• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Huyu Joy Kendi atakupa siri ya kuwa ‘influensa’

Huyu Joy Kendi atakupa siri ya kuwa ‘influensa’

NA SINDA MATIKO

JOY Kendi ni miongoni mwa mafashonista wanaotetemesga hapa nchini. Lakini pia ni mtalii wa ndani na nje ya nchi.

Kutokana na mishemishe zake hizi, Kendi kaishia kuwa miongoni mwa watengenezaji maudhui wakubwa nchini ambao hupata dili za biashara matangazo mara kwa mara kutoka kwa kampuni mbalimbali tajika. Juzi kati, Kipwani tulikaa naye kikao.

Ulijitambulisha kwenye tasnia ya showbiz kama mwigizaji, kisha ukasita kabisa?

Ni kweli Wakenya wengi walipata kunifahamu kupitia kile kipindi cha Changing Times. Ila baadaye nilishindwa kuamini uwezo wangu wa kuigiza. Dukuduku hiyo ndio ikawa chanzo cha mimi kuachana kabisa na masuala ya uigizaji. Niliitiwa fursa nyingi tu za kuigiza ila nikazikataa bila hata ya kuwaza mara mbili. Nilihisi ni bora nikimbizane na kile nilichohisi nina imani nacho zaidi.

Ndio ukageukia fasheni?

Fasheni ni kitu ambacho toka utotoni nilikipenda. Nilianza kupenda kubuni aina ya mavazi nikiwa na miaka saba tu na ni tabia ambayo ilikuwa ikimkera sana mamangu sababu katika umri huo, nilikuwa napenda sana kuchana chana mavazi ili kujaribu kuunda dizaini fulani.

Ni nini ambacho hukuvutia zaidi na tasnia hii ya fasheni?

Wajua kupitia fasheni, ninaweza nikapata majibu ya kutosha kuhusu mtu fulani ni wa sampuli gani. Unaweza ukajua namna mtu anavyojiamini kwa staili yake ya fasheni, anachopenda na anachofanya wakati huo.

Mapenzi hayo ya fasheni yakaishia kukugeuza mtengenezaji maudhui hatari eti eeh?

(Hahaha) Naona unanitekenya kwa maneno. Aaah! Suala la kuwa Influensa lilinikuta tu. Nafikiri watu walianza kupenda ninachokifanya na kuanza kunifuata kunipa dili za kutangaza bidhaa mbalimbali. Ilitokea tu sababu nilianza kama bloga wa fasheni kama nilivyokueleza hapo awali.

Nilikuwa napenda kuona wanachofanya watu wengine nami nafanya kwa namna yangu kisha naposti. Ikawa mtindo wa kila siku ila upande wangu nilipenda zaidi kuelemisha watu jinsi ya kungára kwa bajeti ndogo.

Hapo ndipo jina likazidi kuwa kubwa. Hapo basi kampuni zikaanza kunifuata ikawa sasa sizungumzii tu fasheni lakini pia bidhaa zingine kama bidhaa za kujipodoa, mashine za upishi, simu kati ya zingine kibao.

Kuna watu wengi wanajaribu sana kila kukicha kuwa influensa, ila hajawa rahisi, unahisi wanakwama wapi?

Watu wengi hufikiri kuwa Influensa ni kuposti tu picha nzuri nzuri ukiwa maeneo tofauti tofauti. Kwa baadhi inalipa hivyo ila kama unataka iwe ajira unayoweza kuitegemea ni lazima ufanye mengi ya ziada ndipo uweze kuwa na uhakika wa kupata cheki kila mwisho wa mwezi.

Kuwa influensa ndio mbinu mpya ya kutangaza biashara. Sisi ndio mabango na sura za bidhaa husika tunazotangaza. Kwa maana hiyo ni lazima ujitengenezee brandi ambayo kampuni hizi zikikutizama zinaona kweli unaendana nazo na hivyo zinakuwa na haja ya kukupa kazi.

Hizi dili unazifuata mwenyewe au zinakufuata wewe?

Mwanzo kabisa mimi huchagua sana aina za brandi ninazo fanya kazi nazo. Huwa sifanyi kazi na brandi yoyote tu eti kwa sababu wana bidhaa na wapo tayari kulipia, hapana.

Huwa nataka kufanya kazi na brandi ambazo nafasi yangu imeridhishwa kabisa na bidhaa zao hivyo inakuwa rahisi sana kwangu kuwasukumia mzigo mitandaoni.

Huwa nina kanuni moja hivi, ikiwa siwezi toa fedha zangu kulipia huduma fulani au bidhaa fulani, mbona niitangaze. Pia kuna baadhi ya kazi za matangazo unaweza ukapata na zikakuharibia michongo mingine kabisa.

Kama zipi hizo?

Kwa mfano siwezi kutangaza hizi kampuni za kubeti sababu sio jambo linalikubalika na jamii. Pia ukiangalia brandi yangu, kutangaza kampuni za kubeti itakuwa ni kujichanganya. Isitoshe mwenyewe siamini kabisa katika kubeti au michezo hii ya pata potea.

Huoni huko ni kama kupoteza fedha?

Kila kitu kina ubaya na uzuri wake. Ndio itaathiri kipato sababu hizi ni pesa ninazokataa ila mwisho wa siku malengo yangu ni kuwa na taaluma ndefu zadi kwenye tasnia hii. Nimejifunza kuishi hivi.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi Bonde la Ufa wauliza Rais atatimiza ahadi lini

Rais wa pili wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi aaga dunia

T L