KFCB yalegeza msimamo dhidi ya watengenezaji maudhui YouTube
NA FRIDAH OKACHI
MWENYEKITI wa Bodi ya Uainishaji Filamu nchini (KFCB) Bw Njogu wa Njoroge ameamuru kuondolewa kwa ilani iliyotumwa kwa watengenezaji wa maudhui ya YouTube iliyowaelekeza kulipia leseni kabla ya kupakia kazi zao katika akaunti zao kwa jukwaa hilo.
Bw Njoroge alibatilisha agizo tata lililokuwa limetolewa na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KFCB Bw Paskal Opiyo, akiwaelekeza waundaji maudhui nchini ambao ni Abel Mutua, Njugush, Jacky Vike, Terence Creative, Oga Obinna miongoni mwa wengine kulipia leseni maalumu.
“Wasanii wanahitaji sapoti ya kila aina. Wanafaa kuungwa mkono asilimia 100. Tunafaa kuwaelimisha vijana jinsi wanavyoweza kupata pesa kupitia kazi zao za sanaa,” akasema Bw Wa Njoroge.
Agizo hilo liliwahitaji wasanii hao kupata leseni kukubaliwa kisheria kurekodi maudhui yao, na pia kuwasilisha video zao kwa KFCB kwa uchunguzi na uainishaji kabla ya wao kuzipachika kwa YouTube kwa ajili ya watazamaji na wasikilizaji wao.
Awali KFCB ilikuwa imetoa makataa ya siku 14 kwa wasanii hao kuhusu kupakia maudhui ya sauti na taswira kwenye chaneli zao bila leseni halali.
Pia, iliagiza watayarishaji maudhui kuwasilisha video zao kwa KFCB kwa uchunguzi na kuainisha kabla hazijashirikiwa kwa umma.
“Unaagizwa kwamba uzingatie kikamilifu matakwa ya Sheria ya Filamu na Michezo ya Jukwaani kwa kupata leseni ya kurekodi filamu zako, na kuziwasilisha kwa uchunguzi na uainishaji kabla ya maudhui hayo kuonyeshwa na kusambazwa kwa umma kupitia chaneli yako ya YouTube,” ilisema barua ambayo mmojawapo wa watayarishaji hao wa maudhui alitumiwa.
KFCB iliendelea kuwaonya wasanii hao iwapo wangekosa kutii maagizo ndani ya siku 14, wangechukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa masharti ya sheria husika.
“Tutawachukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Filamu na Michezo ya Jukwaani na sheria nyinginezo husika, bila kurejea kwako na hasara itakuwa kwako mwenyewe na utawajibikia makosa yako,” KFCB iliongeza.
Akijibu maagizo hayo, msanii Jackie Vickie almaarufu Awinja ambaye hakufurahishwa, aliikosoa KFCB kwa kumtumia barua hiyo wakati kumekuwepo na ongezeko la idadi ya watu wanaotayarisha maudhui na kupachika YouTube.
“Ukweli ni kwamba KFCB haijafikiria kukaa chini na waundaji wa maudhui, lakini badala yake imetutafuta moja kwa moja. Hii ni hatua inayofanya nia halisi kutiliwa shaka,” alisema Awinja.
Kwa upande wake Lawrence Macharia almaarufu Terence Creative, alijibu agizo alilopokea kwa kusema yeye hufanya vipindi vya kuhamasisha jamii.
“Wash Wash si ukweli. Ni kipindi tu ambacho mimi hufanya kuhamasisha Wakenya wasiibiwe… ni kuigiza tu…vitu vingi hapo ni vya kuwataka watu kuchangamka huku wakielimika,” alisema Terence Creative.