• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Letoo akiri ‘kuangusha’ wageni kwa kuweka hema la 10,000 pekee arusini

Letoo akiri ‘kuangusha’ wageni kwa kuweka hema la 10,000 pekee arusini

NA FRIDAH OKACHI

MWANAHABARI Stephen Letoo amejibu wakosoaji wake wanaomwelekezea mishale mtandaoni kwa kuoa mke mmoja, tofauti na matarajio yao kuwa angeoa wake wengi.

Letoo anashikilia kuwa ‘mwenyekiti’ hafai kushambuliwa na wote waliokosa kuhudhuria arusi yake.

Akizungumza na Taifa Leo kabla ya kufunga safari ya kuenda kuanza fungate na mke wake, alisistiza kuwa atasalia kuwa “mwenyekiti wa wanaume walio kwenye ndoa za mitara na ambao hawapo”.

“Nimeona wengi wakilalamika mbona ikawa hivi… Kwanza wale wote wanaopiga kelele kwenye mitandao ya kijamii watasimamishwa mara moja. Si vizuri kumshambulia mwenyekiti, ikizingatiwa kuwa hao hawakuhudhuria hafla hiyo ambayo ilifanyika katika uwanja wa Ole Ntimama, Narok,” akasema Letoo.

Mwanahabari huyo hakuficha furaha yake kutokana na jinsi shughuli nzima ilivyofanyika.

Alisema alishangazwa na idadi ya watu waliojitokeza kwenye arusi yake.

Aliongeza kuwa kwenye mipango yake, alitarajia watu 10,000 pekee kuhudhuria ila ikawa tofauti

“Nilishangazwa na jinsi watu waliojitokeza, nilikuwa nimeandaa nafasi ya watu 10,000 tu kwenye mahema. Kufika kwenye uwanja, nilishangaa kuona ukiwa umejaa umati. Nilifurahi kuona jinsi watu walivyojitokeza lakini pia nikaona aibu kwa kutenga nafasi hiyo kwa watu wachache,” akasema huku akipongeza mashabiki wake kwa kujitokeza kushuhudia ndoa hiyo iliyofungwa kwa aina yake.

Wakati wa shughuli nzima ya kufunga ndoa, picha zilisambazwa katika majukwaa ya mtandaoni, baadhi ya watu, wanaume wakiwemo, wakidai mwanahabari huyo alikuwa akiwapotosha wanaume kwa kauli zake kuhusu ndoa za mitara huku kwa upande mwingine akikosa kutimiza ahadi aliyokuwa ametoa.

Hata hivyo, anasalia ngangari, akisema ataendelea kutetea maslahi ya wanaume kama hapo awali.

Letoo alifunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Irene Renoi, katika arusi ya kukata na shoka katika uwanja wa Ole Ntimama mnamo Aprili 20, 2024.

Arusi hiyo ilihudhuriwa na watu kadhaa mashuhuri, wakiwemo wanasiasa na wanahabari wenzake.

  • Tags

You can share this post!

Ni njia tofauti za upendo au mgawanyiko?

Wiyoni yaipa Lamu usasa mtamu

T L