishi nao kwenye mitaa wanatoboka zaidi kwa kutumwagia pesa. Nikienda kwenye kilabu kidume ananipa zaidi ya Sh10,000 lakini Mkenya kama amejaribu sana ni Sh2,000,” akafunguka *Lizzie.
*Lizzie ambaye anaishi Kajiado aliwasifia wanaume kutoka Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambao alisema wamejaa mtaani humo.
Mita chache kutoka kwake *Lizzie, kunaye *Christine ambaye pia amekuwa akiwakwepa wanaume Wakenya kwa kutuma nauli ya Sh800. Aliambia Taifa Leo, binafsi, hawezi kuendeleza mahusiano aliyotaja ni unyanyasaji.
“Tuwe wakweli… umenitumia Sh500 nikutane nawe, kisha nikifika kwako hutanipa za kurudi nyumbani kwangu. Iwapo unatuma kiasi hicho, nitaelekeza kwa shughuli nyingine na mkutano huo hautakuwepo,” akasema *Christine.
Katika mtaa wa Kileleshwa, jumba la Marsabit Plaza, eneo la burudani, mmoja wa wafanyikazi aliambia Taifa Leo, idadi ya juu ya wateja wao ni wanaumme ambao si Wakenya.
“Asilimia kubwa ni wateja kutoka mataifa mengine ambao huja hapa na wanawake Wakenya. Pia, wateja hao hufika mapema. Ukija hapa baada ya saa tano usiku utakosa nafasi,” alisema mfanyikazi huyo.
Mnamo Jumanne kwenye mtandao wa Facebook, hisia mseto zilitolewa na wanamitandao baada ya jamaa mmoja kuomba usaidizi wa kurejeshewa pesa alizotumia mwanamke aliyemuangusha kwa kukosa kufika eneo la miadi.
Kwenye chapisho hilo, mwanamume huyo alishambuliwa kuwa hicho ni kiasi kidogo cha pesa.
Mwanasaikolojia Kennedy Kibbet anasema mahusiano ambayo huchochewa na pesa kwa asilimia kubwa hayadumu. Alisema wengi wa wapenzi hao huishi kwa sababu kuna pesa na iwapo pesa zitaisha, uhusiano unavunjika.
“Watu wengine huchagua pesa badala ya upendo, na hiyo ni tamaa bali si mapenzi,” alisema Kibbet.
Kumekuwa na visa kadhaa vya watu kuwaua wapenzi wao katika baa na vilabu kwa sababu ya kuweka mbele tamaa ya kuvuna mali badala ya kupalilia mapenzi.
Mbinu za kuepuka mauaji ya kinyama katika dunia iliyojaa maovu
Wataalamu wanasema kuwa kuna sababu kadhaa zinazoweza kuchukuliwa na wadau wote katika jamii, kuzuia wimbi la maovu na mauaji ambayo yamekuwa yakishuhudiwa katika siku za hivi karibuni.
Wanasema kwamba tahadhari hizo zinafaa kuchukuliwa na wadau wote katika jamii ili kuhakikisha kuwa kuna suluhu la kudumu.
Kulingana wakili James Kahihia, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kiusalama, serikali inafaa kuimarisha ukaguzi wa raia wa kigeni wanaoingia nchini, ili kuhakikisha ina rekodi na maelezo muhimu ya watu walio nchini.
“Ukitathmini maovu mengi ambayo yamekuwa yakihusishwa na raia wa kigeni, imekuwa vigumu sana kuwanasa wale wanaohusika. Hivyo, serikali inafaa kuimarisha ukaguzi wao, kupitia Idara ya Uhamiaji,” akasema Bw Kahihia.
Mbinu nyingine inayopendekezwa ni wazazi kuhakikisha wamewalea wanao kwa miongozo mizuri ya kidini.
Wanasema kuwa kwa kufanya hivyo, itakuwa vigumu kwa wanao kupotoshwa na watu wasiowajua kujiingiza kwenye uhalifu kama vile ukahaba.
Kulingana na Dkt Margaret Mwihaki, ambaye ni mwanasaikolojia, ni vigumu sana kwa vijana waliolelewa vizuri kujipata kwenye vishawishi vya kushiriki maovu.
“Mara nyingi, watu wakubwa bado huwa wanakumbuka misingi ya mafundisho ya kimaadili kama walivyofundishwa hata wakiwa watoto. Hivyo, kwa kupalilia maadili mema, huenda tukakiokoa kizazi hiki,” asema Dkt Mwihaki.
Anasema pia wazazi wanafaa kufuatilia jinsi wanao wanavyotumia mitandao ya intaneti.
Anasema kuwa mitandao mingi inatumika kueneza maovu, ambapo henda ikawa hatari, ikiwa wazazi na walezi hawatakuwa makini kuhusu jinsi wanao wanavyotumia mitandao ya intaneti kama vile rununu au vipakatalishi.
“Kwa sasa, mtu anaweza kupata jambo lolote analotaka kwenye mtandao wa intaneti kwa rahisi sana. Hivyo, ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanafuatilia kwa kina wavuti ama taarifa wanazotumia wana wao,” akasema Dkt Mwihaki.
Tahadhari nyingine anazopendekeza ni wazazi kuhakikisha wanawapa wanao fedha za kutosha wanapokuwa shuleni, ili kuwazuia kuanguka kwenye vishawishi vya kufanya maovu ili kupata fedha za kujikimu.