Kanyari: Maisha magumu yalinisukumu kuambia waumini kupanda mbegu ya 310
NA FRIDAH OKACHI
PASTA Victor Kanyari aliyezingirwa na utata nchini, sasa amekiri mpango wake wa kuitisha Sh310 za waumini kupanda mbegu kwa ajili ya maombi na uponyaji katika siku za nyuma, ulikuwa ni mojawapo ya njia za kujikwamua kutoka kwa umaskini.
Pasta Kanyari ambaye amekuwa akitoa huduma za kuhubiri kwa takribani miaka ishirini sasa, wakati wa ibada ya hivi majuzi katika kanisa lake la Salvation Healing Ministry, alifichua mbinu hiyo ya kupanda mbegu ilikuwa ni njia ya kujinasua kwenye umaskini ulikuwa umemsukuma.
Pasta Kanyari mwenye radhi na kudai haikuwa nia yake kuwashawishi wafuasi wake kutoa pesa hizo.
“Si kutaka kwangu. Umaskini ulikuwa umenitandika sawasawa lakini nilikuwa na upako. Ni umaskini…,” alisema pasta Kanyari.
“Nilianza kuitisha 310 rafiki yangu, lakini niliuliza Mungu anipatie akili na maarifa. Pesa nitajitafutia. Mungu alinipa upako, lakini haikuwa upako wa pesa. Ilikuwa upako wa kuponya magonjwa kama vile HIV… Watu walikuwa wanajaa, watu kama 10,000. Lakini zile pesa nilikuwa napata zilikuwa kidogo na hazikunitosha. Nikaanza kuitisha mbegu ya 310… nasema panda mbegu na watu wanatuma,” akaongeza.
Mhubiri huyo alisema Mwenyezi Mungu alimuelekeza kutoka katika njia hiyo ya kutafuta pesa zisizo za ukweli na kurejea kwa njia yake halisi.
“Nilikuwa naitisha Sh310, watu wanapona. Lakini naenda kwa nyumba, nalala njaa. Sikuwa na chakula. Na nimekuwa nafanya miujiza!” alishangaa pasta Kanyari.
Baadaye alisema alimuomba Mungu ampe ufunuo na kutaka kupata hekima na jinsi ambavyo angepata pesa kwa njia ya haki, jambo alilosema Mungu kufanikisha.
“Mungu hakuwahi kufunga hii huduma tena. Sikukosa pesa tena. Sasa niko na magari hata nakosa pa kuyapeleka. Watoto wanasoma vizuri…,” alikamilisha ushuhuda wake.
Utata huo wa kupanda mbegu ya Sh310 ulifanya aliyekuwa mke wake na pia mwanamuziki wa Injili Betty Bayo kutengana naye.