• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Itumbi asifiwa kwa kusimama na ‘rafikiye’ Jacque Maribe

Itumbi asifiwa kwa kusimama na ‘rafikiye’ Jacque Maribe

NA FRIDAH OKACHI

MSHAURI wa kisiasa katika Serikali ya Kenya Kwanza Dennis Itumbi amechangamsha wanamitandao kwa kupakia barua ndefu kwenye ukurasa wa Facebook, kufurahia uamuzi wa mahakama kumwondelea lawama mwanahabari Jacque Maribe kwenye mauaji ya Monica Kimani.

Wanamitandao wa kike wakiwa na hisia ya kuwa na marafiki wa kiume wenye ushawishi kama ule wa mshauri huyo ambaye aliamini rafikiye hana hatia na miaka sita iliyopita alichukua hatua hata ya kumwakilisha kwenye kesi ya mauaji hayo.

Mercy Arengo sasa anataka kubadilisha orodha ya marafiki wa kiume na kutafuta walio na mfano wa Bw Itumbi.

“Kwenye orodha ya marafiki wa kiume natafuta walio na imani kama ya Dennis Itumbi,” alisema Mercy Arengo.

Tanui Linda alifurahia jinsi mshauri huyo amekuwa rafiki wa ukweli.

“Leo nimekuwa mwenye matamanio ya kuwa na marafiki aina hii, umekuwa rafiki wa kweli kwa Maribe. Ulimwamini kutoka mwanzo, na kumpa msaada wako kwa miaka sita. Wewe ni mtu muhimu maishani mwake!” alichangia Tanui Linda.

Ann Njeri pia alimpongeza.

“Ujumbe mzuri kwa rafiki mpendwa. Nimepata mafunzo mengi kutokana na heshima hii, rafiki wa kweli daima umekuwa ukimpa moyo na alipohitaji rafiki wa kuzungumza naye, ulifanya hivyo hasa. Kwa Jacque Maribe Mungu akuongoze unapoanza ukurasa mpya wa maisha,” alimpongeza Ann Njeri.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook alichapisha ujumbe mrefu akithibitisha tangu tukio hilo kutokea alikuwa na imani mwanahabari Jacque Maribe hakuwa na hatia.

“Imekuwa miaka sita, safari yenye kivuli, ambapo minyororo isiyo ya haki ilitafuta kufunga roho ya rafiki yangu, aliye na utu wa kupendeza, rafiki ninayemthamini sana,” alisema Bw Itumbi.

“Leo, ukweli umefichuka kwa kuliondoa giza… Maandishi yaliyolenga kwenye vyombo vya habari na si kitu kingine chochote,” alipakia Bw Itumbi.

Kwenye barua hiyo ndefu, Bw Itumbi alitangaza kumshikilia mkono hadi kurejesha miaka yake sita iliyopotea wakati wa kesi hiyo.

Muda mchache baada ya kupakia ujumbe huo, picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha akiwa mahakamani huku akimkumbatia.

  • Tags

You can share this post!

Watoto 700,000 wakodolea macho utapiamlo nchini Sudan

Jaji Grace Nzioka aitisha maji mawakili kupoza joto akisoma...

T L