Mimi si maskini eti ndio naanzisha kanisa, nina gari la V8, asema mhubiri Sammy Irungu
NA WANDERI KAMAU
SIKU chache baada ya kuanzisha kanisa lake katika mkahawa mmoja jijini Nairobi, mwanamuziki Sammy Irungu sasa amepuuza vumi kwamba alichukua hatua hiyo kama njia ya kujipatia pesa.
Mwanamuziki huyo alifanya ibada yake ya kwanza katika kanisa hilo jipya kwenye mkahawa wa Blue Springs, ulio katika barabara kuu ya Nairobi-Thika, Jumapili, Februari 4.
Ikizingatiwa kuwa watu maarufu (celebs) katika ukanda wa Mlima Kenya wamekuwa wakianzisha makanisa yao, Bw Irungu alisema kuwa “hajasombwa na wimbi hilo”.
Mara tu baada ya ibada hiyo, mwanamuziki huyo aliwashambulia vikali watu ambao wamekuwa wakieneza vumi kwamba alianzisha kanisa hilo ili kujitajirisha, badala yake akisema kwamba “amekuwa akipata pesa za kutosha kutokana na muziki wake”.
“Kwa wale wanaosema nimeanzisha kanisa ili kujitajirisha, huo ni uvumi mtupu. Nimekuwa nikipata mapato mazuri kutoka kwa uimbaji wangu. Pili, mimi ni mwanamuziki wa kipekee wa nyimbo za Kikikuyu ambaye wimbo wake umefikisha mitazamo 17 milioni katika mtandao wa YouTube. Nyimbo zangu zina milioni 12 , milioni 10…sasa ni njaa gani inayoweza kunisukuma kuanzisha kanisa langu? Nimejenga kwangu, nina gari aina ya V8. Si ukosefu wa pesa ambao umenisukuma kuanzisha kanisa. Ni mwito wa kueneza injili,” akasema Bw Irungu.
Kauli yake inajiri baada ya baadhi ya watu kudai kwamba watu maarufu katika eneo la Mlima Kenya wanatumia umaarufu huo kuanzisha makanisa ili kujitajirisha.
Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya ‘macelebs’ ambao wameanzisha makanisa yao ni Mcheshi Muthee Kiengei, mwanamuziki Isaac Kahura, Paul Mwai kati ya wengine.
Bw Kiengei (maarufu kama Kaasisi Ben Gathungu) alianzisha kanisa la Jesus Christ Compassion Ministries (JCM) mwaka uliopita, baada ya kudai kufurushwa kutoka kanisa la African Independent Pentecostal Church (AIPCA). Kanisa lake liko katika eneo la By-Pass, Ruiru, Kaunti ya Kiambu.
Ikizingatiwa kanisa hilo limepata ufuasi mkubwa kwa muda wa miezi michache tu, wafuatiliaji wa burudani wanasema kuwa huenda hilo ndilo linalowapa msukumo ‘macelebs’ wengine katika eneo hilo kuanzisha makanisa yao.