Bambika

Mkome kutusi ‘babymama’ na mke wangu – Mulamwah

Na FRIDAH OKACHI July 27th, 2024 2 min read

MCHESHI David Oyando almaarufu Mulamwah, amewataka mashabiki wa mitandao ya kijamii, kuunga ‘babymama’ wake Caroline Muthoni almaarufu Carol Sonnie, pamoja na mke wake Ruth K, kwa kazi wanayofanya mitandaoni ili kujipatia riziki ya kujiendeleza kimaisha.

Katika mahojiano, mcheshi huyo aliwataka mashabiki wao kukoma kurusha vijembe vya matusi ambavyo alieleza huwatatiza wawili hao.

“Mtandaoni kuna mambo mengi yanaendelea, kuna timu upande huu na ule. Matusi ni ya nini?” aliuliza Mulamwah.

“Nataka, hawa wanawake wawili wajijenge kwa kupata riziki kupitia hiyo mitandao. Naomba mashabiki wawasaidie ili kila mmoja wao akue kimapato. Haina haja nyinyi mwendeleze matusi kwao. Adui wa mwanamke asikuwe mwanamke tena,” aliongeza Mulamwah.

Aliongeza kuwa baadhi ya matusi hayo hufanya wazazi wao kupatwa na huzuni.

“Unaporusha cheche za matusi kwa hawa wanawake wawili, kumbuka sio wao tu wanapatwa na matatizo ya kiakili, bali pia wazazi wetu wanahuzunika,” alieleza.

Mulamwah,31, alisema wito wake wa kutaka warembo hao kukosa kudhalilishwa mitandaoni ni baada ya mzazi mwenza (Carol Sonnie) baada kutoa habari kuwa hana chuki naye.

“Kila wakati nimekuwa nikilaumiwa mimi ndiye humkosea kila ninaposema pale mitandaoni. Juzi kwenye mahojiano fulani alisema hana chuki nami na ndio maana nasema tuache chuki na uhasama,” aliongeza.

Baba huyo wa watato watatu alisema kuwa tayari ana amini kukutana na aliyekuwa mpenziwe wa zamani kuhakikishia ulimwengu wako sawa.

“Hii wiki lazima tutakutana na Sonnie ili mjue tuko sawa. Na kama hatutakutana mjue kuwa mambo si sawa.”

Mulamwah ambaye siku za hivi karibuni alifanya sherehe ya kufichua sura ya mwanawe wa kiume na kufichua kuwa kifungua mimba wake ana umri wa miaka mitatu, alieleza sababu ya kukosa kujieleza kwa nini waliachana na ‘babymama’ Carol Sonnie.

“Wengi hamjui kuwa tulitengana naye alipokuwa mjamzito na miezi saba au nane. Nilimuahidi nitajukumika lakini tukawa tumejadiliana ni wakati upi tutafahamisha ulimwengu. Miezi sita baadaye akasambaza mitandoni. Kila mmoja akanichukia na kunichukulia mbaya.”

 “Nilianza kukasirika, nikaanza kujibu kwa kuchapisha vitu ambavyo havikuwa vinafaa. Ninaamini Mungu alinishikilia, ikawa sikuposti kila kitu kwani vikisemwa, vitaathiri vibaya maisha ya watu wengine na kuchukuliwa vibaya,” alisema Mulamwah.

Mulamwa alibainisha kuwa matukio yaliyofuata baada yaa chapisho lake, hayajakuwa mazuri kwani yeye na Carol walipitia unyanyasaji mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mtoto wao.