Bambika

Msanii wa muziki wa Agikuyu atoa kibao kukemea walafi wa mali za wajane, mayatima

June 12th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

MSANII kutoka Mlima Kenya kwa jina Bw Maina Kangoma, amewajibikia balaa iliyokita mizizi katika jamii za eneo hilo ya kupokonyana urithi kupitia utimuaji wa wajane na mayatima pamoja na mauaji.

Katika ngoma yake mpya ya ‘Wakinya Mere’ (Ukifika Waambie), Kangoma anaimba kwamba yeye ni mwathiriwa wa njama hiyo ambapo mama yake mzazi alitimuliwa alikokuwa ameolewa na ndipo baada ya kupambana na maisha ya dhiki sasa ana faraja ya kuachilia ngoma ya kukemea ukatili huo.

“Ukifika waambie mimi niko sawa, sina ubaya na wao kwa kuwa Mungu wangu bado amenilinda vizuri. Lakini la muhimu, uwaambie hayo waliotutendea si kitu. Mimi nilishawasamehe na hata mbinguni nikaweka ombi wasamehewe pia,” asema katika ngoma hiyo yake ya urefu wa dakika sita na sekunde 49 ikiwa kwa lugha ya Gikuyu.

Anawataka wenyeji Mlima Kenya wawaze na wawazue kuhusu hali kwamba “Damu ya ndugu yako ikililia watoto wake akiwa kaburini… Mkipitishia familia ya mtu wenu machungu ya kimaisha juu ya mali”.

Anasema katika ngoma hiyo kwamba hiyo tamaa huenda ikutwike matamu ya mali ya unyakuzi lakini ndani ya utamu huo kuna laana kali hata kuliko urogi.

Anasema kwamba kilio kimejaa eneo hilo ambapo mayatima na wajane wamejaa barabarani wakihangaika huku wengine wakiwa maskwota.

Anasema mali ya aliyeaga dunia huwa inagawanywa bila aibu wala utu nyumbani walikotoka na walioachwa huko.

Anasema kwamba baadhi ya jamaa hao husahau ule wema wote marehemu alikuwa amewatendea katika uhai wake baada ya tamaa ya mali kuwaingia.

“Hata baadhi ya machifu huhongwa hata kwa nyama ili kuweka saini kwamba familia za marehemu zitimuliwe hata kabla ya mwili kukatika shingo kaburini,” asema.

Anasema kwamba kuna hali moja aliyo na ufahamu wayo ambapo “chifu alichinjiwa ndio aweke saini kwamba mjane hakuwa ameolewa kihalali na mwendazake mumewe na hivyo basi kukosa uhalali wa kurithi”.

“Familia nyingi ziko tu sawa na nyinyi wakati mnakula na mnakunywa pamoja lakini shetani wa tamaa akishashuka, hayo yote huwa ni bure na watakutimulia watoto wako ndio wakugawe,” asema kwenye wimbo huo.

Bw Kangoma anasema “ile bahati iko ni kwamba Mungu huja kuwajali waja wake na mwishowe dhiki hizo huishia kuwa faraja kwa wengi ambao huzingatia bidii kiimaisha pasipo kujiingiza katika mizozo na waliowapokonya urithi”.

Msanii huyo anasema kwamba “hata ikiwa huwa chungu, wakati umejipata katika hali hiyo ya kuathirika na ulafi huo, lakini badala ya kuanza kupanga njama za kupigana na badala yake upambane na uishie kufaulu kimaisha, usiwahi kufikiria kulipiza kisasi”.

Asema, “Wakabidhi wao wote na tamaa zao kwa Mungu na usiwaombee mabaya ndio wasiishe kwa laana yao wakulaumu.”

Anashauri mwathiriwa kuwa na roho ya kuwasamehe “ndio hata moyo wako upate ule utulivu na raha ya kusherehekea ufanisi wako”.

Wimbo huo ambao kwa sasa umekuwa kama wa taifa kwa wenyeji, unalenga kuwapa wengi katika eneo hilo shinikizo za kukoma tamaa ya mali ya wanyonge katika familia, akisema kwamba “hata visa vingi vya mauaji vinatokana na hali kwamba waliopokonywa mali hurejea na kisasi huku wengine wakisaka nguvu za giza na kutwika jamii masaibu tele ya mahangaiko”.

Kuhusu muziki, anasema ndio sasa ameanza.

“Nitaingia katika jukwaa hili la utunzi na kurekodi ngoma zangu ili tusaidiane kuosha hii jamii yetu na taifa kwa ujumla, tamaa ya kukimbilia haki za wengine na kuzinyakua ili upate shibe lako wengine wakihangaika,” asema.

Anasema “ule ulafi tulio nao umevuka mipaka kiasi kwamba hata mimi mwenyewe unionavyo hivi ningekuwa mbele sana kiusanii lakini wanamuziki tajika ambao wengine hata ni maafisa wa polisi, walichukua ngoma zangu na wakazirekodi kama zao na hata baada ya kuvuna mamilioni na usanii wangu, hata ndururu moja hawakunipa”.

Anasema “pia hao nimewasamehe, nitawakabidhi kwa Mungu na mimi nizingatie tu yangu ya kujivumisha ndio nikifanikiwa nao wakififia, wasinirejelee wakisema niliwatafutia mikosi”.

[email protected]