Mrembo wa kusaka mamilioni kwa mahindi aona dalili za ndoa 2027
NA MWANGI MUIRURI
MWANAMKE aliyeapa kwamba ataolewa tu baada ya kuwa milionea katika kilimo cha mahindi, sasa anasema fatalaiza ya ruzuku kutoka kwa serikali imeimarisha matumaini ya ndoa hiyo kuwa mwaka 2027.
Bi Grace Wangechi Kamande,28, kutoka katika kijiji cha Gatitika kilichoko Kaunti ya Kirinyaga, alizua msisimko mwaka 2023 alipotangaza kwamba hangekubali uchumba kabla ya kuwa milionea katika riziki yake ya kilimo cha mahindi.
Bi Kamande hupanda mahindi katika shamba la babake la ukubwa wa ekari mbili na kisha kuyavuna yakiwa mabichi na kuyauza.
Sasa, anasema kwamba kuna matumaini makuu ya kuafikia ndoto yake kabla hata ya mwaka 2027.
“Ninasema hivyo kwa sababu fatalaiza iliyokuwa ikinitatiza kwa bei sasa imeteremshwa na serikali kutoka Sh7,000 hadi Sh2,500,” akasema Bi Kamande.
Alisema pesa ambazo anaokoa kutoka kushuka bei huko anazielekeza katika gharama za wafanyakazi na pia katika kununua gesi ya kutoa maji ya kunyunyizia maji.
“Ilivyo ni kwamba, kwa sasa kiwango cha faida kimepanda kwa asilimia 30 kutokana na fatalaiza hiyo na pia kukumbatia utumizi wa gesi kupiga maji ya unyunyiziaji badala ya dizeli,” akasema.
Bi Kamande alisema kwamba “tukifunga mwaka wa 2023 nilikuwa nimepata faida ya Sh200,000”.
Baada ya fatalaiza hiyo ya ruzuku kuingia na pia kukumbatia kwake kwa teknolojia ya gesi kupiga maji, “nimefanya ukadiriaji wangu wa faida ya mauzo ya mwezi wa Machi na kupata nitakuwa na Sh300,000 kama faida”.
Bi Kamande anaongeza kwamba “ukadiriaji wangu wa kina ni kwamba kabla ya mwaka wa 2025 nitakuwa nimejinunulia gari langu la kusafirisha mavuno yangu hadi sokoni”.
Anasema kwamba “nitanunua gari aina ya pick-up ya Sh800,000 na hapo nitakuwa nimepata afueni ya kutegemea madalali ambao huitisha dau la juu mno”.
Alisema kwamba “nikipata gari langu la kusafirisha mavuno yangu hadi sokoni nitakuwa nimejihakikishia nyongeza ya pato kwa zaidi ya asilimia 50 na kabla ya 2027, niwe milionea na ambaye ataingia kwa ndoa kuzidisha riziki ya kilimo”.
“Nilianza kilimo hiki mwaka wa 2020 janga la Covid-19 liliponiondoa jijini Nairobi nilikokuwa nikisuka watu nywele,” anasema.
Anasema kwamba katika harakati zake za kuchumbiana, alikutana na mwanamume ambaye alimpa mtaji wa kujipa riziki mashinani alikotorokea maradhi hayo.
“Kwa kuwa hatukuwa tumeafikiana kuoana, nilichukua mtaji huo wa Sh250,000 na nikaingia katika shamba la babangu ambapo nilianza kufanya kilimo hicho,” asema.
Bi Kamande anasema kwamba “msimu wa kwanza ulinipeleka visivyo kwa kuwa baada ya kulima shamba, gharama za fatalaiza na usaidizi wa vibarua na kisha nikanunua mbegu, nilipata faida ya Sh2,000 pekee”.
Baada ya kungoja miezi mitatu ili mahindi yawe tayari kwa soko, alivuna takriban mabichi 10,000 ambapo bei sokoni kwa kila hindi lilikuwa Sh8.
“Mtaji wangu uliteremka hadi Sh120,000 na nilijua nilikuwa nakodolea macho kufilisika. Ndipo nilipata ushauri kutoka kwa wataalamu wa kutengeneza fatalaiza ya Yara na wakaniwezesha kuingia katika kilimo cha unyunyiziaji maji,” asema.
Kupitia bidii yake, Bi Kamande aliweza kupanga ratiba ya kuwa na takriban mahindi mabichi 50,000 sokoni kila mwezi.
“Wakati wa kiangazi huwa ndio bora wa biashara hii kwa kuwa bei kwa kila hindi hupanda hadi Sh30 huku wakati wa mvua bei hiyo ikishuka hadi Sh5,” akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.
Aliitaka serikali izidi kuteremshia wakulima gharama za uzalishaji ili viwango vya faida viongezeke.
Bi Kamande alisema kwamba kuna matumaini makuu kwamba sekta ya kilimo-biashara ndiyo itazindua awamu mpya ya mamilionea katika miaka ya hivi karibuni.