• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 10:55 AM
Jinsi YouTube inavyoendelea kuokoa vijana kujitengenezea mkwanja na kubadilisha maisha yao

Jinsi YouTube inavyoendelea kuokoa vijana kujitengenezea mkwanja na kubadilisha maisha yao

NA WANDERI KAMAU

KUTOKANA na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini na duniani kote, vijana wengi wamekuwa wakitafuta njia mbadala za kujipatia riziki.

Kutokana na uwepo wa mtandao wa intaneti, wengi wao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kujitengenezea pesa, kupitia shughuli kama uuzaji bidhaa mitandaoni, kutumia umaarufu wao kutangazia bidhaa na mashirika mbalimbali, au hata kutengeneza video na kuziweka mitandaoni ili kutazamwa na watu.

Ijapokuwa kuna mitandao kadhaa ya kijamii ambayo imeibukia kuwa maarufu; kama vile Facebook, Instagram, WhatsAapp, YouTube, X, TikTok kati ya mingine, mtandao wa YouTube ndiyo umeibukia kuwa tegemeo kwa vijana wengi kujitengenezea pesa ama mkwanja kwa lugha ya mtaa.

Vijana kadhaa nchini wamejichumia mamilioni ya pesa kutokana na utengenezaji na upakiaji wa video kwenye mtandao huo.

Ili kuanza kulipwa kutokana na video anazopakia mtu katika mtandao huo, lazima awe na wafuatiliaji 1,000 na video zake ziwe zimetazamwa kwa jumla ya saa 4,000.

Kuna vijana kadhaa nchini ambao wamejitengenezea mamilioni ya pesa kwa kugundua ‘muujiza’ wa kutengeneza fedha katika YouTube.

Baadhi ya vijana hao ni Frederick Marwa almaarufu kama I_Am_ Marwa, dadake Diana Mwango almaaru Dee Mwango, na mwanadada Gertrude Juma almaarufu Miss Trudy kati ya wengine wengi.

Kwa Bw Marwa,33, aligundua  ‘muujiza’ wa YouTube alipoenda kufanya kazi ya ualimu nchini Colombia mnamo 2016, mara tu baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) katika eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu.

Kwanza, alifanya kazi ya uuzaji katika benki moja jijini Nairobi, ijapokuwa mshahara aliokuwa akilipwa haukuwa ukimtosha.

“Nilipata nafasi ya kusafiri Colombia kuwa mwalimu wa Kiingereza. Baada ya kukumbwa na matatizo ya kifedha pia nikiwa katika nchi hiyo, nilianza kurekodi video na kuziweka katika mtandao wa YouTube. Nilikuwa nikifanya hivyo ili kujifurahisha. Sikujua kwamba mtu anaweza kuanza kutengeza pesa kupitia mtandao huo,” akasema Bw Marya.

Baada ya kugundua ‘muujiza’ huo, Bw Marwa aliacha kazi yake ya ualimu na kuegemea ‘kazi’ ya YouTube. Kwa sasa, anasema amekuwa akirekodi video na kuzipakia katika mtandao huo kwa muda wa miaka saba.

“YouTube imenifanyia maajabu. Ninaishi maisha ambayo singedhani ningeishi nikiwa mtoto,”  akasema.

Anasema kuwa kufikia sasa, amesafiri katika zaidi ya nchi 70 kote duniani kutokana na pesa ambazo amekuwa akipata kupitia YouTube.

Kando na hilo, amefanikiwa kuwajengea wazazi wake jumba la kifahari, analosema lilimgharimu mamilioni ya pesa.

Zaidi ya hayo, majuzi alimaliza kujijengea kasri la kifahari, katika kijiji cha Nyabohanse, Kaunti ya Migori.

Ingawa barobaro huyo haelezi kiwango halisi cha pesa ambacho alitumia kujenga jumba hilo, anasema gharama yake si chini ya Sh15 milioni.

“Nimetumia mamilioni ya pesa kujengea jengo hili. Uzuri ni kuwa, haya yote yanatokana na fedha ninazopata kutoka YouTube,” akasema Bw Marwa, ambaye kwa sasa ana wafuatiliaji zaidi ya 500,000.

Hali ni kama hiyo kwa dadake, Diana Mwango.

Anasema kuwa alishawishika kujitosa kwenye utengenezaji video na kuzipakia YouTube, baada ya kuona mafanikio ya kakake.

Anasema aliamua kuwa ‘YouTuber’ mara tu baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Moi, mjini Eldoret mnamo 2018.

Kwa sasa, mwanadada huyo ana wafuatiliaji zaidi ya 400,000 katika YouTube, huku akifanikiwa kumiliki mali kama mashamba, ploti na hata majumba ya kukodisha.

Anasema amefanikiwa kusafiri zaidi ya nchi 40 kote duniani.

Simulizi ni iyo hiyo kwa Miss Trudy.

Licha ya kusomea uanahabari katika Chuo Kikuu cha St Paul’s, Kaunti ya Kiambu, aliamua kujitosa kwenye utengenezaji video katika YouTube, baada ya kuona mafanikio ya vijana wengine wanaotengeneza video katika sehemu tofauti duniani.

“Kutokana na YouTube, nimeweza kuijengea familia yangu, kumnunulia gari kakangu, kununua majumba ya kukodisha, kusafiri zaidi ya nchi 30 kote duniani kati ya mengine,”akasema.

Anasema kuwa wazazi hawafai kuwazuia wanao kufuata ndoto zao.

“YouTube ni mwajiri kwa vijana,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Namna ya kuepuka ugonjwa wa macho mekundu

Wenyeji mjini Kenol kuchanga Sh200,000 kuburudisha polisi

T L