Mike Rua: Mimi ndiye ‘Big Daddy’ wa Mugithi wengine wakijiita wafalme
Aidha, anajua sana kuleta uwiano na mlingano wa kipekee kati ya sauti ya ala na maneno ya wimbo.
Anatambulika bila mabishano kama ‘Big Daddy’ wa mtindo huo na hakuna yeyote hadi sasa ambaye ameelezea nia ya kumng’atua kutoka ubabe huo.
Hii ni kwa sababu mtindo wake wa kuchapa shoo ni wa kipekee ambapo mara nyingi hawezi akacheza saa za kabla watoto kulala.
Rua aliambia Taifa Leo kwamba “yenyewe mimi ni Daddy wa Mugithi”.
“Hakuna yeyote nishawahi kusikia akitaka tubishane kuhusu hilo. Wanabishania majina ya kawaida kama mfalme…” asema Rua.
Kuhusu mtindo wake wa kutumia lugha ya watu wakomavu katika ngoma zake kiasi kwamba hawezi akatumbuiza katika hafla ya wokovu au ya kifamilia ambapo rika zote ziko, Rua anasema kwamba “mimi sijaokoka na sijifanyi kuwa muungwana ndipo nikupendeze”.
“Mimi ni wa Mungu na hata kivyangu huwa najihisi kama aliye katika njia sahihi isipokuwa mambo madogomadogo tu ambayo yatalainika niwe kwa njia hiyo ya wokovo huko ambako sijaokoka,” asema msanii huyo.
Rua anasema kwamba “vile wewe hunichukulia sio hoja, uko na uhuru na sikushawishi ubadili”.
Anasema ni haki ya mtu kumpenda au kumchukia.
“Mimi niko na mashabiki wangu wa kipekee na sio wachache na hao ndio wamenijenga na kunifanya nilivyo na nawashukuru si haba,” asema.
Anaongeza kwamba ukiingia kwa YouTube na umsake huko na usanii wake utaona jinsi ambavyo nyimbo zake zinafuatiliwa sana.
“Bila shaka utaelewa kwamba wewe ukiwa kwa hukumu zako za kujifanya mtakatifu, tuko wengi upande huu mwingine,” asema.
Aidha, mtindo wake wa kupiga gitaa ni wa kipekee na wasanii wengi huwa wamekubaliana kwamba yeye ni mwalimu wa kuheshimiwa tu.
Lakini kumekuwa na hofu kwamba Rua huenda akizeeka kukose wa kurithi mtindo wake kwa kuwa hakuna ambaye amejitolea kuwa na ujasiri wa kuchapa shoo jinsi yeye hupakia zake.
“Ni vigumu sana. Kwanza sio wengi wanaweza kuwa na ujasiri wa kutaja maneno ambayo Rua hutaja. Pili, sijui kama kuna yeyote anayeweza akapata ujuzi wa kucharaza gitaa kama yeye hata akipewa miaka 100 ya kufanya mazoezi. La tatu, siamini kwamba kuna yeyote anayeweza akachanganya hayo mawili na aambatanishe na ubunifu wa Rua katika shoo zake. Ni wa kipekee tu,” asema Ras Munjus ambaye hupewa mawaidha ya showbiz na Rua.
Ras Munjus anasema kwamba “licha ya kuwa mimi ni mwanafunzi wa Rua, niko na uhakika kwamba kuwa kama yeye ni vigumu na haiwezekani”.
“Rua hucheza nyimbo za karibu lugha zote hapa nchini na pia hutesa ndani ya zile za injili na za ushauri bila kutatizika huku mwingiano wake na ala za muziki ukiwa wa kipekee kiasi kwamba ni kama kitu cha kiroho,” asema Munjus.
Huku wengi wakiogopa kumsikiliza Rua kwa upande mmoja, nao wengine wengi kwa upande mwingine wakisaka ngoma na shoo zake, yeye anasema “mjienjoi kwa kuwa niko hapa kujaza pengo ambalo wengi huogopa”.
Huku akielekea umri wa miaka ya 50 na bado akiwa na msukumo wa aina hiyo katika shoo zake, wengi huwaza jinsi watoto wake humchukulia wakimsikiza baba yao katika usanii wake.
“Kwani kuna mtoto wako nimeambia aniite baba?” afoka.
Aidha, Rua yuko na majirani ambao wanamjua vyema na pia mamake mzazi bado ako katika uhai na wengi hujiuliza kuhusu vile hujihisi akitembea nyumbani kwao.
“Mimi sijakuomba nikuje kwenu…Haya maisha ni mafupi na kuna yale ambayo sisi wote tunakimbizana nayo katika njia na mikondo tofauti. Tutafika kwa Muumba wetu kuhukumiwa, kwa sasa acha tupige shoo,” asema.