Miracle Baby wa muziki wa kidunia aapa kumtumikia Mungu
NA FRIDAH OKACHI
MWANAMUZIKI wa Gengetone, Peter Mwangi almaarufu ‘Miracle Baby’ amefichua nia yake ya kuwa mhubiri pindi tu atakaporuhusiwa kuondoka hospitalini.
Msanii huyo amekuwa akiugua kwa muda mrefu, hali iliyolazimu madaktari kumfanyia upasuaji mara tatu kurekebisha tatizo la utumbo.
Katika video mojawapo akiwa na mamake, na ambayo ameipakia mtandaoni, Miracle Baby amesema zingatio lake ni kumtumikia Mungu baada ya upasuaji wa tatu kukamilika.
Baba huyo wa watoto watatu pia aliwashukuru mashabiki waliofanikisha upasuaji huo kwa hali na mali. Baadhi walitoa michango yao.
“Bwana Asifiwe! Nikitoka hapa nitakuwa pasta na nitahubiri Neno la Mungu,” akasema Miracle Baby.
Mnamo Februari 6, 2024, mwanamuziki huyo alifanyiwa upasuaji wa tatu ambao ulisaidia kurejesha hali yake ya kawaida.
Mapema mwaka 2024, mpenziwe ambaye pia ni mwanamuziki, Carol Katrue, alimwombea Miracle Baby.
“Anaenda kufanyiwa upasuaji wa tatu, tunahitaji maombi yenu,” alisema Katrue katika ujumbe aliopakia mtandaoni.
Baadaye alieleza mashabiki kuwa upasuaji uliendelea vizuri na akamshukuru kila mmojawapo aliyesaidia Miracle Baby kwa hali na mali.
“Asante Mungu kwa upasuaji uliofaulu lakini endeleeni kumuombea,” Katrue aliandika kupitia Insta Stories.
Mnamo Februari 11, 2024, Katrue aliandika ujumbe mwingine mtandaoni kuomba mashabiki msaada wa pesa, takriban Sh1.6 milioni ili kulipa bili ya matibabu hospitalini.
Tatizo hilo lilianza mwaka 2018 alipofanyiwa upasuaji wa kwanza na kuambiwa arejee mwaka 2022.
Mwaka huo (2022) alitafuta mawaidha kutoka kwa hospitali nyingine mjini Naivasha na kushauriwa atumie dawa kupunguza makali ya uchungu.
Lakini tena 2024, ugonjwa huo ulimzidia na kufahamishwa kuwa lazima angefanyiwa upasuaji mwingine.