Mazishi ya Brian Chira yadhihirisha ushawishi mkubwa wa mitandao ya kijamii
NA WANDERI KAMAU
MAZISHI ya ‘tiktoker’ Brian Chira yaliyofanyika Jumanne katika eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu, yameonyesha nguvu ambayo mitandao ya kijamii katika ulimwengu wa sasa.
Ijapokuwa Chira alikuwa kijana wa umri wa miaka 22 pekee, umaarufu na ushawishi mkubwa aliokuwa nao katika jamii–hasa kwa vijana wenzake–ulidhihirika wazi wakati wa mazishi hayo.
Kutokana na umati mkubwa katika mazishi hayo, baadhi ya watu wameufananisha umaarufu wa Chira na ule wa mwanasiasa maarufu na mwenye ushawishi nchini.
Kulingana na waliohudhuria, umati uliokuwepo haukuwa chini ya watu 5,000.
“Kisio langu ni kuwa idadi ya watu waliojitokeza katika hafla hiyo ya mazishi ilikuwa zaidi ya 5,000. Wengi wao walifahamu kuhusu kifo chake kupitia mitandao ya kijamii,” akasema Bw Meshack Wanyonyi, ambaye ni miongoni mwa waombolezaji waliokuwa wamehudhuria mazishi hayo.
Kando na watu waliohudhuria mazishi hayo, kuna wale waliokuwa wakiyafuatilia kwa njia ya mitandao ya kijamii, kwani yalikuwa yakipeperushwa moja kwa moja na mabloga waliofika pale na kutundika hema.
Akaongeza: “Haikosi kuwa karibu watu 30,000 au zaidi waliyafuatilia kutoka sehemu tofauti nchini na ulimwenguni kupitia mitandao. Hii ni ikizingatiwa wengi walikuwa wakiyapeperusha moja kwa moja kupitia mitandao tofauti.”
Kando na vijana, baadhi ya wanasiasa na wanamuziki walifika katika mazishi hayo.
Mbunge Peter Salasya (Mumias Mashariki) na mwanamuziki Otile Brown ni miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii ambao walihudhuria mazishi hayo.
Kwenye mazishi hayo, Bw Salasya alitoa mchango wa Sh40,000 kuisaidia familia ya marehemu.
Lakini tangu Chira alipogongwa na gari na kufariki, michango imekuwa ikiendelea ambapo jumuiya ya TikTok ilisaidia kuchangisha zaidi ya Sh8 milioni kumsaidia nyanyake kununua shamba na kujenga nyumba.
Kutokana na hali hiyo, wadadisi wanasema kuwa ni dhahiri kwamba mitandao ya kijamii imethibitisha umaarufu wake, athari na ushawishi mkubwa iliyo nayo katika jamii.
Kulingana na Prof Levi Obonyo, ambaye ni mhadhiri wa somo la mawasiliano, umaarufu wa mitandao ya kijamii unafaa kuzifungua macho taasisi muhimu kama serikali, sekta ya kibinafsi na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika mitandao hiyo.
“Bila shaka, kile kimedhihirika ni kuwa mitandao ya kijamii ina uwezo wa kuleta mageuzi makubwa katika jamii kwenye nyanja tofauti; kama vile masuala ya kisiasa, uongozi au kiuchumi,” akasema Prof Obonyo, kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Anasema kuwa matumizi ya mitandao hiyo yameleta mageuzi makubwa ya kijamii, kiuchumi na muhimu zaidi, kisiasa, katika mataifa tofauti duniani, hivyo Kenya haifai kupuuza ushawishi wa mitandao hiyo katika kuleta mageuzi tofauti.
“Kile mitandao ya kijamii imedhihirisha ni kuwa watu wanaweza kuungana kutekeleza na kutimiza jambo fulani bila kujali mipaka au tofauti zilizopo baina yao, kama vile rangi, tamaduni, dini au hata ukabila,” akasema.