• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Korti yampa Nyashinski siku 14 kuwasilisha mkataba wa dili tamu ya Tecno

Korti yampa Nyashinski siku 14 kuwasilisha mkataba wa dili tamu ya Tecno

NA SINDA MATIKO

MAHAKAMA ya Milimani, Nairobi imempa mburudishaji Nyamari ‘Nyashinski’ Ongegu makataa ya siku 14 kuwasilisha mkataba wa dili tamu ya kuwa balozi wa bidhaa za kampuni ya kutengeneza simu aina ya Tecno.

Nyashinski kashtakiwa na kesi ya ukiukaji wa hakimiliki zake produsa Sam Eli kutoka Nigeria aliyemwandalia hiti ya ‘Wach Wach’ iliyotumika pakubwa kuipigia debe simu aina ya Tecno Camon 20 iliyoingizwa kwenye soko la Kenya na Tecno mwaka 2023.

Mei 2023, Nyashinski alisaini mkataba wa ubalozi na matangazo ya simu hiyo iliyoletwa sokoni na Tecno Kenya Limited ambayo ni tawi la Tecno yenye makao makuu nchini China. Ni mkataba unaoaminika ulimlipa mamilioni ya pesa Nyashinski.

Hata hivyo kulingana na produsa Sam Eli aliyeandaa  biti za wimbo huo na kuuanda hadi ukamilifu wake, Nyashinski hakumlipa stahili yake kutokana na dili hiyo aliyosaini na Tecno akiwa anafahamu bayana kwamba yeye pia ni mmoja wa mumiliki wa wimbo huo.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa kati ya Nyashinski na Sam Eli, kila mmoja wao anamiliki asilimia 50 ya hakimiliki ya wimbo huo wa ‘Wach Wach’ uliofanya vizuri sana ulipotoka mwaka 2022.

Sam Eli aliiambia mahakama mwaka 2023 kwamba baada ya kuona matangazo ya Camon 20 huku wimbo wa Wach Wach ukitumika kuipigia debe lengo likiwa ni kuizidishia mauzo, alijaribu kuwasiliana na Nyashinski kwa ajili ya kupata stahili yake lakini rapa huyo akamchunia.

Sam Eli aliambia mahakama kwamba alimwomba Nyashinski amweleze thamani ya dili hiyo aliyosaini na Tecno lakini msanii huyo akamkaushia jambo lililomlazimu kuelekea mahakamani.

Mwezi Februari 2024, mahakama ilimwamuru Nyashinski kuwasilisha stakabadhi za mkataba huo, kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa rasmi.

Aidha mahakama ilimwamrisha kuwasilisha ripoti ya mirabaha ambayo amekusanya kupitia wimbo huo wa Wach Wach pamoja na nyimbo nyingine ambazo produsa Sam Eli alimwandalia. Kazi hizo zikiwa ni ‘Too Much’, ‘Flower’, ‘Showman’, ‘Lucky You’ na ‘Top Form’.

Hata hivyo kesi hiyo ilipotajwa tena Jumatano mbele ya hakimu Selina Muchungi, mawakili wa Nyashinski waliwasilisha tu ripoti ya mirabaha ya nyimbo tatu ‘Flowers’, ‘Too Much’ na ‘Wach Wach’.

Aidha mawakili wa Nyashinski walidinda kuwasilisha mkataba wa ubalozi aliosaini na Tecno.

“Mkataba husika umefungwa na kipengele cha usiri kati ya mteja wetu (Nyashinski) na Tecno Limited. Kwa maana hiyo, hatuwezi kuuwasilisha mbele ya mahakama,” ikasema kampuni ya mawakili ya Humphrey na wenzake kumtetea Nyashinski.

Kwenye agizo lake jipya, Bi Muchungi aliamrisha mawakili wa Nyashinski, kuwasilisha mkataba huo ndani ya siku 14 bila kufeli tena.

“Korti inaamuru kwamba mkataba huo uwasilishwe ndani ya siku 14 na kwamba mshtakiwa atimize maelekezo mengine yote yaliyotolewa na mahakama hii. Kesi hii itatajwa tena Aprili 12, 2024,” Bi Selina alielekeza.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mamake Diamond amfosi kuoa

Serikali yasutwa kwa kunyima vyombo vya habari matangazo ya...

T L