Miguna Miguna: Simba kwa mapenzi anatulia
NA FRIDAH OKACHI
WAKILI Miguna Miguna ambaye kauli zake ni za kumkemea yeyote anayejaribu kujihusisha na ukiukaji Katiba, amepakia mtandaoni akiwa amemkumbatia mkewe na kufichua kwamba ni miaka 23 sasa wawili hao wakidumu katika ndoa iliyobarikiwa.
Kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter), wakili Miguna alichapisha picha hiyo adimu na kusema kwamba wengi huenda wasifahamu lakini ukakamavu wake ni kutokana na nguvu za mke wake ambaye alimtaja kama nguzo thabiti.
Dkt Miguna alisema kwamba japo mkewe si mtu wa kuongea sana wala kuonekana katika mitandao ya kijamii, kile wengi hawafahamu ni kwamba ni mtu ambaye amechangia mafanikio mengi katika maisha yake katika kipindi cha miaka 23 ambacho wamekuwa kwenye ndoa.
“Miaka 23 kama mwamba wangu thabiti. Mtu mnyamavu. Asiyeyumba. Mwanamapinduzi!” aliandika Dkt Miguna.
Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wanamjua tu Dkt Miguna kuwa ni msomi aliye na msimamo mkali wa kufokea yeyote asiyejua maana ya kutii sheria. Mwonekano wake kwa wengi ni wa simba mkali anayetaka haki itawale.
Mnamo Jumatano, Dkt Miguna alimcharukia Rais William Ruto, akimuonya kwamba hakuna hata dikteta anayeweza kushinda vita akianza kufarakana na Idara ya Mahakama.
“Hakuna anayeshinda vita dhidi ya Idara ya Mahakama na mkondo wa sheria… Hivyo Rais @WilliamsRuto: hata usitafakari, kuota, au kuwazia hilo. Huu ni ushauri wa kirafiki. Puuza kwa hasara yako,” akaandika Dkt Miguna.
Hayo kando, kwa wale wanaodhani kwamba simba ni mkali sana, wajue kwa mapenzi anatulia. Ndicho alichofanya Dkt Miguna kwa kumposti mkewe huyo.
Chapisho hilo likiwa tofauti na ubwatukaji kwenye mitandao ya kijamii, wanamitandao walishiriki na kumpa hongera.
Aliyekuwa kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) Dkt Roselyn Akombe alimpa hongera na kumtakia mema kwenye ndoa yake.
“Hongera na heri ya Mwaka Mpya,” aliandika Dkt Akombe.
Naye Atieno Otieno alichangia na kusema kuwa wakili huyo huwa mkweli katika taasisi ya ndoa.
“Unatoa ukweli kwenye taasisi hiyo na kuwapa tumaini vijana walio kwenye ndoa. Ni hatua nzuri sana na hongera,” alisema Atieno Otieno.
Lakini Murgor Frank DAWA alichangia kwa ucheshi kwa kumweleza wakili huyo kwamba anapaswa kuagiza chakula na si kupiga stori.
“Hongera… Lakini ni vyema uagize chakula… ama mnakula stori?” alisema Frank DAWA.
John wa Kmb alichangia na kushangaa jinsi mwanasiasa na wakili huyo huwa lijapo suala la mapenzi.
“Kumbe unajua kupenda hivi double M?” akauliza John wa Kmb.
Mchangiaji mwingine–Peter Kithela Gachamba– naye alifikiria kuwa picha hiyo ni ya baba na mwanawe.
“Kusema ukweli, nilifikiri ni mwanawe wa kike. Ghee Whez! Mke wako ni mdogo kwa muonekana na mrembo. Hongera jenerali,” aliandik Gachamba.